Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akisisitiza jambo kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakati akikagua moja ya vifaa vya kisasa vya matengenezo ya magari ya Serikali vilivyopo katika Karakana ya Wakala huo jijini Dodoma.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Heriel Mteri, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara vipuri vya matengenezo ya magari katika Karakana ya Dodoma, wakati Naibu Waziri huyo alipoitembelea na kukagua shughuli mbalimbali katika Wakala huo jijini Dodoma.
Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akikagua moja ya vifaa vya
matengeneoz ya magari ya Serikali vilivyopo katika Karakana ya Wakala
huo jijini Dodoma.
Naibu
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akitoa maelekezo kwa Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Heriel Mteri,
wakati alipotembelea Wakala huo na kuzungumza na menejimenti ya Wakala
pamoja na kukagua karakana ya Wakala huo jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akizungumza na Menejimenti ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), katika kikao kazi na uongozi wa Wakala huo, mkoani Dodoma. Kulia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Heriel Mteri.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Heriel Mteri akiwasilisha taarifa ya Wakala kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, wakati alipotembelea Wakala huo, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mara baada ya kikao kazi na uongozi wa Wakala huo, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kuhakikisha wanayatoa magari yote yaliyotelekezwa na wamiliki wake katika karakana zote nchini na kusababisha mrundikano ndani ya karakana hizo.
Akizungumza na Menejimenti ya Wakala huo, jijini Dodoma, Waitara amesema kuwa hatua hiyo itapelekea kupunguza msongamano katika karakana hizo na hivyo kupatikana kwa nafasi ili kuruhusu magari mengine kupata huduma kiurahisi.
“Magari hapa ni mengi na mlundikano ni mkubwa, mengine yanaonekana ni ya muda mrefu, hakikisheni mnayatoa na kuyapeleka kwa wenyewe ili kupunguza msongamano hapa na hata katika karakana zenu nyingine nchi nzima”, amesema Waitara.
Aidha, Waitara ameutaka Wakala huo kuboresha huduma zao nchi nzima ikiwemo kutatua mianya yote inayopelekea uhujumu na kupelekea utendaji wa kusuasua kwa watumishi wa Wakala huo.
“Hakikisheni kuwa mnapunguza gharama, mnatumia muda mfupi na vipuri sahihi katika utengenezaji wenu wa magari, mkifanya hivi mtapunguza malalamiko kutoka kwa washitiri wenu”, amesisitiza Waitara.
Aidha, ameagiza Wakala huo kuhakikisha wanatafuta njia sahihi ya kuhifadhi mafuta machafu yanayomwagika wakati wa utengenezaji wa magari ili kuhifadhi mazingira katika maeneo yao ya kazi.
Kuhusu suala la vivuko, Waitara ameutaka Wakala huo kuhakikisha kila kivuko kinajisimamia na kujiendesha kwa faida na kutaka Wakala huo kupitia upya tozo za nauli za vivuko nchini katika baadhi ya maeneo bila kuumiza wananchi.
“Huduma za Serikali hazitakiwi kufanywa kwa kubahatisha, kwa mfano katika Kivuko cha Nyamisati utaratibu wa safari na nauli haueleweki, wananchi wa huko wanalalamika sana, kaeni mlirekebishe hili, Serikali haitaki watu wababaishaji”, amefafanua Naibu Waziri huyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Heriel Mteri, amesema kuwa Wakala unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikwemo wakala kuendesha baadhi ya vivuko vyenye mapato madogo na hivyo kushindwa kujiendesha vyenyewe na kupelekea Wakala kutoa ruzuku ya kuviendesha.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni uchakavu wa miundombinu na vifaa vya karakana ambapo amesema kuwa karakana hizo zimejengwa miaka mingi iliyopita hivyo kuhitaji ukarabati mkubwa.
Ameongeza kuwa, kwa sasa Wakala unatumia mfumo wa kisasa wa kubaini vipuri ambavyo sio halisi katika karakana zake zote ili kudhibiti udanganyifu ambao unafanywa na baadhi ya wafanyabiashara.
Naibu Waziri Waitara, amefanya ziara TEMESA jijini Dodoma, ili kujionea utendaji wa wakala huo na kuzungumza na Menejimenti kuhusu namna ya kuboresha huduma katika Wakala huo.
No comments:
Post a Comment