Matokeo chanyA+ online




Thursday, May 7, 2020

MAKONTENA YAENDELEA KUMIMINIKA KATIKA BANDARI KAVU YA KWALA

 Moja ya kontena likiwekwa vizuri baada ya kushushwa kwenye treni ya pili iliyokuwa na behewa 20 kuwasili kwenye Bandari Kavu Kwala.
 
 Treni  ya pili ya mizigo yenye jumla ya makontena 20 imewasili katika Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Kibaha mkoani Pwani kutoka Bandari ya Dar es Salaam na kufanya jumla ya makontena yaliyofikishwa katika bandari hiyo kufikia  49.

Kuanza kwa zoezi la kupokea makontena hayo kumekuja baada ya kukamilika kwa sehemu ya mradi huo ambapo jumla ya hekta 5.5 zimewekwa zege na reli kwa ajili ya kupokea kontena na kwamba eneo ni sehemu ya hekta 60 zitakazojengwa na litakuwa na uwezo wa  kuhifadhi kontena 500 kwa wakati mmoja.

Akizungumza wakati wa hafla ya upokeaji wa treni hiyo iliyofanyika bandarini hapo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, amesema kuanza kwa bandari kavu ya Kwala ni hatua muhimu ya kumaliza changamoto ya msongamano inayoikabili Bandari ya Dar es Salaam.

Amefafanua msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam umekuwa ukisababisha malalamiko kutoka kwa wateja na kuishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kusimamia mradi huo hadi kufikia kuweza kupokea treni ya behewa.
 Treni iliyobeba Kontena ikiwa katika bandari kavu ya Kwala iloyopo  Kibaha mkoani Pwani
 
Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV

Ameongeza kuwa bandari hiyi inafungua ukurasa mpya na mwanzo wa operesheni za kuondoa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam zoezi ambalo pia litapunguza kuingia kwa malori ya mizigo katikati ya jiji hivyo kupunguza foleni za magari na kulinda miundombinu ya Barabara zetu," alisema Nditiye.

Amesema amefarijika kuona kazi kubwa iliyofanyika ikiwemo ujenzi wa sakafu ngumu katika eneo kwa ajili ya kuhudumia makasha, ujenzi wa mitaro ya kuzuia mafutiko, miundombinu ya awali ya umeme, maji, TEHAMA, ulinzi, zimamoto, nyumba za watumishi na ofisi.

Kea upande wake  Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) Profesa Ignas Rubaratuka amesema mradi huo ni matokeo ya dhamira ya dhati ya Serikali ya awamu ya tano kupunguza msongamano ndani na nje ya bandari ya Dar es Salaam.

"Mradi huo ni utekelezaji wa dhana ya hapa kazi tu ulioanza kufuatia maelekezo ya Serikali baada ya kuona eneo hilo linafaa zaidi kuliko lile la Kisarawe, " amesema Profesa Rubataruka huku akitoa mwito kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya Tanzania kutumia bandari zilizopo kwani utendaji na usalama umeimarika zaidi.

"Tumeweza kurudisha heshima ya bandari kwa kuongeza ufanisi na kuimarisha usalama na bado tunaendelea na kuboresha bandari za Tanga, Dar es Salaam na Mtwara ili kuweza kuongeza ufanisi zaidi na kuvutia wateja wapya na kurudisha wale wa zamani ambao walituhama," amesisitiza.


Akielezea utekelezaji wa mradi wa Bandari Kavu ya Kwala, Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Deusidedit Kakoko amesema unatekelezwa kwa awamu katika eneo la hekta 60 ambazo ni sehemu ya hekta 500 za eneo lililotwaliwa na Mamlaka hiyo katika Kata ya Kwala.

Amesema mradi huo ulioanza Februari 2017 unatekelezwa na Mkandarasi Suma JKT kwa gharama ya jumla ya Sh. bilioni 47 na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.

Mhandisi Kakoko amefafanua kwamba katika awamu ya kwanza ya mradi huo ilihusisha ufyekaji wa eneo la hekta 120, kulisawazisha, kujaza kifusi, kujaza matabaka ya changarawe na ujenzi wa reli kilomita 1.3 kutoka kituo cha Kwala hadi bandarini hapo.

Awamu ya pili ilihususha kunyanyua tuta kumwaga zege na kuweka reli tano zenye urefu wa mita 500 kila na kuzungusha ukuta wenge urefu wa Kilomita 3.2.

Mhandisi Kakoko amesema awamu hiyo pia inahusisha uwekaji wa miundombinu ya huduma za umeme, maji, mawasiliano na vizima moto pamoja na ujenzi wa nyumba za muda za watumishi na ofisi.

Amesema hadi sasa mkandarasi ameshalipwa Sh bilioni 20.5 sawa na asililimia 45 huku mradi ukiwa asilimia 70 ukitarajiwa kukamilika Julai.

Pia awamu ya tatu itafuata ambayo ni ujenzi wa barabara ya kilomita 15.5 kwa kiwango cha changarawe ikiwa ni hatua za awali za kuijenga kwa kiwango cha zege. Barabara hii inaunganisha bandari kavu ya Kwala na barabara ya Morogoro eneo la Vigwaza.

Mhandisi Kakoko amesema pia bandari hiyo itaunganishwa na reli ya kisasa ya SGR ambayo itatumika kupeleka kontena mikoani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment