Naibu Waziri wa Uchukuzi
na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye ameridhishwa na kasi ya upanuzi wa Bandari
ya Tanga baada ya kushuhudia kazi inayoendelea kufanyika kwenye bandari hiyo
wakati wa ziara yake mkoani humo
Nditiye amesema kuwa
tayari Serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 172 kwa ajili ya kupanua
bandari hiyo kwa kuongeza kina cha sehemu ya kupakia na kupakua mizigo; ujenzi
wa ghati na ukarabati wa ghala ili kuongeza uwezo wa bandari hiyo wa
kusafirisha mizigo na bidhaa mbali mbali ndani na nje ya nchi
“Tunategemea bandari hii
itakapokuwa imekamilika ndani ya mwaka mmoja itaweza kuhudumia mizigo mingi
sana kwa kushirikiana na bandari ya Dar es Salaam kwa sababu tunategemea iweze
kuhudumia meli mbili zenye uzito wa tani 35,000 kwa mara moja, itakuwa ni
bandari ya kisasa, kazi ya kwanza ya kuchimba kina imekamilika, sasa tunaenda
kununua vifaa na itaenda sambamba na ujenzi wa ghati kubwa lenye urefu wa mita
500, tumejipanga kutekeleza IIani ya CCM kwa kuhakikisha kwamba vitu vyote
tulivyoahidi, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Joh Pombe
Magufuli alivyoahidi, na CCM ilivyoahidi kwa wananchi vinatekelezwa kwa
wakati”, amefafanua Nditiye
Ameongeza kuwa mizigo
mingi iliyokuwa inakuja maeneo ya Kaskazini ikitoka nje ya nchi haitakuja tena
mpaka Dar es Salaam, itakuwa inaishia Tanga ili watu wa mikoa ya Arusha,
Kilimanjaro, Tanga wapate mizigo yao kutokea bandari ya Tanga kwa kuwa Serikali
imeimarisha reli, hivyo, mzigo ukishuka Tanga unaingia kwenye treni na kwenda
kwenye mikoa hiyo na nchi za jirani zisizopakana na bahari zitapata huduma ya
kusafirisha bidhaa na mizigo yao
Pia, ameipongeza Bodi,
Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na wafanyakazi wa bandari ya
Tanga kwa usimazi wao mzuri walioufanya kwa kuwa kazi ambayo Serikali
imetegemea imeanza kuonekana ya upanuzi wa bandari hiyo ikiwa ni pamoja na
kutoa ajira kwa watu wengi waishio Tanga kwa kazi ambazo sio za kitaalamu
Kaimu Meneja wa Bandari
hiyo, Juma Mohamedi Juma amesema kuwa Menejimenti ya Bandari ya Tanga iko
tayari kuchapa kazi na wanasimamia mradi huo ili uende vizuri na
utakapokamilika utaongeza uwezo wa bandari hiyo wa kuhudumia meli kwa urahisi,
kwa haraka na kupunguza muda wa kupakia
na kupakua mizigo na bidhaa ambapo itavutia wafanyabiashara wengi zaidi kutumia
bandari hiyo na utaweza kuhudumia eneo lote la nchi za Rwanda, Burundi na
Uganda ambapo mkataba wa kipindi cha mwaka mmoja ulioanza kutekelezwa mwezi
Oktoba mwaka jana umesainiwa baina ya TPA na mkandarasi wa kichina wa kampuni
ya China Harbour Engineering Company Ltd
kwa ajili ya upanuzi wa bandari hiyo
“Hadi sasa kazi ya
kuchimba ili kupanua kina cha bandari kwa ajili ya sehemu ya kupakia na
kushusha mizigo imefikia asilimia 96; kazi ya kuleta vifaa ambavyo vinatengenezwa
nje ya nchi na tukivileta nchini imefikia asilimia 20; na tupo ndani ya
mkataba, na kazi hii ikikamilika tutakuwa na kina cha mita 13 kwenda chini
tofauti na hapo awali tulikuwa na kina cha mita tatu tu, na tutakuwa na uwezo
wa kuhudumia meli zenye uzito wa tani 35,000 tofauti na hapo awali tulikuwa na
uwezo wa kuhudumia meli zenye uzito wa tani 1,200 na kuwa na sehemu ya kuweka
kontena 4,000,” amesema Juma
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, Martin Shigella ameishukuru Serikali kwa uamuzi wa kupanua bandari ya
Tanga kwa kuwa sasa wanajenga viwanda vingi hivyo upanuzi wa bandari hiyo
utapanua wigo wa kibiashara, itaongeza mapato ya mkoa na wananchi kujipatia
shughuli za kufanya za kuwaingizia kipato zitokanazo na shughuli za bandari.
No comments:
Post a Comment