Mkuu
wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo amewatahadharisha mafundi na vibarua wa
mradi wa ujenzi wa vihenge unaojengwa na serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa
Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) kuwa makini na ugonjwa wa homa kali ya mapafu
unaosababishwa na virusi vya Corona kwa kufuata maelekezo ya wataalamu afya
wawapo katika eneo la kazi na wanaporudi kwenye familia zao.
Mafundi na vibarua wakiendelea na Ujenzi wa Vihenge vya kuhifadhia na kusafisha mahindi katika eneo la viwanda kata ya Ntendo, Manispaa ya Sumbawanga. |
Amesema
kuwa afya ya kila mmoja ni muhimu kutokana na mchango wake katika kujenga nchi
na hivyo kuwataka kuwa makini kwa kunawa kila mara hali iliyopelekea kumuagiza
meneja wa mradi huo kwa niaba ya Wakala wa majengo nchini (TBA) Mhandisi mkazi
Haruna Kalunga kuhakikisha eneo hilo la kazi kunakuwa vifaa vya kutosha vya
kunawia maji na sabuni kwa kukanyaga kwaajili ya wafanyakazi na kuondoa ndoo zilizopo
ambazo koki zake hazina usalama.
“Afya
yako ni ya Msingi sana, na familia yako na sisi sote kwa ujumla wake, kwa maana
wewe mtu mmoja ukiugua Corona utaweza kuusambaza kwa watu wengi sana, na wote
hapa mnaweza mkafutika ndani ya wiki moja tu, sasa mtakuwa mmeiweka nchi mahali
pabaya na mradi wenyewe utasuasua, kwahiyo mjihadhari na ugonjwa huu hatari wa
Corona, lakini mchape kazi msiogope kuchapa kazi,” alisema.
Aidha,
alitoa pongezi kwa mkandarasi wa mradi huo Unia araj kutoka nchini Poland kwa
kusaidiana na mkandarasi mzawa Elerai kutoka Arusha pamoja na meneja wa mradi
huo TBA pamoja na mafundi wa mradi huo kwa kufanya kazi ndani ya wakati mbali
na hali ya hewa kutokuwa Rafiki kwa ujenzi huo na hivyo kuwataka kuongeza kasi
ili kukamilisha ujenzi huo ifikapo tarehe 9.3.2021.
“Ningependa
ratiba hiyo izingatiwe, tusirudi nyuma tuongeze kasi kwa kiwango ambacho mradi
huu tunataka umalizike mapema, utakuwa na manufaa makubwa sana kwasababu uwezo
wa kutunza nafaka zetu kimkoa utaongezeka kutoka tani 30,500 za sasa mpaka
kufika tani 55,500 utakuwa ni uwezo mkubwa, kwahiyo hata wakulima wetu
watahamasika kulima mahindi zaidi wakijua kwamba NFRA itaweza kuyanunua na
kuyahifadhi kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi,” Alisema.
Mhandisi Mkazi Haruna Kalunga (kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (mwenye kaunda suti nyeusi) katika eneo la ujenzi wa Vihenge. |
Kwa
upande wake Meneja wa Mradi wa TBA Mhandisi Mkazi Haruna Kalunga alisema kuwa
ujenzi huo utajumuisha majengo 13 ambapo ujenzi wa vihenge 6 vikubwa na vihenge
2 vidogo pamoja na miundombinu yake itachukua asilimia 70 ya mradi huku
asilimia 30 ikibebwa na majengo saidizi.
“Kuna
Jengo la utawala, kuna jengo la kupikia na kulia chakula, kuna jengo la
kutunzia vifaa na dawa, kuna jengo la maabara kwaajili ya upimaji wa hizo
sampuli ambazo zitakuwa zinaingia hapa, kuna vihenge 6 vikubwa na vihenge
vidogo kwaajili ya usafi vyenye jumla ya tani 20,000 na pia tuna ghala la
kuhifadhia mazao lenye uwezo wa kubeba tani 5,000,” alisema.
Bango la Ramani ikionesha namna eneo hilo la ujenzi wa vihenge hivyo vitakavyokuwa pindi mradi huo utakapokuwa umekamilika kwaajili ya matumizi. |
Kwa
mkoa wa Rukwa mradi huo utagharimu Dola za Kimarekani 6,019,399.00 wakati
mkandarasi huyo akifanya kazi katika mioa mingine ya Manyara na Katavi ambapo
jumla ya gharama yake ni $20,280,906.00 ambapo hadi sasa mkandarasi huyo
ameshalipwa $ 10,175,714.22.
No comments:
Post a Comment