Matokeo chanyA+ online




Tuesday, March 9, 2021

ULEGA: USIKIVU WA TBC UNAENDELEA KUIMARIKA

 

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Abdallah Ulega amesema kwamba Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linaendelea kuimarisha usikivu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa studio za Televisheni ya TBC, Mikocheni Dar es Salaam.

 Ulega ameyasema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya jamii ilipopokea taarifa kuhusu mradi wa ujenzi wa studio hiyo pamoja na ujenzi wa Redio ya Jamii Makao Makuu Jijini Dodoma.

“Taarifa inayowasilishwa kwenu leo itawezesha kupatikana uelewa wa hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hii na mtakapoitembelea mtapata fursa ya kuona hali halisi ya utekelezaji” alisema Mhe.Ulega.

Akiwasilisha taarifa hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania  Dkt. Ayoub Ryoba ameeleza kuwa  katika bajeti ya miradi ya maendeleo ya takriban Shilingi milioni 900 iliyoidhinishwa, pamoja na shilingi bilioni 1 kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) zilitekeleza uboreshaji wa mfumo wa umeme na ufungaji wa “AVR na UPS,” ununuzi na ufungaji wa mitambo na vifaa vya redio pamoja na ukarabati wa jengo la studio.

“Baada ya uboreshaji kupitia fedha hizo manufaa mbalimbali yamepatikana ikiwemo kuaandaa na kurusha vipindi vya redio na televisheni kutokea Dodoma, matangazo ya televisheni ya kipindi cha ARIDHIO na Jambo Tanzania yamekuwa yakirushwa kutokea Dodoma” Alisema Dkt.Ryoba.

Dkt. Ryoba aliongeza kuwa, manufaa mengine yaliyotokana na mradi huo ni kurushwa mbashara vipindi vinavyohitaji ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kitaifa kutoka kwa viongozi wa Serikali muda wote inapohitajika kufanya hivyo pamoja na redio jamii kuhusika kurusha habari za kikanda hivyo kuleta uelewa kwa wananchi kuhusiana na kazi wanazofanya.

 

No comments:

Post a Comment