Veronica Simba – Morogoro
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amefanya ziara
ya kushtukiza katika kituo cha kupoza umeme Msamvu na kuagiza kazi ya kufunga
kifaa cha kukata umeme (circuit breaker), ikamilishwe ndani ya siku moja ili
wananchi waendelee kupata huduma ya umeme.
Alifanya ziara hiyo jana Jumamosi ya Aprili 4, mwaka
huu akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) Dkt Tito Mwinuka, Meneja wa Mkoa wa Shirika hilo, Mhandisi FedGrace
Shuma, Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Ahmed
Chinemba na wataalamu mbalimbali kutoka wizarani, TANESCO na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA).
Dkt Kalemani alitoa maagizo hayo baada ya kujulishwa
kuwa changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara ambayo wamekuwa wakiipata
wananchi wa mji wa Morogoro hususan maeneo ya Mtibwa na Kilosa ni kutokana na
kuharibika kwa kifaa hicho kituoni hapo hali inayowalazimu TANESCO kufunga
kifaa kipya.
Waziri alitoa onyo kwa Msimamizi wa Kituo hicho,
Selemani Ibwe, kuwa kosa hilo lisitokee tena kwani tayari alikwishalitolea
maelekezo kwa Mameneja wa TANESCO nchi nzima.
“Hili ni onyo la mwisho kwa Mameneja wa TANESCO nchi
nzima. Mnatakiwa kuhakikisha mnakuwa na vifaa vya akiba katika vituo vya kupoza
umeme ili inapotokea hitilafu tatizo linarekebishwa mara moja badala ya kutumia
muda mrefu na kuwasababishia kero wananchi.”
Aidha, Waziri alitoa muda wa siku saba kwa wafanyakazi
wawili wanaosimamia kituo hicho cha Msamvu kuhamishia makazi yao maeneo ya
jirani ili waweze kushughulikia kwa wakati changamoto mbalimbali zinazojitokeza
katika kituo hicho.
Alisisitiza kuwa hilo pia ni onyo la mwisho kwani
alikwishatoa maelekezo husika kwa watumishi wote wanaosimamia vituo vya kupoza
umeme nchi nzima, kuishi katika maeneo yaliyo jirani na vituo hivyo.
Pia, Dkt Kalemani alitoa maagizo kwa uongozi wa
TANESCO mkoani Morogoro kukamilisha marekebisho yanayofanyika katika njia ya
kusafirisha umeme ya Mtibwa ndani ya siku tatu ili wananchi husika waendelee
kupata huduma ya nishati hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kituoni hapo,
Waziri Kalemani alifafanua kuwa hali ya kukatika kwa umeme ambayo imekuwa
ikitokea haisababishwi na ukosefu wa nishati hiyo bali ni kutokana na changamoto
za ki-usimamizi ambazo alisema ametoa maelekezo namna ya kuzitatua.
“Mathalani hapa Morogoro umeme uliopo ni wa kutosha
kwani kituo hiki kina uwezo wa kuzalisha megawati 88 wakati mahitaji ya
wananchi ni megawati 48 tu,” alifafanua.
Awali, kabla ya kutembelea kituo hicho, Waziri
Kalemani alizungumza na waandishi wa habari akiwa katika eneo la Dakawa,
takribani kilomita 100 kutoka eneo kunapotekelezwa mradi wa kufua umeme wa maji
wa Julius Nyerere (megawati 2,115) ambapo alitoa maagizo kwa wakandarasi wa
Mradi huo kutumia usafiri wa Reli katika kusafirisha mizigo badala ya kutegemea
njia ya barabara pekee.
Huku akiwa amezingatia miongozo ya wataalamu kuhusu kutoweka
mikusanyiko ya watu, Waziri alisema maelekezo hayo aliyoyatoa ni kutokana na
uharibifu wa barabara husika ambao umesababishwa na mvua zinazoendelea
kunyesha.
“Naipongeza Serikali kwani imejenga miundombinu mbalimbali tunayoweza kuitumia ikiwemo reli
ya TAZARA badala ya kutegemea barabara pekee hali inayoweza kusababisha
ucheleweshaji wa mradi.”
Akisisitiza, alisema Serikali haitakubali kuona Mradi
huo unacheleweshwa kwa kisingizio chochote hivyo akawataka wakandarasi husika
kuendelea kuchapa kazi.
Akieleza zaidi, alisema hata yeyé msafara wake umekwama
mahala hapo akiwa njiani kwenda kukagua Mradi huo lakini akasema atatumia njia
mbadala kufika eneo la Mradi siku inayofuata.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Regina Chonjo ambaye
alifuatana na Waziri Kalemani, alisema amewasiliana na watendaji kutoka Wakala wa
Barabara Tanzania (TANROADS) ambao ndiyo wenye dhamana na barabara hiyo na
kwamba wanatarajiwa kufika eneo husika kwa ajili ya kurekebisha kipande hicho
ili kuwezesha magari kuendelea kupita.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka
alisema shirika lake litashirikiana na TANROADS katika kuhakikisha njia hiyo
inakarabatiwa mapema na kuongeza kuwa hata Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa
Julius Nyerere atashirikishwa maana pia anawajibika kuchangia.
No comments:
Post a Comment