Zaidi ya Vijana 36 waliohitimu elimu ya Kilimo katika Chuo Kikuu cha Sokoine wanaondoka hii leo kuelekea Nchini Israel baada ya kupata fursa ya mafunzo ya Kilimo yaliyoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati akiwakabidhi vijana hao tiketi za ndege pamoja na hati za kusafiria Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bw. Alex Mfungo amewataka Vijana hao kuzingatia mafunzo watakayoyapata wawapo nchini Israel kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kufanikisha jitihada za Serikali za kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo ambacho kinategemewa na Watanzania wengi na kukifanya kilimo kuwa biashara na ajira
Bwana Mfungo pia amewaasa Vjana hao 36 wa Kitanzania wanaokwenda Israel kwa mafunzo ya Kilimo kuzingatia sheria na taratibu za nchi hiyo na kuepuka kuvunja sheria pamoja na kuzingatia jukumu kubwa la kuwa mabalozi wazuri kwa Tanzania jabo litakalowezesha kupata fursa zaidi kwa wanafunzi wa Kitanzania.
Mratibu wa safari hiyo ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bwana Leonce Bilauri amesema maagizo ya Ilani ya Chama cha mapinduzi kwa mwaka 2020 hadi 2025 imeielekeza Serikali kuboresha na kuongeza fursa za kilimo ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ambapo kwa kuzingatia hilo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeanza utekelezaji huo kwa kuwatafutia wanafunzi hao nafasi ya kujifunza nchini Isarel
Mmoja wa vijana waliopata fursa ya kwenda nchini Israel Bwana William Msemo ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutekeleza kwa vitendo fursa za kutoa elimu ya kilimo bora kwa vijana jambo litakalowafanya kupunguza tatizo kwa ajira kwa vijana na kuahidi kuisambaza elimu hiyo kwa vijana wengine pindi watakaporejea
No comments:
Post a Comment