Baadhi ya wahitimu wa Cheti cha Awali cha Uhasibu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wa Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma wakisubiri kutunukiwa vyeti vyao kwenye mahafali ya 18 ya Taasisi hiyo yaliyofanyika mkoani Singida juzi.
Brass Band ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ikiongoza maandamano ya wahitimu hao kabla ya kuanza kwa mahafali hayo.
Viongozi mbalimbali kuroka Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma wakiwa wamejipanga mbele ya Jukwaa kuu wakati wa kumpokea mgeni rasmi wa mahafali hayo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga.
Na Dotto Mwaibale, Singida
Wahitimu wapatao 2485 kutoka Taasisi ya Uhasibu nchini, Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma wametunukiwa vyeti vya fani mbalimbali, ikiwemo vile vya awali, astashahada, stashahada na shahada-katika fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Uongozi wa Rasilimali Watu na Usimamizi wa Biashara.
Katika sherehe hizo za mahafali ya 18 zilizofanyika kwenye viwanja vya Kampasi ya Taasisi hiyo mkoani hapa juzi, imeelezwa kwamba, kutokana na maboresho kadhaa ya miundombiu ya kielimu idadi ya wanaodahiliwa imeendelea kupanda mwaka hadi mwaka.
Akihutubia mahafali hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA nchini, Profesa Carolyne Nombo alisema mathalani, kwa mwaka 2019/20 wanachuo waliodahiliwa kwenye kozi mbalimbali kwa kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma pekee walikuwa 2,700.
“Hili ni ongezeko la asilimia 29.9 ukilinganisha na wanachuo 1,894 waliodahiliwa katika mwaka wa masomo 2018/19. Ongezeko hili ni matokeo ya ubora wa elimu inayotolewa, utaratibu mzuri wa serikali kupitia (TAMISEMI) na ongezeko la mikopo kwa wanafunzi wa kozi za shahada,” alisema Prof. Nombo.
Akifafanua zaidi, alisema ubora wa elimu inayotolewa na Taasisi hiyo unatokana na mitaala inayowajengea wanachuo wake umahiri (competency) na hivyo kumwezesha mhitimu kuajiriwa au kujiajiri pindi anapohitimu masomo yake.
Aidha, Nombo alisema binafsi anafarijika na utaratibu mzuri wa serikali kupitia (TAMISEMI) wa kuwapangia vyuo moja kwa moja wale wahitimu wa kidato cha nne waliofaulu na kukidhi vigezo.
“Mathalani, katika mwaka wa masomo 2020/21 jumla ya wanafunzi 2557 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamepangwa kujiunga na kozi mbalimbali za cheti cha awali,” alisema.
Imeelezwa kati ya idadi hiyo, wanafunzi 1200 wamepangwa katika kampasi ya Singida, na wengine 398 kampasi ya Mwanza huku idadi ya 957 ikipangwa Kigoma.
Pia Nombo alipongeza juhudi za serikali, kipekee Rais John Magufuli, kwa maono yake chanya kwenye sekta ya elimu, hususani kwa namna alivyotoa msukumo wa kipekee kwenye ongezeko la mikopo kwa wanafunzi wa kozi za shahada.
“Katika kuhakikisha tunaunga mkono jitihada za serikali katika kuleta ustawi mzuri wa elimu, kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma zimeweza kutembelea shule mbalimbali za sekondari kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kusoma, na kuwaeleza fursa za masomo zilizopo TIA,” alisema.
Awali, kupitia mahafali hayo, Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga, alisema serikali ipo tayari kutoa kila aina ya ushirikiano ndani ya TIA na wahitimu wake, kwa kuzingatia fani zinazotolewa zina umuhimu mkubwa kwa ujenzi wa uchumi wa Taifa.
“Endeleeni kutekeleza majukumu yenu kwa weledi na kubuni mbinu mpya, fani zinazotolewa TIA ni muhimu sana katika kuendesha uchumi wa taifa letu na kuhakikisha matumizi bora ya fedha za umma,” alisema Maganga.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu huyo kwa niaba ya Wizara ya Fedha, alipongeza mchango wa TIA katika kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo, wakulima, wafugaji, wavuvi na vikundi vya ushirika.
“Jitihada hizi ni za muhimu sana katika lengo la Taifa la kurasimisha shughuli za wajasiriamali wadogo, na pia ni maagizo ya Rais Magufuli katika shabaha iliyopo ya kuwawezesha kupatiwa huduma muhimu ikiwemo mikopo,” alisema.
Hata hivyo, Meneja wa Kampasi ya Singida, Abbas Sanga, alisema TIA imejipanga vizuri, na kwamba mpaka sasa inaendelea kuwa kitovu katika kuhakikisha tija ya mafunzo yake inajikita katika mantiki ya uhalisia wa ustawi wa maisha punde tu mwanafunzi anapohitimu.
“Lengo letu ni kuendelea kutoa wahitimu wenye stadi stahiki za kumudu kufanya kazi mbalimbali za kuajiriwa na kujiajiri, lakini shabaha ni kuendelea kuhuisha mitaala yetu ili iendane na mahitaji ya kitaifa na kimataifa,” alisema Sanga.
TIA ina jumla ya Kampasi 6 zilizopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Singida, Mtwara, Mwanza na Kigoma zikiwa na jumla ya wanachuo 18,717.
No comments:
Post a Comment