Matokeo chanyA+ online




Thursday, October 15, 2020

RC NCHIMBI: VIJANA TUMUENZI NYERERE KWA KUJIFUNZA HISTORIA


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na makundi mbalimbali ya vijana waliohudhuria katika Kongamano la Kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye eneo la Chuo cha Uhasibu mkoani hapa.

RC Nchimbi akikabidhi zawadi ya Rozari Takatifu kwa vijana waliohudhuria Kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere kwenye Chuo cha Uhasibu mkoani hapa, kama ishara ya heshima kwa mama huyo wa Yesu, ambaye Waumini wa Kanisa Katoliki na marafiki wa karibu hupata fursa ya kumkumbuka kwa kusali rozari kila ifikapo mwezi Mei na Oktoba kila mwaka.

Mratibu wa Kongamano hilo na Afisa wa Vijana kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Frederick Ndahani akizungumza na vijana wa mkoa huo kabla ya kumkaribisha RC Nchimbi kufungua kongamano.

Mwakilishi wa Vijana Omary Mwangi, akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi zawadi ya Kitabu cha Historia ya Mwalimu Nyerere.
Vijana mkoani hapo wakimkabidhi mama Nchimbi picha ya Mwalimu Nyerere iliyochorwa kwa umahiri mkubwa na vijana wa mkoa.

Washiriki wakisikiliza kwa makini nasaha za Mkuu wa Mkoa (hayupo pichani)

Kongamano likiendelea.

Washiriki wakisikiliza kwa makini nasaha za Mkuu wa Mkoa (hayupo pichani)

Kongamano likiendelea.

Washiriki wakisikiliza kwa makini nasaha za Mkuu wa Mkoa (hayupo pichani)

Mmoja wa Wawezeshaji wa Kongamano hilo, Jacob Kanka akitoa mada

Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi amewataka vijana kuanza kufikiri ‘sawa-sawa- katika muktadha wa kuongozwa na tafakuri ya kina kujua na kuona sawa-sawa historia ya taifa la Tanzania lilipotoka, lilipo na linapoelekea.

Alisema kama vijana watafikiri sawasawa ni lazima watakuwa na upeo mkubwa wa jicho la kuona sawasawa mnyororo mzima wa hatua kadhaa za kimaendeleo zilizofikiwa hatua kwa hatua tangu uhuru

Nchimbi alitoa nasaha hizo wakati akizungumza na vijana mbalimbali jana, kupitia  ‘Kongamano la Kumbukizi ya Baba wa Taifa 2020, lililofanyika jana kwenye Chuo cha Uhasibu mkoani hapa

“Tusipofanya tafakuri ya kina hata tafsiri ya vitu vinavyofanywa na serikali hatutaviona, na matokeo yake itakuwa ni rahisi sana kudanganywa na wapotoshaji wasiolitakia mema taifa letu,” alisema Nchimbi na kuongeza: “Kijana ukifikiri sawasawa utaona sawasawa, utatekeleza sawasawa na utaamua sawasawa.”

Mkuu wa Mkoa aliwaambia vijana kuwa bila ya kumfahamu vizuri na kumtazama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kamwe hawawezi kuwa kiunganishi mahiri kwenye mnyororo wa kiuchumi kutoka kwenye Uchumi wa Kati kwa sasa, kuelekea uchumi wa Juu wa Kati

“Vijana ndio watendaji, na kumbukeni miradi yote hii mikubwa ya kitaifa inayotekelezwa na serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na kipenzi chetu Rais John Pombe Joseph Magufuli inafanyika kwa fedha zetu za ndani na zaidi ni kwa manufaa yenu vijana…fikirini sawasawa ili muone sawasawa,” alisema

Mama Nchimbi alisema Tanzania ni urithi wetu tulioachiwa na Baba wa Taifa, hakuna urithi mwingine, hivyo vijana wanapomkumbuka wana jukumu la kumuenzi kwa kusimama vizuri, kuwa na uzalendo na kujifunza historia ya nchi, ili hatimaye kwenda kwa kasi na tija inayodhihirika katika kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa juu wa kati

“Kijana huwezi kujiangalia wewe bila ya kumtazama Baba wa Taifa…Nyerere ni alama muhimu sana, ili tushiriki ipasavyo kwenye uchumi huu wa kati ni lazima tuijue historia ya tulipotoka kati ni dhahiri tutakuwa na majawabu ya je…hatua hii ya uchumi wa kati, amani na uhuru vinaamanisha nini?..na ni lazima twende katika fikra zitakazotuonyesha sisi ni taifa la Tanzania na sio vinginevyo,” alisema Nchimbi.

Awali, Mratibu wa Kongamano la Kumbukizi ya Baba wa Taifa 2020, Frederick Ndahani, alisema Mwalimu Nyerere aliwahi kunukuliwa akisema “Mjenga nchi ni Mwananchi na Mvunja nchi ni Mwananchi” hivyo kama vijana wanathamini sana amani, na kamwe hawatavunja miiko wala kutumika na yeyote kwa maslahi yake binafsi, kuvuruga amani na utulivu uliopo.

“Sisi vijana wa mkoa huu tumeshuhudia maono ya Baba wa Taifa yakiwa yanatekelezwa kwa kasi katika serikali hii ya Awamu ya Tano kwenye Elimu, Afya, Maji, Kilimo, Madini, Mawasiliano, Miundombinu, Nishati na miradi mingine mingi…hii inatupa taswira na matumaini makubwa kama vijana katika mustakabali wa maisha yetu kwa sasa na vizazi vijavyo,” alisema Ndahani.

Ndahani ambaye ni Afisa Vijana wa Mkoa, na mmoja wa vijana shupavu waliokimbiza Mwenge wa Uhuru nchi nzima kwa mwaka 2017, alisema kama vijana wanajivunia na kutambua mchango mkubwa wa maendeleo katika sekta mbalimbali, uliofanywa na viongozi wa Taifa la Tanzania kuanzia Mwalimu Nyerere mpaka sasa chini Rais John Magufuli.

“Tunawashukuru sana viongozi wetu kwa maono na hatimaye kutufikisha kwenye uchumi huu wa kati. Na kipekee kwa niaba ya vijana wa mkoa huu namshukuru sana Rais Magufuli kwa busara na hekima za alizojaliwa Mwenyezi Mungu kwa namna alivyofanikiwa kulivusha salama taifa hili dhidi ya janga hatari la Corona,” alisema Ndahani na kuongeza:

“Miongoni mwa wahanga wakubwa wa gonjwa hili tulikuwa ni sisi vijana, lakini leo hii kwa ushupavu na ujasiri wa Rais Magufuli tunaendelea kama kawaida na masomo yetu kwenye shule na vyuo vyote nchi nzima, lakini pia tunaendelea kujiachia kwa kukusanyika kama hivi leo…katika kujadili na kukumbushana majukumu yetu kama vijana kwa mustakabali chanya wa Taifa letu,” alisisitiza Ndahani.  

No comments:

Post a Comment