Matokeo chanyA+ online




Wednesday, April 22, 2020

TUSHIKAMANE KATIKA VITA HII DHIDI YA JANGA LA CORONA – WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Askofu Alex Malasusa wa KKKT Jimbo la Mashariki na Pwani (kushoto), Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es salaam, Yuda Thaddeo Ruwaichi (wa pili kushoto), Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakari Zubeir (wa tatu kushoto) na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (wa nne kushoto) katika maombi ya pamoja kuhusu kukabiliana na tishio la ugonjwa wa homa kali ya mapafu – COVID – 19 kwenye viwanja vya ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam, Aprili 22, 2020.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika maombi ya pamoja kuhusu kukabiliana na tishio la ugonjwa wa homa kali ya mapafu – COVID – 19 kwenye viwanja vya ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam, Aprili 22, 2020. Kushoto ni Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es salaam, Yuda Thaddeo Ruwaichi na kulia ni Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Viongozi wa dini wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza katika maombi ya pamoja kuhusu kukabiliana na tishio la ugonjwa wa homa kali ya mapafu – COVID – 19 kwenye viwanja vya ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam, Aprili 22, 2020. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,  amesema ni lazima tushikamane kwenye vita hii kwani mshikamano  ndio utaleta ushindi katika kupambana dhidi ya janga la corona.



Waziri Mkuu amesema hayo wakati akizungumza katika Maombi ya Kitaifa ya kuliombea Taifa dhidi ya janga la corona yaliyofanyika katika viwanja vya Karamjee jijini Dar es salaam.



Waziri Mkuu amesema kuwa mpaka sasa jumla ya wagonjwa 284 wamethibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona ambapo kati ya hao wagonjwa 256 wanaendelea vizuri kiafya, huku wagonjwa 7 wakiwa chini ya  uangalizi wa karibu na wagonjwa 11 wamepona.





Aidha, ameongeza kuwa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) walikadiria kuwa kufikia mwisho wa mwezi Aprili, wagonjwa wangekuwa  zaidi ya laki tano ambapo mpaka sasa makadirio hayo hayajafikiwa, huku Jiji la Dar es Salaam na Zanzibar yakiwa  yanaongoza kwa maambukizi ukilinganisha na Mikoa mingine".



"Serikali tumeunda kamati ya Kitaifa yenye lengo la kufuatilia mwenendo wa ugonjwa huu, tumeunda kamati ambayo itaongozwa na Waziri Mkuu, nyingine ikiongozwa na Makatibu Wakuu, tumeunda pia timu ya Madaktari waliobobea katika utafiti"- amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.




No comments:

Post a Comment