Matokeo chanyA+ online




Monday, April 27, 2020

KATIBU MKUU DKT. CHAULA AKABIDHIWA OFISI RASMI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Zainab Chaula (wa pili kushoto aliyesimama mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na Menejimenti na wawakilishi wa taasisi za Sekta hiyo alipowasili kwa mara ya kwanza Wizarani hapo Mji wa Serikali, Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu anayestaafu, Dkt. Maria Sasabo 
 
Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Zainab Chaula, amewasili rasmi  Wizarani katika ofisi zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba, Dodoma kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa, baada ya kuhamishwa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Dkt. Chaula amesema kuwa amefurahi na kumshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kumhamishia Wizara hiyo  kwa kuwa anafahamu umuhimu na mchango wa Sekta hiyo katika maeneo mengine kwa kuzingatia kuwa amekuwa akitumia TEHAMA katika kutekeleza majukumu yake alipokuwa TAMISEMI na Wizara ya Afya
Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Maria Sasabo (wa kwanza kushoto) akimkabidhi Katibu Mkuu mpya, Dkt. Zainab Chaula nyaraka mbali mbali kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Sekta hiyo alipowasili ofisini kwenye Mji wa Serikali, Dodoma.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (wa kwanza kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula alipowasili Wizarani hapo, Mji wa Serikali, Dodoma, kujitambulisha baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Sekta hiyo
“TEHAMA itatutoa kwenye chagamoto, lazima tuwekeze na tuitumie kama fursa, suala sio wingi wa watu, kuwa na watumishi wengi, kwa kuwa mnaweza kuwa wengi ikawa vurugu, ila mnaweza kuwa wachache na mkafanya kazi vizuri, binafsi nimetumia TEHAMA kwenye sekta ya afya na TAMISEMI, nimekuja huku nimefurahi, nitaendelea kujifunza zaidi, nanyi ndio wataalamu, mjiamini, msiwe na hofu, watanzania tuna akili, uwezo tunao,” amesisitiza Dkt. Chaula

Katibu Mstaafu wa Sekta hiyo, Dkt. Maria Sasabo, akizungumza wakati anamkaribisha na kumkabidhi ofisi Dkt. Chaula, Dkt. Sasabo alisema kuwa Sekta ya Mawasiliano ni mtambuka, inategemewa na Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu mbali mbali ya kila siku ambapo tayari kuna Sera, sheria, miongozo na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa Sekta ikiwa ni pamoja na miundombinu ya mawasiliano ambayo inawezesha utendaji kazi wa mifumo ya kielektroniki nchini
 
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi, akimpongeza Katibu Mkuu wa Sekta hiyo anayestaafu, Dkt. Maria Sasabo (aliyeketi katikati) na kumkaribisha Katibu Mkuu mpya ofisini, Dkt. Zainab Chaula (wa kwanza kulia) Mji wa Serikali, Dodoma
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akizungumza na Katibu Mkuu mpya wa Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Zainab Chaula alipofika ofisini kwake, Mji wa Serikali, Dodoma kujitambulisha baada ya kuhamishiwa Wizarani hapo
Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alimweleza Dkt. Chaula kuwa Sekta hii imetekeleza vema majukumu yake katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2019/2020 na sasa wanajiandaa kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwenye Bunge la bajeti linaloendelea mjini Dodoma

Kamwelwe amemwagiza Dkt. Chaula kuhakikisha kuwa Sera ya Taifa ya Posta inahuishwa ili iweze kwenda na wakati kwa kuwa sekta ya posta imebadilika na Shirika la Posta limebadiilisha namna ya kufanya kazi na kuhudumia wananchi kwa kuwa linatumia TEHAMA kutoa huduma na kusafirisha vifurushi na vipeto kwa wateja
 
 Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Zainab Chaula, akijadiliana jambo na Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Elius Mwakalinga, alipowasili Wizarani hapo kuwa Katibu Mkuu wa Mawasiliano
 
Akisalimiana na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashata Nditiye mara alipowasili ofisini kwake kujitambulisha, Nditiye alimwarifu Dkt. Chaula kuwa Sekta ya Mawasiliano ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa taifa letu kwa kuwa sasa ni moja ya Sekta tano bora kwa kuongoza kuchangia pato la taifa na hata Bungeni maswali mengi yanayoulizwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za mawasiliano

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa amemweleza Dkt. Chaula kuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano viongozi wanafanya kazi kama timu moja bila kujali anasimamia Sekta ipi na mara nyingine amekuwa akishiriki kazi za Sekta ya Mawasiliano ikiwa ni pamoja na kujibu maswali Bungeni
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Zainab Chaula alipowasili rasmi baada ya kuhamishiwa Wizarani hapo, Mji wa Serikali, Dodoma
 
Na Prisca Ulomi, WUUM, Dodoma

Akizungumza na Menejimenti na wawakilishi wa taasisi za Sekta hiyo Wizarani hapo, Dkt. Chaula amesema kuwa anategemea kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi na wafanyakazi kwa kuwa kwenye kazi tunatengeneza upendo, marafiki na kuwa ndugu na sio maadui, tunafungua njia. Hivyo, amewataka kufanya kazi vizuri kama uko nyumbani kwako kwa ajili ya wengine

Pia, amewakumbusha kuendelea kuzingatia miongozo na maelekezo ya Wizara ya Afya ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ili kujilinda na maambukizi ya virusi vya Corona ambavyo ni janga la dunia ambapo kwa Tanzania Serikali imejitahidi na kujidhatiti kuhakikisha kuwa maambukizi yanaendelea kupungua na wagonjwa wanapona na amewataka wasiwe na hofu kwa kuwa Corona ni mafua tu.

No comments:

Post a Comment