HOTUBA YA
MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA KUMI NA TISA WA BUNGE
1.
Mheshimiwa
Spika,
naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia
afya njema na kutuwezesha kufika siku hii ya leo ambayo naiita kuwa ni siku ya
kihistoria kwetu.
2.
Nasema kuwa ni ya kihistoria kwa sababu Bunge
lako Tukufu linahitimisha shughuli za Bunge la Kumi na Moja (11) la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania pia tunahitimisha Mkutano wa Kumi na Tisa (19) wa Bunge
ulioanza mwezi wa Aprili mwaka huu wa 2020.
3.
Mheshimiwa
Spika,
katika Mkutano huu wa Bunge, licha ya uwepo wa ugonjwa wa homa ya mapafu
inayosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19), tumeweza kukaa hapa Dodoma kwa
kipindi kisichopungua miezi miwili na nusu. Aidha, katika kipindi hicho
tumeweza kutekeleza majukumu yetu yote kama ilivyokuwa imepangwa.
4.
Ama kwa hakika hatuna budi kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwani tunakamilisha maisha yetu ya Kibunge kwa kipindi cha miaka mitano
toka Novemba 2015. Tumeshirikiana katika maeneo mengi nje na ndani ya Bunge kwa
kila mmoja kutekeleza majukumu yake.
5.
Mheshimiwa
Spika,
siwezi kuanza kueleza yaliyojiri kwenye majukumu yetu bila kumshukuru Mwenyezi
Mungu aliyeniwezesha kuwa na afya njema na kunisimamia katika kila jambo na
hasa nilipokuwa natekeleza majukumu yangu binafsi na ya umma kwa kipindi chote
hadi sasa. InshaAllah, yeye ndiye msimamizi wa yote.
6.
Mheshimiwa
Spika,
kwa moyo mkunjufu kabisa naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
kitendo chake cha kuniamini na kuniteua kushika wadhifa wenye dhamana kubwa ya
kumsaidia kazi ya utendaji ndani ya Serikali kwa kipindi chote cha miaka mitano.
7.
Kwa niaba ya Familia yangu na Wana-Ruangwa
wote, namshukuru sana kwa ukarimu, imani na upendo aliouonesha kwetu, Mwenyezi
Mungu aendelee kumpa nguvu, ulinzi, kheri na kila lililo jema na aendelee
kuliongoza Taifa hili vyema na kwa mafanikio makubwa kama ambavyo Watanzania
tumeendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika kipindi hiki cha Uongozi wake wa
Awamu ya Tano.
8.
Mheshimiwa
Spika,
Rais wetu ametenda mema kwa Watanzania na watamlipa mema. Ninamwombea kheri pia
kwa Uchaguzi Mkuu ujao ashinde kwa ushindi wa kishindo. Amina.
9.
Mheshimiwa
Spika,
ninamshukuru sana pia Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano wake mkubwa wakati wote
nikitekeleza majukumu ya Waziri Mkuu. Vilevile, ninashukuru sana kwa
ushirikiano mkubwa nilioupata kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mheshimiwa Balozi Seif
Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na viongozi, watendaji na
wananchi wote wa Zanzibar.
10.
Mheshimiwa
Spika,
nitumie nafasi hii pia kukushukuru sana wewe binafsi kwa upendo uliouonesha
kwangu kipindi chote cha uhai wa Bunge la Kumi na Moja (11). Kwa uzoefu ulionao
katika kuendesha Bunge, umekuwa msaada sana kwangu kwa kunipa ushauri na
ushirikiano wa dhati ulionifanya nijenge imani kubwa kwenye majukumu yangu
ndani ya Bunge.
11.
Mheshimiwa
Spika,
nami niungane na wenzangu kukutakia kheri nyingi kwenye Uchaguzi ujao, naamini
Wana-Kongwa watasikiliza na kutekeleza dua zetu za kuwa upite bila kupingwa, na
ukirudi hapa chukua fomu ya Uspika ili upate kura zote za ndiyo uendelee kuwa
Spika wa Bunge la Kumi na Mbili (12).
12.
Mheshimiwa
Spika,
sitasahau tukio la tarehe 19 Novemba, 2015 siku ambayo Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipowasilisha jina
langu katika Bunge lako Tukufu na kupendekeza niwe Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
13.
Mheshimiwa
Spika,
nakushukuru tena wewe na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa imani mlioionesha kwa
kuridhia mapendekezo ya Mheshimiwa Rais na kunipigia kura nyingi za ndiyo na
mkaridhia tufanye kazi kwa pamoja katika kuwatumikia Watanzania.
14.
Waheshimiwa
Wabunge wenzangu, natambua, naheshimu na nathamini ushirikiano
wa dhati mlionipa katika kipindi chote cha Bunge. Nami nawaombea na nawatakia
ushindi wa kishindo kwenye Majimbo yenu ili mrudi tena hapa mwezi Novemba,
2020.
15.
Mheshimiwa
Spika,
pia, nawashukuru sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Akson, Naibu Spika, Wenyeviti wa
Bunge Mheshimiwa Mtemi Andrew Chenge, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga na
Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan ambaye mwishoni alipata uteuzi wa Mheshimiwa Rais
kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kwa kuliongoza Bunge hili
kwa busara na umahiri mkubwa.
16.
Mheshimiwa
Spika,
vilevile, namshukuru Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa
Magharibi na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti pamoja na
Wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha Bajeti ya
Serikali. Pia, nawashukuru Katibu wa Bunge Ndugu Stephen Kagaigai na Watumishi
wote wa Bunge kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia katika Mkutano huu na Mikutano
iliyoendeshwa kipindi chote cha miaka mitano.
17.
Mheshimiwa
Spika,
katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu hapa Bungeni, napenda kutambua
mchango wa Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayesimamia Sera, Uratibu, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu
wenye ulemavu. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mhagama kwa kunisaidia
ipasavyo katika kutekeleza majukumu yangu sambamba na majukumu yake ya unadhimu
na uratibu wa shughuli za Serikali Bungeni. Nakuombea sana kwa wananchi wa
Peramiho, Maposeni, Mgazini, Mdunduwalo, wakupitishe upite bila kupingwa.
18.
Mheshimiwa
Spika, vilevile, namshukuru Mheshimiwa Angela Kairuki
(Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji kwa
kufuatilia na kusimamia hatua mbalimbali za kuimarisha na kuboresha mazingira
ya uwekezaji nchini. Mheshimiwa Waziri Kairuki amekuwa akitembelea maeneo
mbalimbali na kukutana na Wawekezaji wadau wa sekta binafsi ili kusikiliza
changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi. Juhudi zake hizo, zimekuwa na mchango
mkubwa katika kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha mahusiano ya sekta
binafsi na Serikali nchini. Nawe nakutakia kila la kheri huko uendako ili upate
kura za kutosha.
19.
Mheshimiwa
Spika, kwa
upande wa masuala ya maendeleo na uwezeshaji wa vijana napenda kumshukuru
Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini, Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu kwa msaada mkubwa katika kusimamia vizuri masuala ya
vijana na ajira. Kadhalika, namshukuru Dada yangu Mheshimiwa Stella Ikupa Alex
(Mb), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kusimamia vema masuala na maslahi
ya Watu Wenye Ulemavu.
20.
Nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri wenzangu
na Naibu Mawaziri; Professor Adelardus Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Balozi
Mhandisi John William Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi; Makatibu Wakuu na Naibu
Makatibu Wakuu wakiongozwa na Bw. Tixon Tuyangine Nzunda, Andrew Wilson Massawe,
na Bibi Dorothy Aidan Mwaluko kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru kwa
ushirikiano wa dhati mlionipa katika kuratibu na kusimamia shughuli za Ofisi ya
Waziri Mkuu. Bila kuwasahau Watendaji wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
21.
Mheshimiwa
Spika,
nitumie fursa hii pia kuwashukuru Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama akiwemo
Jenerali Venance Mabeyo - Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama; Inspekta
Jenerali wa Polisi - Simon Nyakoro Sirro; Brigedia Jenerali Suleiman Mzee
-Kamishna Jenerali wa Magereza; Dkt. Anna Makakala - Kamishna Jenerali wa
Uhamiaji; John William Hasunga - Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji; Kamishna
Diwani Athumani - Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa; Brigedia Jenerali John
Mbung’o - Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa; James Kaji - Kamishna
Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya.
Wakuu hao wa Vyombo vya Ulinzi na
Usalama wameonesha nidhamu na uzalendo mkubwa katika kuhakikisha Nchi yetu,
raia wake na mali zao wanakuwa salama.
22.
Mheshimiwa
Spika,
nawashukuru pia Wakuu wa Taasisi, Wakurugenzi na Watendaji wote Serikalini kwa
ushirikiano mzuri walioutoa na utendaji wa pamoja wenye mafanikio makubwa.
Aidha, tuendelee kutakiana mema na tuchape kazi hadi hapo utumishi wetu
utakapokoma.
23.
Mheshimiwa
Spika,
nimalizie salamu zangu za shukrani kwa Familia yangu ambayo inaniunga mkono,
kunivumilia pale ambapo nawatumikia Watanzania na kunitia moyo siku hadi siku
kwenye majukumu yangu. Bila kuwasahau Wana-Ruangwa ambao walinipigia kura bila
kujali Vyama vyao na kuniwezesha kuingia Bungeni na hatimaye nikapata uteuzi wa
Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya kuwatumikia
Watanzania. Nataka niwahakikishie Wana-Ruangwa kuwa bado tuko pamoja katika
harakati za kuleta maendeleo. Nawashukuru sana.
24.
Mheshimiwa
Spika,
nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru wananchi na Watanzania wote kwa
kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano na ushirikiano walioutoa kwa Serikali
wakati wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya Taifa kwa ujumla
bila kujali tofauti zao za kiitikadi au dini. Sambamba na kuonesha uzalendo,
mshikamano na kudumisha amani na utulivu uliowezesha Serikali kutekeleza
majukumu yake kwa ufanisi na weledi, kwa mujibu wa taarifa zinazotolewa na
taasisi ya GLOBAL PEACE INDEX 2020 inayofuatilia masuala ya amani duniani.
Tanzania ni nchi ya saba kwa amani na utulivu Afrika na ni nchi ya kwanza kwa amani Afrika Mashariki.
Naamini wananchi wataendelea kuiunga mkono Serikali yetu ili ifanye mambo
makubwa zaidi katika kipindi cha pili cha Awamu ya Tano kwa amani na maendeleo
yake.
25.
Mheshimiwa
Spika,
baada ya salamu za shukurani nami naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu
walionitangulia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Mbunge wa
Iramba Magharibi kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mheshimiwa
Dkt. Godwin Aloyce Mollel, Mbunge wa Siha kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Aidha, mkiwa viongozi
mlioteuliwa, tambueni kuwa mnalo jukumu kubwa la kuwahudumia Watanzania,
hususan katika kipindi hiki ambacho Nchi yetu imekumbwa na changamoto
mbalimbali likiwemo janga la Corona.
SALAMU ZA POLE
26.
Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na Mkutano huu wa 19, Bunge lako Tukufu lilipata pigo
kwa kuondokewa na Wabunge wenzetu akiwemo Mheshimiwa Mchungaji Dkt. Getrude
Pangalile Rwakatare, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum; Mheshimiwa Richard Mganga
Ndassa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumve na Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine
Philip Mahiga, aliyekuwa Mbunge na Waziri wa Katiba na Sheria.
27.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho pia, tuliondokewa na aliyekuwa Jaji Mkuu Mstaafu,
Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhan. Aidha, niungane na Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Magufuli kuwapa pole majirani zetu, wananchi wa Burundi kwa kifo cha
aliyekuwa Rais wa Nchi hiyo, Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza. Tuendelee kumuomba
Mwenyezi Mungu azipumzishe Roho za wapendwa wetu wote mahali pema. Amina.
28.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Taifa letu lilikumbwa na majanga mbalimbali ikiwa ni pamoja na
mafuriko, COVID-19 na ajali za barabarani ambazo zilisababisha vifo, majeruhi
na uharibifu wa mali. Napenda kutoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki
waliopoteza wapendwa wao na wengine kupata majeraha kutokana na matukio hayo. Tumuombe
Mwenyezi Mungu aziweke Roho za marehemu mahali pema na waliopata majeraha
awajalie nafuu na kupona mapema. Amina.
MAFANIKIO
YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO
29.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa nitumie
fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kutokana na fikra na uongozi makini katika ujenzi wa
Taifa letu. Ni dhahiri kuwa maono yake katika kuongoza na kusimamia utekelezaji
wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 na mipango ya Serikali, zimeleta mafanikio
makubwa ambayo hivi sasa wote tunayaona.
30.
Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Rais na Makamu wake Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan, wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawafikia
Watanzania, wanawasikiliza na kutatua kero zao. Lengo la ziara hizo, pamoja na
mambo mengine lilikuwa ni kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Chama
cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 ikiwemo kukagua miradi ya maendeleo;
kuzungumza na watumishi na kuwafahamisha kuhusu falsafa ya Serikali ya awamu ya
tano ya Hapa Kazi Tu.
31.
Mheshimiwa Spika, ziara hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utendaji wa watumishi
wa umma. Hivi sasa, wananchi wanapokwenda katika ofisi za umma wanapokewa,
wanasikilizwa na kuhudumiwa vizuri. Aidha, usimamizi wa miradi ya maendeleo umeimarika
sambamba na kuakisi thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Hapa Bungeni ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa maoni, ushauri na
ushirikiano ambao mmekuwa mkiutoa wakati wa ufuatiliaji wa shughuli za
maendeleo sambamba na kuisimamia Serikali yetu.
Mambo mengi ya kujivunia yamefanywa na tumekuwa tukiyaeleza katika maeneo
mengi kupitia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari, nyaraka mbalimbali, uwepo
wa miradi mingi ya kimkakati hadi kwa wananchi wa kawaida.
32.
Nitaeleza majukumu
na miradi michache tena kwa kifupi ili kuwakumbusha nini Serikali imefanya
katika kipindi hiki cha miaka mitano.
·
Marekebisho ya
nidhamu kwa utumishi wa umma na uwajibikaji Serikalini ili kuwezesha Watumishi
kutambua majukumu yao na kuwatumikia Watanzania.
·
Mapambano dhidi ya rushwa
ndani ya Serikali na nje ya Serikali ili kulinda mali na fedha za umma. Hatua
hii ni endelevu, lengo ni kung’oa mizizi ya rushwa nchini.
·
Kuimarisha vyombo
vya ulinzi na usalama, mhimili wa Bunge na Mahakama. Matakwa yetu ni kuhakikisha
kuwa nchi inabaki salama na mihimili ifanye kazi yake.
·
Mapambano dhidi ya
matumizi ya dawa za kulevya ili kujihakikishia kuwa tunakuwa na Taifa lenye
nguvukazi inayofanya kazi. Mapambano bado yanaendelea. Tutapambana na
wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya.
·
Utambuzi wa
watumishi hewa waliokuwa wanalipwa fedha wakiwa hawapo. Katika zoezi hili tumepata mafanikio makubwa na
kuokoa shilingi Bilioni 19.83 kwa kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo
watumishi hewa 19,708 na wenye vyeti vya kugushi 15,411.
·
Ukusanyaji wa mapato
ili kuwezesha Serikali kujenga miradi na kutoa huduma muhimu. Ukusanyaji
wa mapato umeongezeka kutoka wastani wa shilingi Bilioni 800 kwa mwezi mwaka
2015 hadi wastani wa shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi katika kipindi
cha Julai 2019 hadi Aprili 2020.
·
Kuimarisha uwekezaji
kwa kujenga viwanda. Hadi Aprili 2020 jumla ya viwanda vipya 8,477
vikiwemo vidogo, vya kati na vikubwa vimeanzishwa katika maeneo mbalimbali
nchini na hivyo kuwezesha ongezeko la ajira viwandani za viwandani zipatazo
482,601.
·
Kuimarisha kilimo na
masoko. Tumeimarisha kilimo cha mazao makuu, kama vile, Korosho, Pamba, Chai, Tumbaku,
Kahawa, Michikichi na Mkonge pamoja na mazao ya chakula ili kuwa na uhakika wa
usalama wa chakula.
·
Kuimarisha ushirika wa
kilimo na upatikanaji wa pembejeo pamoja na huduma za ugani ili kuwafanya
wakulima kuzalisha kwa tija.
·
Marekebisho ya Sheria ya madini yamefanyika
sambamba na kuanzisha masoko ya madini 28 na vituo 12 vya ununuzi wa madini
katika maeneo ya uchimbaji na hivyo kuongeza makusanyo ya Serikali, kupungua
biashara haramu na utoroshaji madini kwenda nje. Mwezi Machi hadi Septemba,
2019 jumla ya kilo za dhahabu 4,680.28 zenye thamani ya shilingi bilioni 432.49
zimezalishwa na Serikali kukusanya shilingi bilioni 30.27.
·
Kuhamishia Makao
Makuu Dodoma ambapo tayari Watumishi wapatao 15,361 wamehamia Dodoma na
sasa fursa za uwekezaji zimeongezeka katika Jiji la Dodoma.
·
Kuboresha miundombinu
na taaluma Sekta ya Elimu kwa ngazi zote kuanzia awali hadi Elimu ya Juu
ikiwemo ujenzi na ukarabati wa madarasa, maktaba, maabara, nyumba za walimu,
mabweni na ukarabati wa shule kongwe ili kuziongezea uwezo wa kupokea wanafunzi
wengi zaidi.
·
Sera ya Elimu bila Ada
ambayo inatumia zaidi ya Shilingi Bilioni 20.8 kila mwezi kwa ajili ya fidia ya
ada, posho ya madaraka kwa walimu wakuu, wakuu wa shule na waratibu kata kila
mwezi toka 2016 na tutaendelea. Hii imesaidia kuongeza uandikishaji na
mahudhurio shuleni.
· Kuimarisha huduma za afya kwa kujenga Zahanati, Vituo vya Afya, kujenga
Hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na za Kitaifa, huduma za Madawa na Vifaa Tiba.
Tumejenga Zahanati 1,198 Vituo vya Afya 487, Hospitali za Wilaya 71,
Hospitali za Rufaa za Mikoa 10, na Hospitali za Kanda 03 za
Kusini – Mtwara, Magharibi – Tabora na Kanda ya Ziwa - Burigi.
· Ujenzi wa miradi ya maji Vijijini na Mijini tumefikia asilimia 84
Mijini na asilimia 70.1 Vijijini.
· Ufufuaji wa Shirika la Ndege kwa kununua ndege kumi na moja (11) ambazo
zinatoa huduma mikoa yote yenye Viwanja vya Ndege na nje ya nchi.
· Ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya Ndege kwenye mikoa isiyo na Viwanja
vya Ndege unaendelea.
· Ununuzi wa Rada nne mpya za kuongoza Ndege za kiraia zilizo Mwanza,
Mbeya, Dar-es-Salaam na Kilimanjaro.
· Ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme (Mwalimu Nyerere Dam) utakaozalisha
Mg 2115 kwa sasa umefikia asilimia 40. Ujenzi una gharama ya Shilingi Trilioni
6.5
· Usambazaji wa umeme Vijijini kupitia Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) tumefikia Vijiji kwa asilimia
80% ambapo hadi Aprili 2020 shilingi trilioni 2.27 zimetumika na kufanikisha
jumla ya vijiji 9,112 kati ya 12,268 vya Tanzania Bara kuunganishwa na umeme
kutoka vijiji 2,118 mwaka 2015.
· Ujenzi wa Mradi
wa Reli ya Kimataifa (SGR) wa Kilomita 300
Dar-es-Salaam–Morogoro. Mradi umefikia asilimia 78. Kipande cha Morogoro hadi
Makutupora Kilomita 422 mradi umefikia asilimia 30 ya kazi. Lengo ni
kukamilisha mradi huu ifikapo Juni 2021 kwa gharama ya Shilingi Trilioni 7.5.
·
Ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na za
wilaya zenye thamani ya
zaidi ya Shilingi Trilioni 7.6. Pia serikali inaendelea kujenga barabara ya
njia nne kutoka kutoka Kimara hadi Kibaha (km 19.2)
· Ujenzi wa madaraja: ujenzi wa
daraja la juu la Mfugale (Dar-es- Salaam), daraja la Furahisha (Mwanza) na
daraja la Magufuli (mto Kilombero) umekamilika; ujenzi wa barabara ya pete (Ubungo
interchange) umefikia asilimia 77 kwa shilingi bilioni 247; Aidha, ujenzi unaendelea kwa daraja la New Selander
(Dar- es-Salaam) kwa shilingi Bilioni 270. Daraja la Kigongo- Busisi shilingi
Bilioni 699.2
· Ujenzi wa
Bandari, uboreshaji na upanuzi wa Bandari za Tanga,
Dar-es-Salaam na Mtwara kwa Shilingi zaidi ya Trilioni 1.2. Pia, ujenzi wa
Bandari ya Kigoma na Kalema umeshatengewa fedha.
· Ujenzi wa Meli mpya yenye uwezo
wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria na ujenzi wa
chelezo; ukarabati wa meli ya MV Victoria na MV Butiama ambapo katika kipindi
cha mwaka 2015/16 hadi Aprili, 2020 jumla ya shilingi bilioni 111.7 zimetumika.
Vile vile, Serikali
imekamilisha ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani
200 za mizigo katika Ziwa Nyasa; na ukarabati wa meli ya mafuta ya MT Sangara
katika Ziwa Tanganyika.
· Ujenzi wa
Vivuko vya MV Kigamboni, MV Pangani, Kigongo -Busisi, MV Sengerema na
Nyamisati.
· Urejeshaji na usimamizi wa mali za Ushirika zilizokuwa zimechukuliwa
kinyume na utaratibu, kama vile, NYANZA, SHIRECU, KNCU, Mamlaka ya Mkonge
Tanzania, n.k.
· Kusimamia maboresho kwenye Sekta ya Uvuvi na Mifugo kwa kuvua na kufuga kisasa,
kujenga viwanda na masoko yake.
33.
Mheshimiwa
Spika, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupitia Bunge lako
Tukufu katika kipindi cha miaka minne imeidhinisha jumla ya shilingi
trilioni 33.1 kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi ya maendeleo kote nchini ikiwemo miradi ya kimkakati niliyoitaja hivi
punde
MVUA KUBWA
ZILIZONYESHA NCHINI
34.
Mheshimiwa
Spika,
baadhi ya maeneo ya Nchi yetu yalikumbwa na mafuriko kufuatia mvua nyingi
zilizonyesha nchini. Mafuriko hayo yalisababisha madhara mbalimbali ikiwemo
uharibifu wa miundombinu, mali na vifo. Serikali imeendelea kuchukua hatua za
kurejesha hali ya miundombinu iliyoharibika na zoezi hilo ni endelevu.
35.
Mheshimiwa
Spika,
mvua nyingi tulizopata msimu huu zimeleta neema ya mavuno lakini pia katika
baadhi ya maeneo mazao yameharibika. Hivyo, niendelee kusisitiza kauli ya
Waziri wa Kilimo wakati akiwasilisha Hoja ya Wizara yake kuwa hali ya chakula
nchini imeendelea kuimarika. Kwa msingi huo, hatutarajii kuwa na upungufu
wowote wa chakula kwa msimu ujao. Muhimu kwetu ni kuongeza umakini wa matumizi
kwa kuweka akiba ya chakula ili kitosheleze mahitaji ya familia hadi msimu
ujao.
MAPAMBANO DHIDI YA
HOMA KALI YA MAPAFU COVID 19
36.
Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2020, baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO)
kutangaza kuwa COVID 19 ni janga la dunia, ambako nchi nyingi duniani zilipata
maambukizi makubwa, Tanzania tulitangaza kisa cha kwanza tarehe 15 Machi, 2020.
37.
Nchi nyingi duniani zikiwemo nchi za Bara la
Afrika ugonjwa huu ulianza kuingia. Kila nchi ilichukua hatua kadhaa za
kudhibiti maambukizi zikiwemo watu kutotoka ndani ya nyumba zao “Lockdown”, kuzuia mikusanyiko kwa
kufunga mashule, vyuo, michezo, aina zote za usafiri wa ndani na nje, maeneo ya
Ibada na shughuli za uzalishaji maeneo ya kazi, viwanda, n.k. vilifungwa.
38.
Tanzania nasi tulianza kuchukua hatua kadhaa
ili kukabiliana na maambukizi kwa kuunda Kamati 3 za ngazi ya Mawaziri,
Watendaji na Wataalam wa Afya kwa lengo la kufanya tathmini ya hatua za
kuchukua ili kupunguza maambukizi na kulinda anguko la kiuchumi.
39.
Hatua zilizochukuliwa ni kupunguza misongamano
kwa kufunga shule, vyuo, mikutano, kunawa maji, matumizi ya vitakasa mikono na
kuvaa barakoa.
40.
Mheshimiwa
Spika,
siku ya tarehe 22 Machi, 2020 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Jijini Dodoma na tarehe 03 Mei, 2020
akiwa Chato aliwataka Watanzania kuwa watulivu waondoe hofu ya ugonjwa huu na
ni ugonjwa kama magonjwa mengine, kama vile Malaria, UKIMWI, Kifua Kikuu, n.k.
na kuwataka Watanzania kuchukua tahadhari na kuendelea na shughuli za
uzalishaji mali, kufanya kazi ofisini, viwandani, mashambani na kutofunga
nyumba za Ibada.
41.
Mheshimiwa
Spika,
Mheshimiwa Rais alihutubia tena Taifa tarehe 16 Aprili, 2020 kwa kutoa maelekezo
na kusisitiza yafuatayo:
Mosi: Aliwasihi Watanzania kuondoa hofu kwa
kuwa Mungu yupo nasi na hivyo, waendelee kuchapa kazi ili kunusuru uchumi wa
mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla na kuzingatia kanuni za afya.
Pili: Watanzania watumie
siku tatu kumuomba na kumlilia Mwenyezi Mungu kwani Mungu yu pamoja nasi na
atatusikia huku akiendelea kusimamia kauli yake ya kuwataka Watanzania wafanye
kazi kwa bidii na kumtegemea Mungu bila kujali kauli za kebehi na ukosoaji
kutoka pande mbalimbali za dunia;
Tatu: Alihimiza Watanzania kumtegemea
Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu pekee ndiye atakayetuvusha na
kutuepusha na janga hili;
Nne: Aliwahimiza Watanzania kutopuuza
umuhimu wa tiba mbadala katika mapambano dhidi ya COVID-19. Kauli hii, imekuwa
chachu katika kuimarisha tafiti za dawa za asili ambazo zimekuwa na mchango
mkubwa katika kupambana na maradhi mbalimbali ikiwemo COVID-19; na
Tano: Tarehe 20 Mei, 2020 akiwa Singida,
aliwaomba Watanzania watumie siku tatu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maajabu
aliyoyafanya kwa Taifa letu kwa kutuepusha kusambaa kwa virusi vya COVID-19.
42.
Mheshimiwa
Spika,
hali iliyoko sasa, ni kuwa maambukizi yamepungua na wagonjwa wamepungua
hospitalini. Kama kuna anayestahili sifa ni Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msimamo wake usiotetereka
na maono ya mbali aliyokuwa nayo yamekuwa chachu katika kupunguza maambukizi ya
COVID-19 na kulinda uchumi wa Nchi. Mheshimiwa Rais ameifanya Tanzania kuwa ya
kupigiwa mfano duniani kwa namna alivyoshughulikia ugonjwa huu.
43.
Mheshimiwa
Spika,
pongezi maalum kwa Viongozi wa dini kwa namna walivyoshirikiana na waumini
katika mapambano ya ugonjwa wa COVID-19. Wakati wote Viongozi hao wamekuwa
wakiwapatia waumini (Watanzania) faraja pia na wagonjwa kwamba Mwenyezi Mungu
atawaponya. Hatua hizo zimekuwa mhimili mkubwa wa upendo, umoja, mshikamano na
ujasiri miongoni mwa Watanzania. Tunawashukuru sana.
44.
Mheshimiwa
Spika,
taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (Organisation
for Economic Cooperation and Development - OECD) inabashiri kuwa kitendo cha
kuwafungia watu ndani yaani “Lockdown” kumesababisha vifo kwa njaa na kusinyaa kwa uchumi wa nchi
zilizoendelea kwa asilimia 2 kila mwezi.
45.
Mheshimiwa
Spika,
hivi sasa, nchi nyingi zinakubaliana kuwa “Lockdown”
si hatua sahihi ya kukabiliana na COVID-19. Vilevile, kisayansi inakadiriwa
kuwa nchi ambazo ziliwafungia watu wake na mipaka yake zipo katika hatari ya
kukumbwa na madhara makubwa ya ugonjwa huo pindi utakapotokea mlipuko wa pili
na hata wa tatu.
46.
Mheshimiwa
Spika,
kwa mantiki hiyo, mtizamo na hatua zilizochukuliwa na Tanzania katika kupambana
na COVID-19 zinaonesha upekee tulionao kama nchi. Serikali, inayo kila sababu ya kuwapongeza Watanzania ambao si tu
walipokea maelekezo ya Serikali lakini pia walifanya hivyo kwa uaminifu mkubwa
na kwa hiari yao wenyewe bila kushurutishwa na mamlaka yoyote ya nchi.
47.
Mheshimiwa
Spika,
nitumie fursa hii kuwashukuru wataalamu wetu wa afya kwa kuwahudumia wagonjwa
wa COVID19. Wataalamu wetu hao, walitekeleza majukumu yao bila kujali hatari ya
virusi hivyo kwa maisha yao na wapendwa wao. Vievile, naishukuru sekta binafsi,
mtu mmoja mmoja na wadau wote ambao waliitikia wito wa Serikali kwa kutoa
michango ya hali na mali katika kufanikisha vita dhidi ya COVID19 nchini.
Kipekee, niwashukuru wamiliki wa viwanda ambao waliitikia wito wa Mheshimiwa
Rais na kuanza kuzalisha vifaa kinga hapa nchini badala ya kuagiza nje waende
kufanya hivyo.
48.
Mheshimiwa
Spika,
ni matumaini yetu kwamba zile nchi zilizoondoa vizuizi sasa zinalo somo la
kujifunza kutoka Tanzania. Aidha, suala la kudhibiti maambukizi ya COVID 19
litaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali kwa sasa sambamba na malengo ya muda
mrefu ya kumaliza ugonjwa huo hususan katika kipindi hiki ambacho Shirika la
Afya Duniani (WHO) nalo limebainisha kwamba COVID 19 si gonjwa la kuondoka mara
moja. Hivyo, watu na dunia kwa ujumla hatuna budi kujifunza namna ya kuishi na
virusi hivyo kama ilivyo kwa UKIMWI na virusi vingine, huku tukifanya kazi ili
kujiletea maendeleo.
49.
Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Juni Bunge
lako Tukufu lilipitisha Azimio la kumpongeza na kumuunga mkono Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna
alivyomudu kuivusha nchi katika janga la COVID-19. Waswahili husema mnyonge
mnyongeni, haki yake mpeni. Katika hili, nami naomba niseme kidogo kwa kumpongeza
Mheshimiwa Rais kwa hotuba zake zote zilizohusu ugonjwa huu ambapo alihimiza
masuala muhimu kwa Watanzania katika kukabiliana na janga hili na zilitibu hofu
kubwa iliyokuwa imetanda kwa Watanzania.
50.
Mheshimiwa
Spika,
leo tunaona idadi ya wagonjwa wanaougua inapungua sana. Kwa mfano, taarifa ya
leo, Jumatatu tarehe 15 Juni, 2020 kutoka katika Vituo vya kutolea huduma na Hospitali
za Serikali na Binafsi nchini, inaonesha kuwa tuna wagonjwa 75 katika Mikoa 12
na Mikoa 14 haina wagonjwa ikiwemo Mkoa wa Dodoma, Geita, Kagera, Katavi,
Kigoma, Lindi, Mara, Manyara, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Simiyu, Songwe na Tabora.
Pamoja na mwenendo huu, ninawaomba wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari
zote za kiafya na miongozo inayotolewa na Serikali.
51.
Nampongeza sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb), kwa
kazi kubwa aliyoifanya usiku na mchana kuhakikisha kuwa maambukizi yanapungua
kwa kasi. Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua tuliyofikia. Pia, nawashukuru Katibu
Mkuu, Mganga Mkuu wa Serikali na Watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa usimamizi
wa tatizo hili na naamini mnaendelea vema. Hongereni sana.
SHUGHULI ZILIZOTEKELEZWA
KATIKA BUNGE LA 11 (2015–2020)
52.
Mheshimiwa Spika, wakati Bunge la 11 likielekea kuhitimisha shughuli zake, limefanikiwa
kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kujibu maswali na hoja zilizowasilishwa
na Waheshimiwa Wabunge; kujadili na kupitisha Miswada ya Serikali; Maazimio
mbalimbali yenye kuhusisha Mikataba na Itifaki za Kikanda na Kimataifa; kupokea
kauli za Serikali kuhusu ufafanuzi wa mambo mbalimbali pamoja na kuunda Tume
kwa ajili ya kufuatilia masuala muhimu yenye maslahi mapana kwa Taifa letu.
Maswali na
Majibu
53.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi chote
cha Bunge la 11 linaloelekea
kuhitimisha uhai wake tarehe 16 Juni, 2020 jumla ya maswali ya msingi 3,962 yameulizwa na Waheshimiwa Wabunge
na kujibiwa na Serikali. Aidha, maswali ya nyongeza 9,563 yameulizwa kutokana na maswali ya msingi na kujibiwa na
Serikali. Vilevile, jumla ya maswali 178
ya kawaida na ya nyongeza 162 yameulizwa
na Wabunge na kujibiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kupitia utaratibu wa maswali
ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
54.
Mheshimiwa
Spika,
kupitia Mkutano huu wa Kumi na Tisa, jumla ya maswali 471 ya msingi na mengine 69 ya
nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kupatiwa majibu na Serikali.
Miswada,
Maazimio ya Bunge na Kauli za Serikali
55.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa Serikali
imewasilisha jumla ya Miswada 60 ya
Sheria ambayo imejadiliwa na kupitishwa na Bunge la 11 wakati Sheria 159
zimefanyiwa marekebisho. Vilevile, jumla ya
Maazimio 38 ya Bunge yamejadiliwa na kuridhiwa na Bunge. Pia,
Kauli 20 za
Serikali
zimetolewa ikiwa ni ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyowasilishwa na
Mawaziri. Aidha, Kamati
Maalumu 4 za Bunge zimeundwa katika
Bunge la 11 kwa ajili ya uchunguzi wa masuala mbalimbali.
56.
Mheshimiwa
Spika,
katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu lilipitisha kwa hatua zake zote Miswada
ya sheria sita ambayo ni:
(i)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali (Na.2) wa Mwaka 2020;
(ii)
Muswada wa Sheria ya Afya ya Mimea wa Mwaka
2020;
(iii)
Muswada wa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza
Uvuvi wa Bahari Kuu wa Mwaka 2020;
(iv)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali (Na.3) wa Mwaka 2020;
(v)
Muswa wa Sheria ya Fedha za Matumizi wa Mwaka
2020; na
(vi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020.
Maazimio ya Serikali
57.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali iliwasilisha katika Mkutano huu Maazimio matano ya
Bunge. Maazimio hayo yaliyoridhiwa na Bunge ni kama ifuatavyo:
(i)
Azimio la Bunge la
Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Utoaji Mafunzo na Vyeti vya Wafanyakazi wa
Meli za Uvuvi wa Mwaka 1995 F;
(ii)
Azimio la Bunge la kuitaka Serikali Kutobadili
Uamuzi wa Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi na Shughuli za Serikali;
(iii)
Azimio la Bunge la
Kumpongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa Mafanikio ya
Bunge la Kumi na Moja;
(iv)
Azimio la Bunge la Kumpongeza Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa namna
alivyoliongoza Taifa katika Mapambano Dhidi ya Janga la Ugonjwa wa Corona
(COVID-19);
(v)
Azimio la Bunge Kuhusu Marekebisho ya Kanuni
za Kudumu za Bunge.
Kamati za
Kudumu za Bunge
58.
Mheshimiwa Spika, wakati wa Mkutano huu,
Kamati za Kudumu za Bunge 15 ziliwasilisha Bungeni taarifa za mwaka za kazi.
Taarifa hizo zilisheheni uchambuzi wa kina, maoni, ushauri na mapendekezo
mbalimbali kwa Serikali. Nitumie fursa hii kuwapongeza Wenyeviti, Makamu
Wenyeviti na wajumbe wote wa Kamati hizo kwa kazi nzuri waliyoifanya kuanzia
maandalizi ya kazi za Kamati hadi kuwasilisha taarifa zao katika Bunge lako Tukufu.
UTEKELEZAJI WA MPANGO
NA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2020/2021
59.
Mheshimiwa
Spika,
leo hii tarehe 15 Juni, 2020 Waheshimiwa Wabunge 304 kati ya Wabunge 371 wamepitisha
kwa kishindo Bajeti ya Serikali ya mwaka 2020/2021 ya jumla ya shilingi trilioni 34.88. Kati ya fedha hizo,
shilingi trilioni 21.98 ni za
matumizi ya kawaida na shilingi trilioni
12.90 ni za miradi ya maendeleo sawa na asilimia 37 ya bajeti yote.
60.
Mheshimiwa
Spika,
naomba nitumie fursa hii kuungana na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), Waziri wa Fedha na Mipango, kwa kuwasilisha kwa
umahiri mkubwa Hotuba ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2019 na Mpango wa
Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021 na kuhitimisha hoja hiyo. Ninawapongeza
pia Mheshimiwa Dkt. Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango; Katibu Mkuu; Naibu Makatibu Wakuu na
Watendaji wa Wizara kwa kufanya kazi kwa ushirikiano. Matunda tunayaona.
61.
Mheshimiwa
Spika,
kipekee niwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao
ambayo imesheheni maoni na ushauri mzuri kwa Serikali wakati wa kujadili
makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara mbalimbali kwa mwaka 2020/2021 pamoja
na mjadala kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo
na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021. Nalishukuru Bunge lako Tukufu kwa
kupitisha Bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha kwa kura nyingi za ndiyo.
62.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
ya Awamu ya Tano chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imejipanga vizuri kutekeleza
mipango yote iliyowekwa katika Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka
2020/2021. Nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kuendelea kushirikiana
na Serikali katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Aidha, natoa wito kwa sekta binafsi, wadau wa
maendeleo na wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa
mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.
63.
Mheshimiwa
Spika,
sambamba na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, utekelezaji wa kazi za Serikali
utaendelea. Hivyo, Watumishi wote wa Umma wanashauriwa kuendelea kutekeleza
majukumu yao kwa weledi, uaminifu na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa ufanisi
na tija wakati wote. Aidha, katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango na Bajeti
ya Serikali kwa mwaka 2020/2021, napenda kutoa msisitizo katika maeneo
yafuatayo:
Kwanza: Serikali itaendelea kutekeleza Mpango na
Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021 kwa kuzingatia athari na changamoto za
ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona;
Pili: Serikali itakamilisha mchakato wa
shughuli zilizobaki za maandalizi ya uchaguzi mkuu wa ubunge, urais na udiwani
na kuiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia kikamilifu shughuli zote za
uchaguzi huo kwa uhuru na haki;
Tatu: Serikali itatoa msukumo wa kipekee
katika kukamilisha miradi ya kipaumbele na miradi ya kimkakati inayoendelea
kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tano ili wananchi waendelee kupata huduma
bora;
Nne: Serikali itashirikiana na sekta
binafsi kuleta mageuzi kwa kutekeleza kwa kasi mpango wa kuboresha mazingira ya
biashara na uwekezaji nchini (yaani Blue
Print for Business Environment). Lengo ni kuhakikisha shughuli za uchumi na
biashara zinashamiri na kuchangia kuondoa umaskini nchini; na
Tano: Serikali itaendelea kuboresha huduma
za jamii pamoja na kuhakikisha kwamba ulinzi na usalama unaimarishwa.
UCHAGUZI
MKUU WA MWAKA 2020
64.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi
inaendelea vema na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Hivi sasa, pamoja
na mambo mengine Tume imekamilisha matakwa ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya
kufanya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya
Uchaguzi Mkuu mmoja na mwingine.
65.
Mheshimiwa Spika, zoezi la Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wa awamu ya kwanza lilianza rasmi tarehe 18
Julai, 2019 na kukamilika tarehe 23 Februari, 2020 kwa Nchi nzima wakati awamu
ya pili ilianza tarehe 17 Aprili, 2020 na kukamilika tarehe 05 Mei, 2020.
66.
Mheshimiwa Spika, takwimu za
awamu ya kwanza na ya pili, zinaonesha kuwa wapiga kura wapya walioandikishwa
ni 7,326,552, wapiga kura
walioboresha taarifa zao ni 3,548,846
na wapiga kura 30,487 wamepoteza
sifa. Hadi sasa jumla ya Wapiga Kura halali kwa mwaka 2020 ni 29,804,992 ikilinganishwa na Wapiga
Kura 23,161,440 wa mwaka 2015.
67.
Mheshimiwa
Spika,
Tume inaendelea na uchambuzi wa taarifa za Wapiga Kura waliojiandikisha na
baada ya zoezi hilo kukamilika, Daftari la mwisho litakalotumika katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 litaandaliwa na kuwekwa wazi.
68.
Mheshimiwa Spika, niwasihi viongozi na
wanachama wa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla kuendelea kulinda amani
yetu na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki na wakati wa uchaguzi mkuu.
Natoa wito kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wadau wengine wa uchaguzi
kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni na miongozo iliyopo katika uendeshaji wa
shughuli za uchaguzi.
MICHEZO
69.
Mheshimiwa
Spika, kwa
miaka hii mitano tunaendelea kuonesha upekee wa Mheshimiwa Rais wetu mbali ya
kazi kubwa ya ujenzi wa miradi ya huduma za jamii, pia Mheshimiwa Rais wetu
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amehamasisha masuala ya kijamii ikiwemo michezo.
70.
Mheshimiwa
Spika,
Mheshimiwa Rais ni mwanamichezo na msanii ambaye amekuwa hasiti kuonesha kipaji
chake cha matumizi ya ala ya ngoma. Aidha, wote ni mashahidi kila awapo palipo
na wasanii wanaotoa burudani ya ngoma huwa lazima akaungane nao na kuonesha
umahiri wake kwa kupiga ngoma. Naye anaingia kwenye orodha ya washiriki
waliochomoza kuwa maarufu kwa kumudu kutumia ala hiyo kwa kipindi hiki cha
miaka mitano.
71.
Mheshimiwa
Spika,
kwa upande wa michezo na burudani tunao Watanzania waliofanya vizuri kwenye
eneo hilo katika kipindi cha miaka mitano. Ikumbukwe kuwa ninaowazungumzia hapa
ni baadhi ya wanamichezo na wasanii waliolibeba Taifa letu na kupeperusha vema
bendera ya Taifa nje ya Nchi.
72.
Mheshimiwa
Spika,
kwenye michezo ya riadha ni muhimu tukampongeza kijana wetu Alphonce Felix
Simbu aliyetuletea medali ya fedha na kupeperusha vyema bendera ya Taifa kwenye
mashindano ya mbio ndefu ya majeshi ya Dunia yaliyofanyika nchini China. Wanamichezo
wengine waliochomoza nje ya nchi ni pamoja na Mwanamasumbwi Hassan Mwakinyo
aliyemtwanga Sam Eggington wa Uingereza kwa knock out katika Raundi
ya 2 na kupeperusha Bendera ya Taifa huko Uingereza.
73.
Mheshimiwa
Spika,
eneo la sanaa na burudani hususan muziki wa Bongo Flavour limekuwa na mchango
mkubwa katika kuitangaza nchi yetu. Natumia fursa hii kuwapongeza vijana wetu ambao
ni wasanii wa muziki wa Bongo Flavour akiwemo Naseeb Abdul
Juma maarufu kama Diamond Platnumz (Simba)
pamoja na Rajabu Abdul Kahali maarufu kama Harmonize
(Konde boy–Tembo). Tumekuwa tunashuhudia mapokezi wanayopata huko nje na
wakitumbuiza muziki wetu na kupeperusha Bendera yetu kwenye mataifa mbalimbali.
Wako wengine wengi kama Vanessa Mdee, Raymond Mwakyusa (Rayvanny), Ali Kiba
(King Kiba), n.k.
74.
Mheshimiwa
Spika,
mchezo wa soka nao licha ya kuwa ndio mchezo unaoongoza kwa wapenzi hapa nchini
pia umetoa vijana wengi nje wanaoiletea sifa nchi yetu. Kwa upande huu wa soka,
sote tumpongeze kijana wetu Mbwana Samata anayelitangaza Taifa letu katika ligi
kuu ya Soka nchini Uingereza kwenye Timu ya Aston
Villa. Tunawapongeza sana wachezaji wetu kama Simon Msuva, Hassan Kessy, Abdi
Banda, Kelvin John, n.k. ambao wanatangaza Taifa letu nje ya nchi. Ni matarajio
yetu wapo watakaofuata nyayo zao ili kuliletea sifa Taifa letu.
75.
Soka la Vijana nalo limeendelea kuimarika
ambapo Timu za Soka za Vijana wa umri wa miaka 17 na 20 na Timu ya Wanawake – Twiga Stars, zimefanya vizuri katika
michezo ya kimataifa na kuleta makombe hapa nchini.
76.
Mheshimiwa
Spika, Taifa Stars nayo
katika kipindi cha miaka 39 imeweza kucheza AFCON mara ya pili katika kipindi
cha miaka mitano hii.
77.
Mheshimiwa
Spika,
katika kipindi hiki cha miaka mitano, tumeshuhudia Klabu kongwe ikipeperusha
Bendera ya Taifa nje ya nchi na ikitutoa kimasomaso katika medani za soka la
kimataifa kwa kuweka historia ya Taifa letu kwa kucheza hatua ya robo fainali
ya Mabingwa wa Afrika baada ya kufuzu hatua ngumu ya makundi nayo si nyingine
bali ni SIMBA SPORTS CLUB, Klabu
ambayo inakaribia kutangaza ubingwa wa Tanzania kwa Ligi ya ndani kwa mara ya
tatu mfululizo ikiwa haijakamilisha michezo 9.
78.
Mheshimiwa
Spika,
kama inaweza kutangaza ubingwa ikiwa haijamaliza michezo yote hiyo nini faida
ya mkuki. Mheshimiwa Spika, ili kuonesha ubora wa Timu mchezaji anayeongoza kwa
kufunga magoli mengi ni Medie Kagere aliyefunga magoli 19 kutoka SIMBA SPORTS
CLUB na wachezaji wanaofuatia kwa magoli mengi ni Reliants Lusajo wa
Namungo FC magoli 11; Yusuph Mhilu
wa Kagera Sugar magoli 11;
Bigirimana Bleiz wa Namungo FC magoli 10
na Paul Nonga wa Lipuli FC magoli 10.
Hatua hii haiwezi kufikiwa na Timu yoyote kwa kuwa mikuki mingi ni butu. Mkuki
wenye ncha kali uko SIMBA SPORTS CLUB.
HITIMISHO
79.
Mheshimiwa
Spika, nihitimishe hotuba yangu kwa kumshukuru tena
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa uongozi wake makini uliolipatia Taifa letu mafanikio makubwa
katika kipindi kifupi cha miaka mitano. Watanzania wanakuhitaji kuliongoza
Taifa hili. Nitoe wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi ili tumpigie kura za
kutosha.
80.
Mheshimiwa
Spika,
naomba kwa mara nyingine niwashukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa
kusimamia vema utekelezaji wa Ilani ya CCM.
81.
Mheshimiwa
Spika,
vilevile, namshukuru sana Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd, Makamu wa Pili wa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ushirikiano ambao amekuwa akinipatia
wakati wote wa kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
82.
Mheshimiwa
Spika,
narudia tena kukushukuru na kukutakia afya njema. Namshukuru pia Mheshimiwa
Prof. Ibrahimu Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania kwa ubunifu wake wa kuendesha
shughuli za Mahakama kwa njia ya mtandao katika kipindi cha ugonjwa wa COVID-19.
Namshukuru pia Mheshimiwa Dkt. Eliezer Feleshi, Jaji Kiongozi, Waheshimiwa
Majaji wote, Mahakimu na watendaji wote wa mhimili wa Mahakama kwa kazi nzuri
ya kuwahudumia Watanzania.
83.
Mheshimiwa
Spika,
nitumie fursa hii kuwashukuru tena Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Ofisi ya
Waziri Mkuu, Makatibu Wakuu pamoja na Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi zilizopo
chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wafanyakazi wote kwa ushirikiano mkubwa
wanaonipatia katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
84.
Mheshimiwa Spika, napenda pia
kuwashukuru washirika wa maendeleo zikiwemo Nchi rafiki, Taasisi na Mashirika
ya Kimataifa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa
kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga uchumi wa viwanda na kuiletea Nchi yetu maendeleo. Ninawashukuru
pia, Viongozi wote wa dini na wanahabari wote kwa ushirikiano mkubwa
waliouonesha kwa Serikali katika kipindi chote cha miaka mitano. Mchango wao
umekuwa muhimu katika kuiwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa kimaendeleo
kulingana na mipango tuliyojiwekea.
85.
Mheshimiwa
Spika,
katika kipindi hiki cha miaka mitano tumekuwa karibu sana na kupata ushirikiano
mkubwa kutoka kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi katika ngazi zote. Hivyo, Mheshimiwa
Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa pamoja na Dkt. Bashiru Ally,
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi; nawashukuru sana Viongozi wangu wa CCM kwa
kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Ilani ya Chama chetu.
86.
Mheshimiwa
Spika, kabla
sijafika mwisho, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano wao
mkubwa katika kuishauri Serikali. Pia ninawashukuru Watumishi wote wa Bunge kwa
huduma nzuri na msaada ambao wamekuwa wakitupatia kipindi chote tulichokuwa
hapa Bungeni. Aidha, ninawashukuru Watendaji wote wa Serikali na Taasisi
mbalimbali kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, umahiri na ufanisi
mkubwa na hivyo kufanikisha utekelezaji wa shughuli zilizopangwa na Bunge bila
kuwasahau Wanahabari kwa uchambuzi na kuuhabarisha umma na Madereva wote
walituhudumia wakati wote wa shughuli za Bunge
87.
Mheshimiwa
Spika,
kipekee, nitumie nafasi hii kuishukuru tena familia yangu ambayo imeweza
kunivumilia wakati mwingi nilipokuwa nikitekeleza majukumu yangu ya kitaifa.
Namshukuru sana mke wangu Mary Majaliwa na watoto wangu kwa kuniombea, na kunitia
moyo wakati wote ninapokuwa nikitekeleza majukumu yangu.
88.
Mheshimiwa
Spika,
katika utekelezaji wa majukumu ya Waziri Mkuu inawezekana kabisa kwa namna moja
au nyingine niliwakwaza baadhi ya viongozi na watendaji, lakini yote ni katika
kutekeleza majukumu ya Waziri Mkuu. Imani yangu ni kwamba tutaendelea kulijenga
taifa kwa pamoja hususan katika kipindi hiki tunachoelekea kwenye
kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu.
89.
Mheshimiwa
Spika,
mwisho wa Bunge hili, ndiyo kiashiria cha Bunge lijalo. Hivyo, nawaaga wote kwa
kuamini kuwa wale waliofanya vema katika kipindi hiki wataaminiwa tena na
wananchi na kurejea kwenye Bunge lijalo. Hivyo, tuombeane heri ili kila mmoja
wetu atakayechukua fomu za kugombea tena apate ushindi na fursa ya kuwatumikia
wananchi.
90.
Mheshimiwa
Spika,
naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment