Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako amekipongeza Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kwa
kusimamia vizuri ukarabati wa majengo ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi
Msinga (FDC) kilichopo Wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro.
Waziri
Ndalichako ametoa pongezi hizo mara baada ya kukagua ukarabati wa
majengo katika Chuo hicho ambapo amesema ameridhishwa na ubora kazi
iliyofanyika na kuwataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwa kuwa Serikali
yao inawajali na imeboresha mazingira ya kujifunzia.
Amesema Chuo
cha Maendeleo ya Wananchi Msinga ni moja kati ya Vyuo 54 vilivyofanyiwa
ukarabati kupitia Mradi wa Mukuza Ujuzi na Stadi za Kazi unaosimamiwa
na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Akizungumzia masuala
ya nidhamu kwa wanafunzi, Waziri Ndalichako amewataka walimu pamoja na
kufundisha masomo ya darasani kuhakikisha mafunzo juu ya uraia na
uzalendo yanakuwa endelevu ili kuwa na vijana wenye nidhamu na
wazalendo wanaothamini tunu zilizoachwa na waasisi wa nchi hii.
“Hii
kazi nzuri ambayo tumeifanya hapa muienzi na vifaa ambavyo mmeomba
naahidi kuwa nitavifanyia kazi, itakuwa haina maana yoyote kama ninyi
mtakuwa hamna uzalendo kwa sababu vifaa vinaweza vikaja na mkaviaharibu
ni lazima vijana mlinde rasilimali za nchi yenu,”alisema Waziri
Ndalichako.
Amewapongeza wanafunzi wa fani ya uashi katika Chuo
hicho kwa kujenga jengo la mlinzi na kusistiza kuwa hayo ndio mafunzo
yanayotakiwa kwa kuwa vijana wanamaliza wakiwa na ujuzi.
“Mafunzo
na mitaala yetu ni mizuri lakini wakati mwingine vijana mnakuwa
hamzingatii na kufuatilia kwa ukaribu masomo, kwa hiyo walimu niwasii
kama ambavyo nimeona kazi nzuri mmeifanya muendelee kuwafundisha vijana
wetu na msisahau kuwajengea maadili mema kwa ajili ya taifa
letu,”amesisitiza Waziri Ndalichako
Waziri Ndalichako ameahidi
kufanyia kazi changamoto za baadhi ya vifaa vya kufundishia na
kujifunzia katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi ili wanafunzi waweze
kusoma vizuri.
Nae Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msinga
Miriam Msomvu amesema ukarabati uliofanyika umetumia zaidi ya Sh milioni
560 na kwamba umewezesha kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 130 mwaka
2019 kufikia wanafunzi 312 mwaka 2021.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msinga wameishukuru Serikali kwa kufanya ukarabati mkubwa katika Chuo chao na kumuaomba Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwaondolea changamoto ya upungufu wa baadhi ya vifaa vya kujifunzia.
Muonekano wa moja ya majengo ya Chuo cha Maendeleo wananchi Msinga kilichopo wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro baada ya ukarabati.Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya wananchi Msinga kilichopo wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani kilimanjaro mara baada ya kukagua ukarabati uliofanyika chuoni hapo .
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiangalia wanafunzi wa fani ya Uashi katika Chuo cha Maendeleo ya wananchi Msinga kilichopo wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani kilimanjaro wakijifunza kwa vitendo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiangalia moja ya barakoa iliyoshonwa na wanafunzi katika Chuo cha Maendeleo ya wananchi Msinga kilichopo wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani kilimanjaro
No comments:
Post a Comment