Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, ametoa siku
kumi kwa Mamlaka ya Udhibiti huduma za Nishati na Maji (EWURA) kumpatia majibu
ya uwiano wa viwango vya bei ya mafuta katika maghala ya Kupokea na kuhifadhia
mafuta nchini.
Dkt. Kalemani alisema hayo alipofanya ziara ya
kutembelea ghala la kuhifadhia mafuta la kampuni ya GBP iliyoko mkoani Tanga, Mei
10, 2020, ili kuona kama agizo lake alilolitoa mwezi Machi, 2020, la kuwataka
waagizaji mafuta nchini wanaagiza shehena kubwa kutokana na tishio la kuwepo
kwa virusi vya Corona.
Pia alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya
usambazaji wa umeme vijijini katika wilaya ya Mkinga na Muheza mkoani huo
pamoja na kuwasha umeme.
Baada ya kupata taarifa ya mwenendo wa uingizaji,upokeaji
na uhifadhi wa mafuta nchini katika maghala pamoja na mambo mengine, Dkt.Kalemani
aliiagiza EWURA kufanya tathmini ya bei ya mafuta katika maghala hayo kwa lengo
la kuboresha biashara ya mafuta kwa maslahi ya watumiaji na wafanyabiashara.
Dkt.Kalimani alisema kuwa, serikali imeweka
utaratibu wa kuweka maghala ya kupokea na kuhifadhi mafuta katika kila ukanda
wa nchi kwa lengo la kuwapunguzia gharama za usafiri wafanyabiashara wa mafuta
wanaotembea umbali mrefu kuyafuata mafuta hayo, pia kuwezesha watumiaji kupata
huduma hiyo kwa haraka, karibu na kwa bei nafuu wakati wote.
Sambamba na hilo kulinda ubora wa miundombinu ya
barabara nchini kwa kuwa magari yanayobeba mizigo mizito ikiwemo mafuta
yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa barabara.
“EWURA na PBPA nawapa siku 10,muangalieni uwiano na
uratibu sahihi wa bei ya mafuta katika maghala ili bei hizo zisitofautiane sana
na taratibu za bei zilizowekwa, kwa kuwa mafuta yapo mengi nayakutosha, na
mniletee majibu, Lengo la serikali ni kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa urahisi
na kwa bei nafuu wakati wote kwa kuwanufaisha wafanyabiashara na watumiaji”, alisema
Dkt. Kalemani.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa mafuta kwa kanda ya
kaskazini ikiwemo Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro,Manyara na Tanga kutumia ghala
la kuhifadhi na kupokea mafuta lililopo mkoani Tanga kuliko kuyafuata mkoani
Dar Es Salaam.
“Wafanyabiashara wanaofuata mafuta Dar es salam
watalazimika kuuza kuwauzia watumiaji kwa bei ya juu hivyo kuwakandamiza
watumiaji hii si sahihi na ndiyo maana karibu kila ukanda wa nchi tumeweka
ghala la kuhifadhi na kupokea mafuta,tofauti na ilivyokuwa awali mafuta yote
yalikuwa yakipatikana mkoani Dar Es Salaam pekee”,alisisitiza Dkt. Kalemani
Alitoa wito kwa makampuni yote ya uwagizaji wa
mafuta nchini kwa kushirikiana na EWURA na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa
pamoja (PBPA)kushirikiana kwa pamoja kuendelea kuleta mafuta mara dufu ili
kujihakikishia uwepo wa mafuta nchini hata kama ugonjwa wa corona utaendelea
kuwepo.
Dkt. Kalemani alifafanua kuwa mafuta yaliyopo nchini
kwa sasa yanauwezo wa kutumika zaidi ya miezi miwili hadi mitatu mbele na bado
kila siku wanapokea mafuta, ambapo kwa sasa nchi inapokea inapokea mafuta lita
milioni 428.7 tofauti na awali kabla ya agizo kutoka ilikuwa ikipokea mafuta
lita milioni 185.
Aidha aliwataka wafanyabiashara ya mafuta kujenga
vituo vya mafuta katika maeneo yaliyo vijijini ili kulinda ubora wa mafuta na
kusogeza huduma karibu na watumiaji hasa wadogo akitolea mfano waendesha
pikipiki ambao ndiyo wanaotegemeo kubwa la usafiri katika maeneo ya vijijini.
Alisema kuwa watumiaji wadogo wa vyombo vya moto,
wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma ya mafuta, na wengine wamekuwa
wakihifadhi mafuta katika nyumba zao jambo ambalo linahatarisha usalama wao.
Aidha alisema kuwa pia kumekuwa na tabia ya kuuza
kiholela mafuta na uhifadhi mbovu wa mafuta hayo na hivyo kupunuza ubora
waviwango vya mafuata kwa watumiaji na hivyo hata kulazimu mafuta hayo kuchanganywa
na hivyo kuchangi uharibifu wa yyombo vinavyotumia mafuta hayo.
“Wafanyabiashara nendeni mkajenge vituo vidogo vya
mafuta vijijini, mrahisishe huduma ya upatikanaji wa mafuta na bei nafuu kwa watumiaji
wadogo ambao wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo,tuungane
kutekeleza lengo la serikali la kuhakikisha kila mtumiaji wa mafuta anapata
bishaa hiyo kwa wakati na kwa bei nafuu”, alisisitiza Dkt. Kalemani.
Pamoja na mambo mengine alitembelea eneo inapojengwa
kifaa kitakachotumika kupima mafuta (Flow Meter), yanayoingia nchini kutoka
katika Meli kwenda katika maghala ya kuhifadhi na kupokea mafuta katika Bandari ya Tanga.
Aliiagiza mamlaka ya bandari nchini kukamilisha
ujenzi wa mtambo huo haraka ili serikali ipate kiwango sahihi cha mafuta
yanayoingia nchini kupitia Bandari ya Tanga ili kupata kodi na tozo stahiki.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uagizaji
mafuta ya GBP, Badar Seif Sood alimueleza Waziri wa Nishati kuwa wamefanya
upanuzi wa bandari hiyo, hivyo kwa sasa inauwezo wa kuhifadhi na kupokea mafuta
lita milioni 182, tofauti na walivyokuwa wananza mwaka 2017 walipokuwa
wakihifadhi na kupokea mafuta lita milioni 182, na upanuzi utaendelea kulingana
na mahitaji.
Aliishukuru serikali kupitia wizara ya nishati,
kuendelea kuwalinda wafanyabiashata wa mafuta wakiwamo wamiliki wa maghala ya
kuhifadhi na kupokea mafuta pamoja na waagizaji wakubwa wa mafuta kwa kuhakikisha
wanafanya biashara zao katika mazingira rafiki: Huku akiahidi kuendelea kutoa
huduma bora kwa watumiaji wa mafuta hayo nchini.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kalemani, pia alikagua
maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini katika Wilaya ya Mkinga na kuwasha
umeme katika kijiji cha Mbuyuni kata ya Mapatano na kutembelea kisima cha maji katika
kijiji cha Jihirini na kuliagiza Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kupeleka na
kuwasha umeme katika kisima hicho mwishoni mwa mwezi huu.
Vilevile alitembelea Wilaya ya Muheza na kukagua
kazi ya usambazaji wa umeme katika kijiji cha Kwakokwe na kuwataka wananchi
kuendelea kulipia gharama za kuunganishiwa umeme kwa kuwa vijijini vyote nchini
vitapata umeme na kwamba wasikubali kuuziwa miundombinu ya umeme na pia watumie
wakadarasi wanaotambulika na TANESCO katika kutandaza nyaya katika nyumba zao.
No comments:
Post a Comment