Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa akijadiliana jambo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu Bungeni |
Wizara ya
Afya, kupitia Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii inatarajia kutumia Jumla ya
shilingi bilioni 33.195 ili
kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii hususani zilizopewa kipaumbele kwa
mwaka wa fedha 2020/21.
Akiwasilisha Hotuba ya Wizara ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema katika mwaka wa
fedha 2020/21 Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii inatarajia kutumia kiasi hicho
cha fedha kwa lengo la kuimarisha huduma na mafunzo kwenye Taasisi za Ustawi na
Maendeleo ya Jamii, kukarabati makazi ya wazee, kujenga mahubusu za watoto na
kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Alisema
kuwa bajeti hiyo itasaidia kuimarisha Kujenga kumbi pacha na hosteli katika
Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ambapo jumla ya shilingi bilioni
2.7 zimetengwa, pia kuboresha utoaji wa mafunzo ya taaluma ya
maendeleo ya jamii ili kukidhi mahitaji ya soko sambamba na kukuza ujuzi wa
wahitimu ikiwemo kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kwa kutenga jumla
ya shilingi bilioni 6.6.
Maeneo
mengine yaliyotengewa fedha ni pamoja na ukarabati wa majengo na miundombinu
katika makazi ya wazee kwa shilingi milioni 400, ujenzi wa Shule ya
Maadilisho katika Mkoa wa Geita shilingi milioni 200, kuimarisha
ujenzi wa mahabusu ya watoto katika mikoa ya Kigoma na Mtwara shilingi
milioni 700 na kuwezesha Taasisi ya Ustawi wa Jamii kuboresha utoaji
wa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya soko shilingi milioni 250.
Aidha,
jumla ya shilingi milioni 827.95 zimetengwa kwa ajili ya shughuli za
kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii.
“Ili kutekeleza vipaumbele vilivyoanishwa kwa mwaka 2020/21,
Wizara kupitia Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii imekadiria kutumia kiasi
cha shilingi bilioni 33 kwa ajili ya kutekeleza majukumu
mbalimbali ya Wizara ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa ofisi na miradi ya
maendeleo” alisema
Ummy
amesema Wizara imeendelea kukuza ari ya jamii kushiriki katika kujiletea
maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kutumia nguvu kazi na rasilimali
zinazowazunguka na kusimamia masuala yote ya ushirikishwaji wa jamii kwenye
sekta mbalimbali.
No comments:
Post a Comment