Matokeo chanyA+ online




Monday, October 26, 2020

SINGIDA YATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI BIASHARA USAFIRISHAJI BINADAMU


Katibu wa Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu, Seperatus Fella, akiweka mkakati wa namna bora ya kukabiliana na biashara hiyo, alipokutana na wadau mbalimbali kwenye mafunzo maalumu mkoani Singida juzi.

Afisa wa Sekretarieti hiyo, Ahmad Said Mwen-dadi, akitoa mada kwenye mafunzo hayo.

wa Sekretarieti hiyo, Alex Lupilya akitoa mada kwenye mafunzo hayo.

Picha ya Pamoja ya baadhi ya wadau walioshiriki mafunzo hayo.

Na Godwin Myovela, Singida

Wakazi mkoani hapa wametakiwa kuwa makini kabla ya kuwaruhusu mabinti kuchukuliwa na kupelekwa maeneo mbalimbali nchini kwa kigezo cha kutafutiwa au kufanya kazi za ndani, badala yake wahakikishe kwanza wanahusisha uongozi wa Serikali ya Mtaa husika ili mchakato huo ufanyike kihalali.

Pia ‘dalali’ au mtu yeyote anayetaka kumchukua binti yako hakikisha anakuwa na mdhamini wa kuwezesha kurahisisha  mawasiliano ya mara kwa mara, lengo hasa ni kuwa na uhakika wa mazingira ya usalama wa mwanao huko aendako.

Katibu wa Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu, kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Seperatus Fella aliyasema hayo jana mkoani hapa, wakati akitoa mafunzo kwa wadau mbalimbali ya namna ya kupambana na biashara ya usafirishaji binadamu.

“Singida ikitanguliwa na Wilaya ya Kondoa Dodoma ni miongoni mwa mikoa ambayo wasichana wanachukuliwa na kwenda kutumikishwa kwa kufanyishwa biashara za ngono kwenye majiji kama Dar es Salaam na kwingineko,” alisema Fella.

Aliongeza kwamba tangu kuanza kwa mafunzo hayo kwa kushirikiana na mashirika ya kitaifa na kimataifa mwaka 2017, mkoa wa Singida ulikuwa bado haujafikiwa, na kinachofanyika kupitia mafunzo hayo ni kuwaelekeza wadau mbinu bora za kuzuia na kukabiliana kisheria na biashara hiyo haramu.

 Fella pamoja na mambo mengine, alisema kwa muktadha wa kitaifa hali siyo ya kuridhisha sana kutokana na mabinti wengi kuendelea kusafirishwa nje ya nchi kwa siri, kwa ahadi za kutafutiwa ajira zenye mshahara mnono jambo ambalo sio kweli, na kinyume chake hugeuzwa watumwa kwa kufanyishwa biashara za ngono na madawa ya kulevya kwa maslahi ya waliowasafirisha.

“Tunaendelea na juhudi za kuwaokoa, na hivi karibuni tumewaokoa mabinti wa kitanzania waliokuwa wakitumikishwa kama watumwa kutoka Iraq, Malaysia na India…na wametueleza kuwa bado wamewaacha wenzao wengi wakiendelea kuteseka,” alisema Fella.

Kwa upande wake Afisa wa Sekretarieti hiyo, Ahmad Mwen-Dadi, alisema biashara hiyo ni ya tatu kwa kuingiza fedha nyingi ikitanguliwa na ile ya Madawa ya Kulevya na Uuzaji wa Silaha Haramu, hivyo ni jukumu la kila raia wa Taifa la Tanzania kuchukua tahadhari kwa ulinzi madhubuti wa watoto na mabinti kuanzia kwenye ngazi ya familia.

Alisema madalali wa biashara hiyo wanapokutana na mabinti wamekuwa wakiwahadaa kwenda kufanya kazi kwenye mahoteli makubwa, maduka makubwa (supermarkets), Saluni na kazi nyinginezo zenye maslahi makubwa, jambo ambalo hatimaye huwashawishi mabinti walio wengi kutoroka bila kuaga wazazi.

“Wengi wanasafirishwa kupelekwa nchi za Thailand, China, Malaysia, Bangladesh na hata Iraq na wakifika huko wanajikuta kazi walizohaidiwa sio wanazifanya. Wengi tuliowaokoa wanasema wenzao wapo katika hali mbaya ya kutumikishwa kikatili mpaka pale watakapomaliza kulipa deni la gharama za kuwasafirisha hadi kufika kwenye hizo nchi,” alisema Mwen-Dadi.

Aidha, alitoa tahadhari kwa wana-singida na taifa kwa ujumla kuwa makini kutokana na ukweli kwamba kwa sasa usafirishaji wa ndani kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine hadi Zanzibar umeuzidi ule usafirishaji wa watoto na mabinti wa kitanzania kupelekwa nje.

“Naomba sana tuwe makini, bado hatujafikia umasikini wa kuacha watoto na mabinti zetu kwenda kudhalilishwa na kufanyiwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu. Mapambano dhidi ya biashara hii haramu ni jukumu letu sote kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa,” alisema.

Wadau waliopata fursa ya kushiriki mafunzo hayo ni Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka Singida, Mashirika yasiyo ya kiserikali, kikiwemo Kituo cha Faraja na Jeshi la Wokovu, Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Maafisa Serikali za Mitaa.

Mafunzo hayo pamoja na mambo mengine yanalenga kuelimisha na kutoa taswira ya namna bora ya kukabiliana kisheria na biashara haramu ya usafirishaji binadamu, kuendesha kesi, kupepeleza na kutoa misaada ya utambuzi na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

No comments:

Post a Comment