Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali ya CCM imedhamiria kuhakikisha kilimo kinamnufaisha mkulima wa Tanzania.
"Watu wasije kuwadanganya kwamba Serikali haiwajali, siyo kweli. Kuna sababu zilizochangia kuyumba kwa bei ya kahawa kwenye soko la dunia."
Ametoa kauli hiyo mchana (Jumatatu, Septemba 28, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Rubale kwenye mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Rubale, wilayani Bukoba, mkoani Kagera.
"Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, iliazimia kufufua mazao matano ya kimkakati ambayo ni kahawa, pamba, korosho, chai na tumbaku. Mazao haya bei ilishuka na si katika zao la kahawa tu."
"Kuyumba kwa bei haikuwa katika zao la kahawa tu bali katika mazao mengine kama pamba na korosho. Kahawa bei yake iliathirika kwa sababu ya ugonjwa wa Corona. Korosho bei ilishuka kutoka sh.3,300 hadi sh. 1,900. Pamba pia ilishuka bei," amesema.
Amesema Kenya ndiko mnada wa kahawa huwa unafanyika lakini hadi sasa bado wanasumbuliwa na ugonjwa wa Corona kwa hiyo haikuwa rahisi kufanya biashara katika kipindi chote hicho.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewapokea wanachama 20 kutoka Chama cha Demokrasia (CHADEMA) ambao wameamua kurudi CCM.
Wanachama hao wameongozwa na Mwenyekiti wa Vijana wa CHADEMA wa Mkoa wa Kagera, Bw. Francis Mutachunzibwa ambaye pia alimtambulisha Naibu Katibu Mkuu wa BAVICHA, Bi. Getrude Ndibalema ambaye alijiuzulu uongozi tangu mwaka jana.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bw. Mutachunzibwa alisema: “Ninaijua vizuri CHADEMA, nilipotea, nilitenda dhambi lakini sasa nimeamua kurudi nyumbani, nipokeeni.”
“Ninawaomba wana-Bukoba tumchague Dkt. Magufuli, mashine ya kusaga na kukoboa, jembe la nguvu. Kuanzia kesho, nitamnadi yeye na Advocate Byabato hadi kieleweke.”
Akizungumza na maelfu ya wakazi wa mji wa Bukoba leo jioni (Jumatatu, Septemba 28, 2020) waliojitokeza kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Mheshimiwa Majaliwa aliwataka wakazi hao wajitafakari sana wanapofikiria kumchangua mtu wa kuongoza nchi.
“Tunataka kiongozi mwenye hofu ya Mungu na ili umpate ni lazima umjue historia yake. Kuongoza nchi si lelemama, kiongozi wa nchi ni Mkuu wa Nchi, tena ni Mkuu wa Majeshi.”
No comments:
Post a Comment