Waziri wa
Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, ameitaka Kampuni
ya kikandarasi ya SinoHydro Corporation kutoka China kuhakikisha kuwa
wanakamilisha kazi ya ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa kwa muda
uliopangwa ili kuruhusu ndege kubwa kuweza kutua katika kiwanja hicho.
“Kama
mnavyoona, sasa hivi huduma ya ndege ya ATC imesimama kwa sababu ya
ukarabati huu, hakikisha Mkandarasi unatekeleza kazi hii kwa haraka kama
mkataba unavyosema, wananchi wa hapa wanasubiria kwa hamu Kiwanja
hiki”, amesema Chamuriho.
Aidha, amemtaka Meneja wa Wakala wa
Barabara (TANROADS), Mkoa wa Iringa, Mhandisi, Kindole Daniel, kukaa na
Mkandarasi huyo kuona namna ya kuunganisha awamu mbili za ukarabati kama
zilivyoainishwa na Mkandarasi ili kukamilisha mapema kazi hiyo.
Amesisitiza
kwa Meneja huyo kuhakikisha kuwa, wananchi wa maeneo jirani ya mradi
huo wanapata ajira ili waweze kunufaika na mradi huo, pia kuweka
matangazo kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhusu ajira za kitaalamu ambazo
zinatolewa na Mkandarasi huyo ili wataalamu wazawa nao kuweza kuomba
nafasi hizo.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS), Mkoa wa Iringa, Mhandisi, Kindole Daniel, amesema kuwa mradi
wa ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa unahusisha matengenezo
makubwa ya njia ya kuruka na kutua ndege ya sasa yenye kiwango cha lami
nyepesi, ujenzi wa eneo la usalama, njia ya michepuo ya ndege, maegesho
mapya ya ndege, jengo la muda la abiria na mnara wa muda wa kuongozea
ndege.
Ameongeza kuwa, mradi huu pia unahusisha ujenzi wa jengo
la zimamoto, ujenzi wa jengo la kituo cha nishati na kuweka taa za
ardhini kwenye njia ya kuruka na kutua ndege.
Naye, Mkuu wa
Wilaya ya Iringa ameomba ujenzi huo ufanyike kwa awamu moja ili uishe
haraka kwani wananchi wa Mkoa huo wanapata tabu kwa sasa kutokana na
Kiwanja hicho kupokea ndege ndogo pekee.
Mradi wa Ukarabati wa
Kiwanja cha ndege cha Iringa, ulisainiwa mwezi Mei mwaka jana, ambapo
Ukarabati wake unahusisha kazi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa njia ya
kuruka na kutua ndege kutoka urefu wa kilometa 1.6 hadi kufikia kilometa
2.1 na hivyo kupelekea hata ndege za masafa ya kati kuweza kutua kwa
urahisi pindi ukarabati huo utakapokamilika.
Kazi ya Ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa ikiendelea. Ukarabati huu unahusisha matengenezo makubwa ya njia ya kuruka na kutua ndege ya sasa yenye kiwango cha lami nyepesi, ujenzi wa eneo la usalama, njia ya michepuo ya ndege, maegesho mapya ya ndege, jengo la muda la abiria na mnara wa muda wa kuongozea ndege.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, akitoa maelekezo kwa wakandarasi wa Kampuni ya SinoHydro Corporation Limited kutoka China wakati Waziri huyo alipotembelea mradi wa Ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa kujionea maendeleo yake.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Iringa, Kindole Daniel akielezea jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho (WaTatu kushoto mbele) wakati Waziri huyo alipotembelea mradi wa Ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa kujionea maendeleo yake.
Msimamizi wa mradi wa Ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Iringa, kutoka Kampuni ya SinoHydro Corporation Limited ya China, Yuan Rui, akionesha mchoro wa picha ya mradi huo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho (WaPili kushoto) wakati Waziri huyo alipotembelea mradi huo kujionea maendeleo yake.PICHA NA WUU
No comments:
Post a Comment