Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Sweetbert Njewike, akizungumza na viongozi wa dini na wadau wengine (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Veta mkoani hapa jana.
Boniphace Jilili na Dotto Mwaibale, Singida.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Sweetbet Njewike ametoa rai kwa wananchi wa mkoa huo kujiepusha na makundi yanayolenga kuleta uvunjifu wa amani katika kipindi cha uchaguzi.
Kamanda Njewike alitoa rai hiyo jana alipokutana na viongozi wa dini mkoani hapa na wadau wengine katika makundi mbalimbali kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Veta.
Aliyataka makundi mbalimbali yakiwemo ya Vijana kutojiingiza kwenye makundi yanayolenga kuleta uvunjifu wa amani katika kipindi cha kampeni,wakati wa zoezi la kupiga kura na matokeo kwani jeshi la polisi limejipanga sawasawa.
"Askari watakuwepo kwenye maeneo yote kunakofanyika kampeni na kila kituo cha kupigia kura na sio kwamba watakuwepo kutisha wananchi hapana ni kuhakikisha wanalinda amani na usalama wa wananchi." alisema kamanda.
Njewike alisema maendeleo ambayo yapo mkoani hapa yanatokana na amani iliopo, hivyo amewaomba Viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao kuzingatia sheria na taratibu wasije wakajikuta wako mikononi mwa vyombo vya sheria.
"Mkiwahimiza na kuwafundisha waumini wenu kuacha dhambi wakiacha watakuwa wametii sheria za nchi." alisema Njewike.
Aidha aliwasisitiza viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na ambayo yamekwisha tolewa na tume ya uchaguzi ikiwemo muda wa kuanza na kumaliza kampeni.
Nao wadau na Viongozi wa dini walipongeza hatua hiyo huku wengine wakiomba maelekezo hayo yatolewe na maaskari kwenye makanisa na misikitini licha ya kuwepo wawakilishi ambao ni viongozi hao.
Kwa upande wake Sheikh Issa Nassoro alisema anaamini kiongozi wa dini akimfundisha kwa unyenyekevu mtu akiwemo mwanasiasa ukiukwaji wa sheria hautakuwepo.
"Wapo wanasiasa ambao dhamira zao ni kuwasaidia wananchi lakini pia tufahamu wapo ambao wanatumiwa na watu/nchi kuleta machafuko,ni wajibu wetu sisi viongozi kuwakemea watu wa namna hiyo." alisema sheikh Nassoro.
Wengine waliwataka wanasiasa na wananchi kufahamu kuwa kuna maisha baada ya kupita uchaguzi, hivyo wasije wakakatisha maisha yao kwa jambo ambalo ni la mda mfupi,huku wakiwaomba wanasiasa kuwa wastaarabu wanaponadi sera za vyama vyao ili kuepuka uvunjifu wa amani.
No comments:
Post a Comment