Rais
wa DICOTA Dkt Frank Minja,Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia
Masuala ya Afya; Mhe Dkt Festo Dugange,Naibu Katibu Mkuu Afya na Mbunge
wa Viti Maalumu (CCM) Kundi la Asasi za Kiraia (NGOs) Mh Neema Lugangira
wakifungua vipimo vya Oxijeni ili kujaribu ufanyaji kazi wake.
Baada ya kukabidhiwa wanaviangalia vipima Oxijeni hivyo
Mbunge
wa Viti Maalumu (CCM) Kundi la Asasi za Kiraia (NGOs) Mh Neema
Lugangira na Rais wa Baraza la Watanzania wanaoishi Marekani (DICOTA)
leo wamekabidhi msaada wa Vipima Oxijeni (Pluse Oximeters) 108 kwa Ofisi
ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya Vituo vya Afya kutoka Mikoa 11 ikiwa ni
mchango wao katika kuthamini juhudi za Serikali katika kuimarisha Afya
za Watanzania.
Msaada huo umepokelewa na Naibu Waziri wa
Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Masuala ya Afya; Mhe Dkt Festo
Dugange ambapo vifaa hivyo vitagawiwa katika mikoa ya Dar-es Salaam,
Dodoma, Kigoma, Kagera, Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Ruvuma, Mbeya, Lindi
na Njombe.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo wa
vifaa, Mbunge wa NGOs Tanzania Bara, Mhe Neema Lugangira alimshukuru
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe Ummy Mwalimu kwa ushirikiano
mkubwa aliowapatia katika kufanikisha shughuli hiyo ya leo.
Mbunge
Neema Lugangira alisema pia wanashukuru Dkt Grace Maghembe, Naibu
Katibu Mkuu na Dkt Ntuli Kapologwe, Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya
Afya, Lishe kwa ushirikiano wao mkubwa ambao wamekuwa wakiendelea
kuwapatia.
“Sisi tunamshukuru sana Waziri wa Nchi OR TAMISEMI
Mhe. Ummy Mwalimu, kuridhia kupokelewa kwa msaada huu, ambao
umepokelewa na Naibu Waziri, Dkt. Festo Dugange. Mimi kama Mbunge
nitaendeleza jitihada hizi kwa niaba ya Serikali ili lengo la kuimarisha
Afya ya Mtanzania iweze kutimia,” Alisema Lugangira.
Awali
akizungumza wakati akiipokea msaada huo wa vifaa tiba ambavyo vinatumika
kupima kiasi cha Oxijeni katika mwili wa mwanadamu, Naibu Waziri Ofisi
ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia afya, Mhe Dkt. Festo Dugange
amewapongeza Watanzania hao waishio Marekani kwa kuthamini juhudi za
Serikali ya Nchi yao za kujenga na kukarabati miundombinu mbalimbali ya
afya nchini.
Alisema ili kuhakikisha kuwa jukumu hilo
linatekelezwa kikamilifu, Naibu Waziri ameongeza kuwa katika bajeti ya
mwaka 2021/22 serikali imetenga shilingi bilioni 65 kwa ajili ya
kununulia dawa na vifaa tiba.
“Serikali imefanya kazi kubwa
ya ujenzi wa Miundombinu na katika mwaka wa fedha 2021/22 tumeweka
kwenye bajeti ya dawa na vifaa tiba kama hivi na vingine kiasi
kinachofikia Bil.65, hivyo kwa jitihada hizi za wadau hawa na wengine
wote watakao kuja hapo baadaye ni ishara kwamba lengo letu la kuweka
vitendanishi na dawa litatimia,” amesema Mhe Naibu Waziri Dkt. Dugange.
Akiongea
kwa niaba ya Watanzania waishio nchini Marekani, rais wa DICOTA, Dkt.
Frank Minja, amesema, wanaona fahari ya kuchangia vifaa hivyo ambavyo
vitakwenda kugawiwa kwenye ngazi ya Hospitali za Wilaya na kutumika na
watanzania wenzao na kuahidi ni mwanzo ambapo wanatarajia kufanya mengi
zaidi kwa kushirikiana na Serikali na Mbunge Lugangira katika Sekta hii
ya Afya.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI
anayeshughulikia Afya Dkt. Grace Magembe, amesema kuwa atahakikisha kuwa
vifaa vilivyopokelewa vinatunzwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu.
Hafla
ya kukabidhi vifaa tiba ilifanyika Makao Makuu ya Ofisi ya Rais
TAMISEMI jijini Dodoma na kuhudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Huduma za
Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli
Kapologwe na Katibu Mtendaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu Paulina
Mkwama.
No comments:
Post a Comment