Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
Serikali kupitia Wizara ya Maji imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika maeneo ya mijini na vijijini kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002.
Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 inaelekeza kuwapatia wananchi waishio vijijini maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao, hatua inayolenga kuwaondelea changamoto mbalimbali ikiwemo maskini na magonjwa yanayosababishwa na maji.
Wizara ya Maji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini kwa kujenga, kupanua na kukarabati miradi ya maji, lengo ikiwa ni kufikia asilimia 85 ya wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya vijijini ifikapo mwaka 2020.
Miradi ya Maji Vijijini inatekelezwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na wananchi pamoja na sekta binafsi ambapo katika kuwapunguzia wananchi gharama, Serikali kwa kushirikiana na wadau inaandaa mifumo itakayofaa kusimamia na kuendesha miradi ya maji ikiwa ni pamoja na kuviimarisha Vyombo vya Watumiaji Maji.
Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi inatekeleza miradi mbalimbali ya maji katika vijiji mbalimbali vya Wilaya hiyo hatua inayolenga katika kutoa huduma endelevu kwa wakazi waishio mijini na pembezoni mwa miji.
Wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama kutoka katika vyanzo vya Visima vifupi, Visima vya kati, Visima virefu ambavyo vimefungwa pampu za mikono, miradi ya maji bomba ya maporomoko na miradi ya maji ya kusukumwa na mitambo.
Tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini imeongezeka kutoka 38.5% mwaka 2015 hadi kufikia 51.20% kufikia mwezi Novemba, 2018 ikiwa ni ongezeko la 12.7% ambapo jumla watu 64,498 waishio vijijini wanapata huduma ya maji.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Maji wa Naunambe-Mpekenyera unaosimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kushirikiana na Kamati za Vijiji vya Naunambe na Mpekenyera katika kuhakikisha kuwa Serikali inamtua mama ndoo kichwani na kumuondolea changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji.
Kufuatia juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Wilaya ya Ruangwa mradi huo ulikamilika mwezi Juni, 2018 na jumla wananchi 7,000 wameanza kupata maji na salama na kiasi Tsh. Milioni 828 zimetumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo ununuzi wa vifaa mbalimbali ikiwemo mashine za kusafisha maji na miundombinu mbalimbali kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa maji kutoka katika vyanzo na kuwafikia wananchi.
Akizungumza na Timu ya Maafisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO) waliofanya ziara Wilayani humo, hivi karibuni, Katibu wa Mradi huo, Selemani Nyamiri anasema mradi huo ulianza kuibuliwa na wananchi mwaka 2010 kwa kaya mbalimbali katika vijiji hivyo kuchangishana fedha kwa ajili ya kuhakikisha mradi huo unatoa huduma endelevu ya maji katika vijiji hivyo vyenye wakazi zaidi ya 10,000.
‘Maji yaliyokuwa yakizalishwa katika chanzo cha Mpekenyeara yalikuwa yana chumvi sana, pia yalipatikana katika vyanzo visivyo safi na salama hivyo ilitulazimu kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya kutumia mafundi na utaalamu wa ziada ili kuhakikisha kuwa maji yanarejea katika ubora wake’’
Nyamiri anasema kwa sasa kiwango cha chumvi katika maji hayo kimepungua na kufanya maji hayo kuwa na ubora wa matumizi kwa binadamu, ambapo watumiaji wanalazimika kuchangia gharama ya Tsh. 200 kwa kila ndoo, ikiwa ni fedha zinazokusanywa na kamati hiyo kwa ajili ya kufanya matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya mradi.
Akifafanua zaidi anasema wananchi wa vijiji hivyo wataendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za maendeleo ya jamii ikiwemo huduma ya maji ambapo wananchi wamekuwa na mwamko wa kusimamia uhifadhi wa maeneo ya vyanzo vya maji ili kufanya vijiji vyote vinapata maji ya uhakika.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Naunambe Bi. Amina Abdalla aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa umeondoa kero kwa akina mama wa vijiji hivyo waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.
Bi. Rehema Mussa Mkazi wa Kijiji cha Mpekenyera alisema kwa kipindi cha nyuma hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika vijiji hivyo haikuwa ya kuridhisha, hususani wakati wa kipindi cha kiangazi na kuwalazimu wananchi wengi kutembea umbali wa kilometa 3 kufuata huduma ya maji katika vyanzo visivyo rasmi huku wakitembea na watoto migongoni.
‘Utekelezaji wa mradi huu ni mkombozi mkubwa sana kwetu wananchi wa Naunambe na Mpekenyera kwani kwa sasa shida ya maji imeisha, tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Mbunge wetu wa Ruangwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa’’ alisema Rehema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Andrea Chezue alisema hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya hiyo umefikia asilimia 55 huku kukisaliwa na maeneo machache ambayo yanakosa huduma ya maji ambapo Ofisi yake imekuwa ikiendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha huduma ya maji inafikia walau asilimia 70 ifikapo mwishoni mwaka 2020.
‘Halmashauri ya Ruangwa inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji katika vijiji mbalimbali ikiwemo mradi wa maji wa Naunambe-Mpekenyera wananchi wanapata maji na wanafurahia huduma inayotolewa kwa mwaka 2019 pekee tulipata miradi minne ikiwemo mradi wa maji Kitandi na tayari tumeanza kufanya mawasiliano na Halmashauri ya Mtama kuhakikisha kuwa maji yanafikishwa katika vijiji jirani ikiwemo vijiji vya Nangumbu A na B’’ alisema Chezue.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maji Kata ya Mandawa Rashid Mshamu anasema mradi wa maji mandawa unahuhudumia jumla ya vijiji 5 vya Nahanga, Chikundi, Mandawa Chini, Mchichili na Mtondo unaogharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 1.7 zilizotolewa na Serikali, ambapo mradi huo unawanufaisha jumla ya watu 13,756.
Anaongeza kuwa mradi huo ulioasisiwa mwaka 1975 ulikuwa na miundombinu chakavu na kusababisha kero kubwa kwa wananchi hususani wazee, wanawake na watoto ambapo walikuwa wanahangaika, ambapo Serikali iliamua kuufua mradi huo katika bajeti ya mwaka 2014/15.
Anasema kuwa kwa sasa mradi huo unaendelea vyema na huduma ya maji ni ya uhakika na wananchi wa vijiji hivyo wanalazimika kuchangia kiasi cha Tsh. 50 inayopelekwa katika mfuko wa maji wa kijiji hicho na kutumika kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya mradi.
Miradi mingine ya maji inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ni pamoja na mradi wa maji Nanganga, mradi wa maji Likunja, mradi wa maji Namahema, mradi wa maji Chenjele, ambapo katika maeneo yote hali ya upatikanaji wa maji ni ya kurithisha.
Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mibure, Namakuku na Namahema ambao tayari umekamilika na jumla ya watu 6,133 wananufaika, ambapo kiasi cha Tsh. Milioni 631,593,444.50 zimetumika.
Serikali imewekeza katika miradi ya maji mikubwa na midogo ili kufikisha huduma ya maji kwa wananchi, ambapo uwekezaji huo umeleta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali nchini na maisha ya wananchi kwa ujumla.
Ili kuleta matokeo tarajiwa utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji hapa nchini unahusisha ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi na pia wadau wa maendeleo kutokana na ukweli kuwa Serikali imeweka lengo la kufakisha huduma ya maji kwa asilimia 85 kwa upande wa wananchi.
Kazi nzuri go on comrades
ReplyDelete