Na Grace Semfuko, MAELEZO
Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul
amewataka Wasanii Nchini kuacha kutangaza mitandaoni mambo yao binafsi
na badala yake watangaze kazi zao ili kuleta tija ya maendeleo yao
kiuchumi.
Pia amewataka Wazazi wa Wasanii kulinda hadhi za Watoto
wao kwa kutowahusisha kwenye migogoro yao ya mahusiano pindi Baba na
Mama wanaporafakakana kwani wanawaingiza kwenye historia isiyofaa katika
maadili ya Kitanzania.
Ameyasema hayo katika ziara yake kwenye
Ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa-BASATA na kulitaka Baraza hilo kuwa na
kanuni imara za kuimarisha maadili na mienendo ya wasanii Nchini.
“Kama
kuna kitu Watanzania haturidhishwi nacho ni kitendo cha msanii kuelezea
maisha yake binafsi, kwamba nimezaa na huyu, nina Wanawake kadhaa, hii
inadidimiza utamaduni wetu, mnatuharibia kizazi hiki ambacho kinakua
kuona kwamba ni fasheni kueleza mahusiano kwenye mitandao, mahusiano ni
ya mtu binafsi, na je Wasanii wetu ni lazima wafanye mwingiliano? Kwamba
mimi ni msanii lazima nitembee na wewe, na wewe na wewe!” amehoji
Gekul.
Aidha amesema ni muhimu sheria na kanuni za maadili ya
Wasanii zikaongezewa nguvu ili kuhakikisha wanaondokana na vitendo hivyo
ambavyo amevitaja kuwa vinashusha hadhi ya Wasanii nchini.
“Hivi
hakuna sheria inayowabana, si ipo? Au adhabu na fine zimekuwa ndigo
sana? Tunasimamia kwa kiasi gani hizo kanuni? Hili jambo lazima liwe
makini sana, wengi hawafurahishwi, tunatamani tuwafahamu Wasanii kwa
mambo mazuri ya kujenga jamii zetu, lakini sio kwa mambo yake binafsi,
kila mtanzania akiweka mambo yake binafsi hiyo mitandao ingekwama tu,
yaani maisha yako binafsi ni sehemu ya sisi kufahamu? Ili tukupe kiki?”
amesema Gekul.
Kuhusu Wazazi wa Wasanii kuingiza Vijana wao
kwenye migogoro ya mahusiano ya kifamilia, Gekul amesema ni muhimu Mzazi
kulinda hadhi na maslahi ya mtoto wako kwa kumuondolea historia
isiyofaa kwa jamii inayomzunguka na kwamba ni muhimu kuzingatia maadili
ya kitanzania.
“Mama unaanza kusema mtoto wangu baba yake sio
huyu ni yule! unamjengea mazingira gani huyu Mtoto? Hebu tuongeeni kama
watanzania, miongoni mwetu tumezaliwa kwenye mazingira ya kitanzania,
wengine huenda tumezaliwa kwenye mazingira ya Baba na Mama wametulea
lakini huyo Baba sio wako na hujawahi kujua kama sio Baba yako mzazi,
Wazazi wetu walivyotukuza, walivyotulea sicho tunachokiona kwa sasa,
yaani mtoto anakuwa mjadala wa siku kwenye mitandao? Kwa nini? Mtoto ni
zawadi kutoka kwa Mungu, ni Malaika, lakini sasa unamleta kwenye
mitandao tunamjadili, ili iweje?” alihoji Gekul.
No comments:
Post a Comment