Matokeo chanyA+ online




Tuesday, March 9, 2021

MBUNGE CHALINZE ATEMBELEA WANANCHI WALIOPATA MAAFA YA KUBOMOKA KWA NYUMBA ZAO KITONGOJI CHA PINGO

                        Na. Andrew Chale, Chalinze

Mbunge wa  Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete amewatembelea  kuwafariji Wananchi wa Kitongoji cha Pingo  eneo la Mbiki katika Kata ya Pera  walioezuliwa na kuangushwa nyumba zao kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali, iliyotokea Machi Mosi mwaka huu.

Katika ziara hiyo 6 Machi, Ridhiwani Kikwete aliambatana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze,  Geoffrey Kamugisha na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ramadhani Possi pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wa Chama cha Mapinduzi (CCM)  na wa Kata na  Kijiji ambapo walitembea kujionea athari za mvua hiyo.

Wakiwa katika eneo hilo la Pingo Mbiki, waliweza kushuhudia nyumba na miti ya mikorosho na ile ya mazao ikiwa imeangushwa pamoja na nyumba zingine kuezuliwa mapaa.

Baada ya kushuhudia tukio hilo,  Mbunge Ridhiwani Kikwete alisema kuwa wamefika maeneo hayo  kuwafariji na kuona namna ya kuwasaidia kwa kushirikiana na Serikali.

"Baada ya viongozi wa Kijiji kutujulisha tukio hili, tukaona tuje maeneo haya kuja tuyaone.

Sisi kwa upande wetu kama Halmashauri tumeona yapo mambo ambayo tutaenda kushahuriana na Mkurugenzi na Mwenyekiti ilikuona ndani ya Halmashauri tunayabebaje." Alisema Mbunge na kuoongeza:

"Lakini pia yapo mambo ambayo tunasema yapo juu ya Halmashauri yale ambayo ya kupeleka ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, lakini pia ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Maafa ilikuona pia nao kwa Serikali kwa ukubwa wake wanatusaidiaje hii hali". Alisema Mbunge, Ridhiwani Kikwete.

Hata hivyo Mbunge alibainisha kuwa, ameona hali halisi na hivyo watakavyorejea Ofisini wataona namna ya kupanga ilikuwasaidia Wahanga hao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Geoffrey Kamugisha alibainisha kuwa, wamefika hapo ikiwemo kuwapa pole kwa tukio hilo.

"Tunaenda kukaa pamoja na Mbunge na Mwenyekiti kuona namna ya kutatua hali hii ya athari". alisema Mwenyekiti Kamugisha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ramadhani Possi alisema licha ya kuona hali halisi, yupo tayari kupokea maelekezo ya viongozi hao ikiwemo kufanyia kazi yale yote aliyoyaona katika tukio hilo na kuona jinsi watakavyochukua hatua za haraka.

Kwa upande wao baadhi ya wahanga wa tukio hilo walipongeza kwa kitendo cha Mbunge Ridhiwani Kikwete kufika eneo hilo ba kuwafariji huku wakimuombea baraka katika uongozi wake.

Bi. Mariam Salehe  ambaye ni mmoha wa Wahanga wa tukio hilo la kubomolewa nyumba yake, alimshukuru Mbunge kwa kuwatembelea ambapo wanaamini watapata msaada wa haraka.

Kwa upande wake, Muhidin Rashid alimshukuru Mbunge kwa kufika eneo hilo huku akimuombea dua kuendelea kuwatumikia wananchi usiku na mchana.

"Ujio wa Mbunge na viongozi wengine kutufariji sisi ni heshima kubwa hivyo tunawaombea wazidi kututumikia wananchi wao hasa sisi tuliopo huku vijijini.

Tunamuombea kwa Mungu Mbunge wetu katika uongozi wake". Alimalizia Muhidin Salehe.


Mnamo Machi Mosi mwaka huu mvua hiyo kubwa yenye upepo mkali iliweza kusababisha athari kwa nyumba zaidi ya 39  kuangushwa na zingine kuezuliwa paa zake huku nyumba za ibada mbili nazo zikikumbwa na athari hizo.

No comments:

Post a Comment