Matokeo chanyA+ online




Thursday, April 16, 2020

MADAKTARI WATUMIA TEKNOLOJIA MPYA KUOKOA MAISHA YA WATOTO WANAOZALIWA UTUMBO UKIWA NJE


Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa mara ya kwanza Tanzania wamefanikiwa kuokoa maisha ya watoto wawili waliozaliwa wakiwa na tatizo tumbo kuwa wazi na utumbo kuwa nje kwa kitaalamu (Gastroschisis) kwa kutumia utaratibu (procedure) wa kuwavalisha mifuko maalumu (Silo bags) ambao hauhusishi mtoto kufanyiwa upasuaji wala kupewa dawa za usingizi.

Awali kabla ya kuwepo kwa teknolojia hiyo uwezekano wa   watoto wanaozaliwa tumbo wazi na utumbo nje kufariki ilikuwa ni asilimia 100 lakini kwa teknolojia hii uwezekano wa kupona ni asilimia 100.

Kabla ya teknolojia hii kuwepo watoto wenye tatizo hili ilibidi wafanyiwe upasuaji na kuvalishwa mifuko ya kawaida ambayo ufanisi wake ulikuwa mdogo na ulihusisha kupitia taratibu mbalimbali za upasuaji ikiwemo kupewa dawa za usingizi ambapo kutokana na uchanga wa watoto na muda ulikuwa unatumika kurejesha matumbo watoto walipata madhara   mbalimbali ikiwemo vifo.

Kuanzia sasa mtoto akizaliwa na tatizo hili atavalishwa mfuko maalumu unaotunza majimaji akiwa wodini ambapo kila siku watoa huduma watakua wanausukuma utumbo kurudi tumboni kwa vipimo maalumu na katika kipindi cha siku tatu hadi tano utumbo huo utakuwa umerudi ndani kwenye hali ya kawaida. Baada ya hapo mtoto atafungwa tumbo kwa njia maalumu ambayo haiusishi kushonwa na nyuzi.

Ili kuhakikisha huduma hii inapatikana katka maeneo mengi nchin, tayari Hospitali ya Taifa Muhimbili imechukua jukumu lake la kutoa mfunzo maalumu kwa Hospitali zote za Kanda za zilizopo Mkoa wa Dar es salaam kuhusu namna ya kuwapa huduma ya kwanza watoto wanaozaliwa na na tatizo hili kabla ya kuwapa rufaa ya kufika Muhimbili ambapo kwa sasa ndio sehemu pekee ambapo utaalamu huu unapatikana. Hospitali itaendelea kutoa mafunzo haya kwa Hospitali nyingine nchini.

No comments:

Post a Comment