Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Jerry Silaa amefanya ziara katika Hospital ya Mama na Mtoto iliyopo Nguvu Kazi Chanika ambapo pia amepokea kero mbalimbali.
Katika ziara yake hiyo Jerry Silaa ameweza kutembelea vitengo vyote vya Hospital na kupokea Changamoto mbali mbali ikiwemo eneo ambalo linatakiwa kujengwa chumba cha kuhifadhia maiti, kujengwa General Wodi pamoja na mahitaji ya kuzungushiwa ukuta hospitali hapo.
Akiwa katika ziara hiyo, Jerry Silaa ameweza pia kumpa pole mmoja wa akina mama ambaye alieleza changamoto zake za uzazi kutokana na kufuata huduma mbali.
"Hospitali hii kwa sasa imekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Jimbo la Ukonga na maeneo ya nje ya Ukonga.
Pole sana Mama Samia.... kwa changamoto ulizokutana nazo awali na kwa sasa Serikali yetu chini ya Chama Cha Mapinduzi CCM na Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kero zote zimeendelea kutatuliwa." Alisema Jerry Silaa.
Akimuelezea mama huyo aitwae Samia ambaye alijifungua mtoto wa kiume na bado hajapewa jina,
"Mama Samia anaishi Yongwe Chanika huyu ni mtoto wake wa tatu.
Wa kwanza alijifungulia umbali wa Kilometa 40 Hospitali ya Amana (Bahati Mbaya), Wa pili alijifungulia tena Amana yupo hai.
"Mama Samia alijiwekea nadhiri hatazaa tena...Hospitali hii ilipojengwa amebadilisha mawazo. Mama Samia ni mmoja kati ya kina mama 25-30 wanajifungua hapa toka Kata ya Chanika na Kata za jrani, Kisarawe na Mkuranga wanaojifungulia hapa" Alieleza Jerry Silaa.
Mbunge huyo ambaye anahistoria kubwa na Hospitali hiyo kwa kuiomba kwa serikali ya Korea, Kuandika upembuzi yakinifu wake , kupata msaada na hadi kusaini mkataba wa ujenzi kwa niaba ya Serikali ya Tanzania alisema wazo na ombi lake huko nyuma leo limekuwa msaada mkubwa kwa Mama Samia na akina mama wengine wanaofika kupata huduma Hospitalini hapo.
"Ningeweza kunywa soda na Naibu Spika wa Korea, kumshukuru kwa Hospitali ya Mnazi mmoja, tukacheka na angeondoka.
Niliamua kuukana unazi na kumweleza wazi waliojenga Hospitali Mnazi mmoja walikosea.
Leo Mama Samia na wengine wengi wanapata huduma hapa" Alieleza Jerry Silaa.
No comments:
Post a Comment