Wakati akitoa tamko hilo kwa niaba ya kamati, Kaimu Katibu Mtendaji wa kamati hiyo Mchungaji Emanuel Adam Sikazwe wa Kanisa la Monravian alisema kuwa amani ni tunu pekee ambayo watanzania wamepewa na Mwenyezi Mungu na hivyo wana kila sababu ya kuiheshimu, kuilinda na kuitunza ili isitoweke wala kuvunjika.
Aidha, aliwataka vijana kujiepusha na vishawishi vya maandamano, pamoja na kutumika kuanzisha fujo kwani kwa kufanya hivyo mkono wa sheria utawakabili na kutahadharisha kuwa endapo vurugu hizo zikitokea watakaoathirika ni wale wasio na nguvu na wasiojiweza.
“Sisi viongozi wa dini kama wadau wa amani tumekubaliana kuwa na siku maalum ya kufanya maombi kwaajili ya amani kabla ya siku ya uchaguzi ya tarehe 28.10.2020, siku maalum iliyoandaliwa na kamati hii ni siku ya Jumatatu ya tarehe 26.10.2020 na maombi haya pamoja na dua vitafanyika kwenye viwanja vya Sekondari ya Kizwite kuanzia saa tatu asubuhi, hivyo tunawasihi raia wa dini zote kuhudhuria siku hiyo ili kuungana pamoja kumuomba Mwenyezi mungu kuwaleta viongozi waliochaguliwa na kutuondolea ghasia na fujo zitakazoweza kujitokeza siku hiyo ya uchaguzi.”
“Upande wa viongozi wa dini, imebainika kunawatu wanaojitokeza wakiungana na watu wanaohamasisha vijana kufanya fujo ili waweze kuandamana kipindi cha uchaguzi, sisi kama viongozi wa Kamati ya Amani ya Mkoa, tunawaomba viongozi wote wa kidini wasijihusishe kabisa na siasa katika kuelekea uchaguzi mkuu.” Alisisitiza
Hayo yamejiri baada ya wajumbe wa kamati hiyo kukutana na kutoa tamko la pamoja kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa pamoja na wadau wote wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi kuzingatia misingi ya sheria na kuheshimu taratibu zilizowekwa katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Askofu Ambele Mwaipopo wa kanisa la KKKT alisisitiza kuwa kamati inatoa tamko hilo kwa nia njema hasa kwa kujali amani nchini tunu ambayo nchi imepewa na Mwenyezi Mungu na wana wajibu wa kuiendeleza wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi ili shughuli za wananchi ziendelee kwa usalama
Halikadhalika, mmoja wa viongozi wa Taasisi ya Istiqama Mkoani Rukwa Sheikh Ali Baruti alisema kuwa nafasi yao kama viongozi wa dini nchini ni kuendeleza kuhimiza suala la amani na kuongeza kuwa hakuna asiyefahamu umuhimu wa amani kabla ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.
No comments:
Post a Comment