Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida Issa Nassoro, akiongoza dua katika arobaini ya Marehemu Maalim Selemani Kingu.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Iramba, Ali Katembo, akizungumza katika mkutano huo.
Mwanafunzi, Ali Mohamed akisoma Qulaan katika mkutano huo.
Mzee Juma Kengele, akizungumza katika mkutano huo.
Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida Issa Nassoro, akiingia Msikiti wa Kata ya Shelui kuzungumza na Waislamu.
Na Dotto Mwaibale, Singida
Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida Issa Nassoro amewaomba Waislamu mkoani hapa kuinusuru nyumba yao iliyopo mjini hapa isipigwe mnada.
Sheikh Nassoro alitoa ombi hilo juzi wakati akizungumza na Waislamu wa Shelui katika ziara yake ya kikazi ya siku moja.
"Waislamu wenzangu nina ujumbe muhimu kwenu ambao nitawaachia Sheikh na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wilaya ambao watausambaza hadi kwenye kata nao si mwingine tuna nyumba ya Bakwata ipo pale mjini karibu na Msikiti wa Kati ni Block H No 13 inapigwa mnada.Kabla sijawa Kaimu Sheikh wa mkoa nilimfuata Mufti Sheikh Abubakar Zubery kumuomba kumuambia kwanini nyumba hiyo hiuzwe hivyo nilimuomba anipe jukumu la kusimamia suala hilo kwa maana ya kuepuka isipigwe mnada ndio maana nimekuja kwenu ili tuinusuru kwani zinahitajika Sh.Milioni 70 ambazo si pesa nyingi kwa watu wengi kwani tukifanya kila mmoja atoa Sh.10,000 kwa wilaya zote saba za Singida tutapata Sh.Milioni 47 na hizo zitakazo salia tutatafuta njia nyingine ya kuzipata ili tuigomboe nyumba hiyo tukijipanga vizuri naamini hatutakosa fedha hizo" alisema Nassoro.
Katika hatua nyingine Sheikh Nassoro aliwataka Waislamu wa Mkoa wa Singida kuacha kugombana na kueleza kuwa kata, wilaya, mkoa na Taifa lenye magomvi haliwezi kupata maendeleo na ili maendeleo yapatikane kuanzia ngazi ya familia, jamii hadi katika nyumba za ibada nikuacha magomvi.
Aidha Sheikh Nassoro akizungumza na Waislamu hao alisema mbele yao wana majukumu mengi makubwa na moja ya jukumu alilonalo ni kuboresha taaluma ya dini hasa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari.
Alisema licha ya Serikali kuweka vipindi vya dini katika shule hizo kwa ajili ya kuwaelimisha vijana wa kiislamu kumekuwepo kusuasua na kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Bakwata wenye jukumu la kusimamia vipindi hivyo ni baraza la masheikh wa kata waliopo kwenye maeneo zilipo shule hizo.
" Jambo ninalolisisitiza ni masheikh wa kata wajitahidi kutoa walimu katika kata zao ili vijana wa kiislamu waweze kupata taaluma za dini." alisema Nassoro.
Akizungumza katika mkutano huo Mzee Ismail Mang'oma alisema kazi kubwa ya kwanza ambayo Sheikh Nassoro anatakiwa kuifanya ni kuwaunganisha Waislamu wa Mkoa wa Singida na kuwa wamoja baada ya kupalaganyika kwa kila mtu kuwa kivyake.
Alitaja kazi ya pili ambayo anatakiwa kuifanya ni kuwainua waislamu kiuchumi.
Katika ziara hiyo Sheikh Nassoro alipata fursa ya kuzuru kaburi la Sheikh Yusuf Iddi Katalama ambaye alikuwa ni mmoja wa waanzilishi wa dini ya Kiislamu Bonde la Iramba pamoja na kuongoza dua katika arobaini ya Marehemu Maalim Selemani Kingu.
No comments:
Post a Comment