Na Teresia Mhagama, Dar es Salaam
Waziri
wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Viwango Tanzania
(TBS) kuhakikisha kuwa uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta kama vile
petroli na dizeli unafanyika kuanzia kwenye matenki yanayohifadhi mafuta
hayo badala ya magari ili kuhakikisha kuwa mafuta yote yanayosambazwa
nchini yanakuwa na ubora na Serikali inapata kodi stahiki.
Dkt.Kalemani
alitoa agizo hilo tarehe 28 Aprili, 2021 mara baada ya kufanya ziara
kwenye maghala ya mafuta ya kampuni za Camel Oil na Oil Com, Kurasini
mkoani Dar es Salaam na kukuta wataalam kutoka TBS wakifanya kazi ya
uwekaji wa vinasaba kwenye magari ya kusafirisha mafuta ya kampuni
tajwa.
“Nataka muanze kupima mafuta kuanzia kwenye matenki
yenyewe, hadi kwenye vituo, siyo tu kusubiri pale wanapopakia kwenye
magari, Je ikitokea wamepakia wakati hampo, mtajuaje kuwa mafuta husika
yana ubora?”Alisema Dkt.Kalemani
Dkt.Kalemani alieleza kuwa,
amefanya ukaguzi wa kazi ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta ili
kujiridhisha kama TBS wanafanya kazi husika kwa ufanisi baada ya
kukabidhiwa kutekeleza jukumu hilo ambalo awali lilikuwa likifanywa na
mkandarasi binafsi ambaye alikuwa akilipwa takriban shilingi Bilioni
Tano kwa mwezi.
Aliongeza kuwa, Serikali imekuwa ikipoteza fedha
nyingi kumlipa mkandarasi binafsi kuweka vinasaba kwenye mafuta badala
ya TBS ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha kuwa mafuta yanayouzwa
nchini yanakuwa na ubora stahiki.
“Lengo la Serikali ni
kuhakikisha kuwa, mafuta yanakuwa na ubora, kodi zinapatikana na pia
tunajenga uwezo wa watu wetu kufanya kazi husika na Taasisi zetu
zisimamie kazi hii badala ya kutegemea watu kutoka nje ya nchi.”
Alisisitiza Dkt.Kalemani
Katika ukaguzi huo, Dkt.Kalemani
aliiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),
kuhakikisha kuwa, wanasimamia kikamilifu kazi ya uwekaji wa vinasaba
kwenye mafuta nchini kwani TBS ina jukumu la kupima mafuta hayo na EWURA
ndiye mwenye jukumu la kumsimamia mpimaji.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya alimhakikishia Waziri wa
Nishati kuwa, TBS ina uwezo wa kufanya kazi ya uwekaji vinasaba kwenye
magari na kwamba mafuta yote yanayosambazwa nchini yanakuwa na vinasaba.
Katika ziara yake kwenye maghala hayo ya mafuta mkoani Dar es
Salaam, Waziri wa Nishati aliambatana na Kaimu Kamishna wa Petroli na
Gesi, Sebastian Shana, na Wakuu wa Taasisi za Wakala wa Uagizaji Mafuta
kwa Pamoja (PBPA), TBS na EWURA.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (wa Pili kushoto) akikagua kazi ya uwekaji vinasaba kwenye ghala la mafuta la kampuni ya Camel Oil mkoani Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (wa Tatu kushoto) akiwa katika ghala la mafuta la kampuni ya Camel Oil wakati alipofika kukagua kazi ya uwekaji vinasaba kwenye ghala hilo mkoani Dar es Salaam. Wa Pili kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya.
No comments:
Post a Comment