Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaasa wajasiliamali Mkoani
Rukwa kutotaja ugonjwa wa Corona (Covid-19) kama kikwazo cha kushindwa
kununua kitambulisho cha mjasilimali kwa mwaka huu 2020, kwani wananchi
wa Tanzania walihimizwa kuendelea kuchapa kazi na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli hali ambayo ni tofauti na nchi nyingine ambapo wananchi wake
walikuwa wamefungiwa.
Mh.
Wangabo amekataza vitambulisho hivyo kuuzwa rejareja kwani jambo hilo
huzalisha wadaiwa (defaulters) na hivyo kuwataka wahusika kuviuza
vitambulisho hivyo kwa fedha taslimu na kisha fedha hizo ziwasilishwe
kwenye akaunti ya Katibu Tawala wa Mkoa ili zifikishwe Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kwaajili ya kutumika katika maendeleo ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) Akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda vitambulisho vya ujasiliamali vya mwaka 2020. |
“Kwahiyo
fedha zitolewe kabla ya kupewa kitambulisho lakini kusiwe na kisingizio
cha Covid – 19, kwamba mzunguko wa fedha, sijui nini, hiki ni
kitambulisho kinachomtambulisha mjasiliamali ili asipate bugudha yoyote,
vinginevyo ukisema kwamba huwezi, watawabugudhi , kwa namna wanayoona
wao na kwa sheria zao, kwasababu hawakutambui wewe kama mjasiliamali
mdogo, wewe unajitambua lakini hutambuliki, Mheshimiwa Rais amekupa
heshimu ya kukutambua kuwa wewe ni mfanyabiashara mdogo, ukivaa
kitambulisho chako unakwenda nchi nzima,” Alisema.
Aidha,
Mh. Wangabo alitaja changamoto kadhaa zilizokwamisha zoezi la kwanza la
uuzaji wa vitambulisho hivyo ikiwemo usimamizi na ukosefu wa Kanzi data
ya wafanyabiashara wadogo pamoja na ucheleweshaji wa kuweka mapato
kwenye akaunti ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) hali iliyopelekea
kuchelewa kwa taarifa, hivyo kuwaonya wale wote watakaochelewa kuweka
fedha hizo kwenye akaunti ya RAS.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) Akimkabidhi Mkuu wa
Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule vitambulisho vya ujasiliamali
vya mwaka 2020. |
Mh.
Wangabo ametoa kauli hizo wakati akikabidhi vitambulisho 3,000 vya
awamu ya kwanza kwa wakuu wa wilaya tatu za mkoa wa Rukwa ambapo kwa
mwaka 2019, Mkoa wa Rukwa ulipokea vitambulisho 55,000 na kuuza
vitambulisho 32,028 ambavyo ni sawa na asilimia 58.2 na hivyo kukusanya
shilingi 640,560,000/= na mwaka huu mkoa unatarajia kupokea vitambulisho
25,000.
Akitoa
neno la shukrani Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda
alimuhakikishia mkuu wa Mkoa kuwa maelekezo yanayotolewa na serikali
hayahitaji kujadiliwa zaidi ya kuyatekeleza na kuongeza kuwa changamoto
zozote watakazokumbana nazo watakuwa tayari kukabiliana nazo ili
kuhakikisha uchumi wa nchi unaimarishwa na wanachi wenyewe.
“Mimi
nimepokea na nitakwenda kutekeleza kwasababu maelekezo ya serikali sisi
watendaji tulioko huku chini tunayapokea na kuyatekeleza, kwahiyo
changamoto zozote ambazo zitajitokeza, tutakabiliana nazo kwasababu mimi
pia naamini, uchumi wa nchi hii utajengwa na wananchi wenyewe, kwahivyo
hii ni sehemu ya wananchi katika kuokoa na kuimarisha uchumi wa nchi
yao kwa faida yao, kwahiyo ni suala ambalo tunaipongeza serikali na
wajasiliamali wadogo wana nafasi ya kuchangia kwenye uchumi wa nchi
yao,” Alisema.
Kwa
awamu ya Kwanza, Manispaa ya Sumbawanga wamepewa vitambulisho 800,
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wamepewa vitambulisho 800,
Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi wamepewa vitambulisho 800 na Halmashauri
ya Wilaya ya kalambo Wamepewa vitambulisho 600 na hivyo kusubiri awamu
ya pili ya ugawaji huo ambao utahusisha vitambulisho 22,000 kwa
halmashauri zote nne za mkoa huo.
No comments:
Post a Comment