Matokeo chanyA+ online




Thursday, June 4, 2020

DKT. ZAINAB CHAULA AZIKUMBUSHA TAASISI ZA SERIKALI KUTUMIA HUDUMA ZA POSTA KUSAFIRISHA BIDHAA NA VIFURUSHI KWA USALAMA ZAIDI


Na Prisca Ulomi - WUUM,  Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula amezikumbusha taasisi za Serikali kutumia huduma za Shirika la Posta Tanzania (TPC) kusafirisha bidhaa, vifurushi na vipeto kwa usalama zaidi

Dkt. Chaula ameyasema hayo wakati wa kikao cha Menejimenti ya Wizara yake na viongozi wa TPC wakiongozwa na Posta Masta Mkuu wa TPC, Hassan Mwang’ombe kilichofanyika jana kwenye ukumbi wa Wizara hiyo uliopo Mtumba, Mji wa Serikali, Dodoma ambapo Shirika hilo lilifika ofisini hapo kwa lengo la kujitambulisha na kuwasilisha taarifa ya Shirika hilo kwa Dkt. Zainab Chaula, Katibu Mkuu mpya wa Wizara hiyo


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula

Dkt. Chaula alisema kuwa TPC imepewa dhamana kisheria kuwa msafirishaji mkuu wa barua, vifurushi, vipeto na bidhaa mbali mbali kwa mujibu wa sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Na. 19 ya mwaka 1993 iliyoanzisha Shirika hilo nan i Shirika la umma ambapo Serikali imewekeza

Ameongeza kuwa TPC imefanya kazi kubwa ya kusafirisha sampuli kutoka hospitali mbali mbali nchini kwenda Maabara Kuu ya Serikali wakati wa kipindi cha janga la virusi vya Corona pamoja na kusafirisha nyaraka za mahakama zote nchi nzima, benki, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Mifuko ya Hifadhi za Jamii, hisa za kampuni mbali mbali na kutumia usafiri wa ndege kwenda ndani na nje ya Tanzania

Ameitaka TPC kuunganisha huduma za posta na anwani za makazi na postikodi na simu za mkononi ili kuhudumia wananchi katika kufanikisha azma ya Serikali ya kurahisisha na kufanikisha usambazaji na usafirishaji wa barua, vifurushi, vipeto na bidhaa kwa wananchi

“Tunataka mwananchi afikishiwe nyanya nyumbani kwake na sio atumie piki piki kuzunguka kwa muda mrefu na kupiga simu bila kufika kwa mteja kwa wakati,” amesisitiza Dkt. Chaula

Naye Posta Masta Mkuu wa TPC, Hassan Mwang’ombe ameziomba taasisi za Serikali kutumia Shirika hilo kusafirisha barua, vifurushi na vipeto kwa kuwa bidhaa zao zitafika kwa usalama na uhakika kwa kuwa Shirika hilo linatumia huduma ya mtandao wa TEHAMA kutoa huduma zake kwa wateja kwa kuunganisha ofisi zake 202 zilizopo maeneo mbali mbali nchi nzima; wana wataalamu wa lojistiksi; na wanatumia anwani za makazi na postikodi kuhudumia wateja.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amelishauri Shirika hilo kuwa pamoja na kuboresha huduma zake ndani ya nchi pia amelitaka kufungua milango yake na kufanya biashara na nchi nane za jirani zinazopakana na Tanzania  kwa kuongeza huduma za lojistiksi kwenda nchi za jirani za usafirishaji wa bidhaa, biashara mtandao, uwakala na maduka ya kubadilisha fedha ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti mara kwa mara ili kuendeleza biashara za Shirika hilo

Naye Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara wa Shirika hilo, Mwanaisha Ally Said, ameiomba Wizara kuhakikisha kuwa watoa huduma za usafirishaji wa nyaraka, vifurushi na vipeto wasio na leseni ya kuendesha biashara hiyo inayotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ili kuhakiisha kuwa wananchi wanapata huduma za sekta ndogo ya posta na Serikali inapata mapato yake

No comments:

Post a Comment