Na Richard Mwaikenda, CCM Blog, Dodoma.
Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dodoma imeuagiza uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuweka kamera za usalama katika Jiji la Dodoma.
Agizo hilo limetolewa wakati wa kikao cha Baraza hilo kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Desemba 16, 2020 jijini Dodoma.
Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ambaye alikumbushia agizo la awali la Bodi hiyo kuhusu umuhimu wa kuweka kamera katika mitaa mbalimbali za Jiji zitakazosaidia masuala ya usalama.
Amesema Jiji la Dodoma ambalo ni Makao Makuu ya Nchi linatakiwa liwe na kamera hizo kama zilivyowekwa Unguja Zanzibar na Moshi Kilimanjaro kwa upande wa Tanzania lakini vile vile liwe sawa na hadhi ya majiji ulimwengu.
Amesema kamera hizo zimesaidia sana kupunguza uhalifu kwa upande wa Zanzibar ambako kabla ya kuwekwa, vitendo vya uhalifu vilikithiri kwa watalii na wananchi kukabwa. Lakini pia Bodi iliagiza Tanroads na Tarura kuweka taa katika maeneo yote hatarishi.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Kondoa, Dk. Ashatu Kijaji aliiomba Tanroads na Tarura kuweka taa za usalama katika baadhi ya maeneo ya Mji wa Kondoa yanayohatarisha usalama wa wananchi kwa kukabwa na vibaka na kung’atwa na wadudu wenye sumu hasa wakati wa usiku wa giza.
Akitoa agizo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, alisema Tanroads na Tarura zinatakiwa kuweka jambo hilo la uwekaji kamera za usalama na taa katika mpango wa bajeti ijayo ili utekelezaji ufanyike.
Naye, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai aliitaka Tanroads, kupanua barabara kwa kuweka maeneo ya maegesho ya magari makubwa na madogo katika eneo la Kibaigwa, Kongwa ili kuinua biashara na kusaidia ajira kuongezeka katika eneo hilo lenye shughuli nyingi.
Aidha, Ndugai aliitaka Bodi kuiagiza Tanroads na Tarura kuweka lami katika Mji wa Kibaigwa ambao kwa hivi sasa umepanda hadhi ya kuwa Mji Mdogo, hivyo unastahili kupata haki hiyo na anashangaa ni nani anayechelewesha.
No comments:
Post a Comment