Saturday, August 21, 2021
Wananchi wa Puma wakishuhudia ukaguzi wa mradi huo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Denis Nyiraha akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa vyoo vya Zahanati ya Puma. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ikungi, Mika Likapakapa na kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Mkoa wa Singida, Yohana Msita, akichangia jambo kwenye ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa vyoo vya Zahanati ya Puma. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa Singida, Dkt.Binilith Mahenge.
Ukaguzi wa madarasa Shule ya Sekondari Ikungi ukiendelea.
Na Dotto Mwaibale, Singida
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida imekagua miradi ya maendeleo wilayani Ikungi na kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo hususani eneo la maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika chini ya Serikali ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya afya.
Pia kupitia ukaguzi wa utekelezaji wa miradi hiyo CCM kwa namna ya kipekee imeguswa na mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kata ya Issuna iliyopo Wilaya ya Ikungi ambao unakwenda kutatua changamoto za wananchi wa eneo hilo za kusafiri umbali mrefu kwenda kata zingine kufuata huduma za afya.
Akizungumza jana wakati wa ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa maagizo ya ilani ya CCM, Mwenyekiti wa kamati hiyo Alhaji Juma Kilimba alihimiza sekta hiyo na nyingine kuhakikisha inakamilisha miradi yote kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.
"Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo nchini kote hivyo nawaomba wasimamizi wa ujenzi wa miradi hii kuwa wazalendo katika matumizi ya fedha hizo,". alisema Kilimba.
Katika hilo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Gutete Mahava akitoa taarifa ya ujenzi wa Zahanati hiyo alisema mradi huo ulibuniwa mwaka 2014 na upo Kijiji cha Issuna 'A'
Alisema zahanati hiyo ikikamilika itatoa huduma kwa wananchi wa vijiji vitano vya Issuna 'A, Issuna 'B', Ng'ongosoro, Nkuhi na Tumaini na kuwa ujenzi wake upo katika hatua za mwisho kukamilika.
Mahava alisema kuwa walipokea Sh.50 Milioni kutoka Serikali kuu na ununuzi wa vifaa vyote umefanyika na tayari Wizara ya Fedha imetenga Sh.8 Milioni kwa ajili ya dawa na vitendanishi.
Hata hivyo kamati hiyo imeomba hatua za haraka zichukuliwe ili kuharakisha ujenzi wa Hospitali ya wilaya hiyo ambao bado mradi wake unasuasua kutokana na changamoto za kifedha -kutokana na umuhimu wake mkubwa kwa idadi kubwa ya watu wanaozunguka wilaya hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza baada ya kukamilika kwa ziara hiyo aliwashukuru wakurugenzi na wakuu wote wa wilaya zote kwa kusimamia miradi hiyo.
"Niwashukuru wakurugenzi wote na wakuu wa wilaya kwa umoja wenu na kusimamia miradi hii ambayo inatumia fedha nyingi kutoka Serikalini,". alisema Mahenge.
Akizungumzia mradi wa maji wa Kipumbuiko Dkt. Mahenge aliwata wahusika kutoangalia faida zaidi badala yake wazingatie utoaji wa huduma kwa wananchi na kuutunza.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro aliishukuru kamati hiyo na akatumia nafasi hiyo kuelezea mikakati ya maendeleo ya wilaya hiyo hususani katika sekta ya kilimo hasa cha zao alizeti na mpunga ambao unalimwa kwa wingi maeneo ya Iyumbu.
Alitaja eneo lingine watakalo liangalia ili kupata mapato ni kwenye madini, ufugaji wa nyuki na miradi mingine.
Kamati hiyo katika wilaya hiyo ilikagua mradi wa ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja Shule ya Sekondari Ikungi, ujenzi wa madarasa mawili Shule ya Msingi Ikungi, ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali ya wilaya hiyo, ujenzi wa mradi wa maji Kipumbuiko, ujenzi wa matundu saba ya vyoo Zahanati ya Puma, ufugaji wa nyuki (Kikundi cha Save The Bee Issuna, ukamilishaji wa ujenzi wa Zahanati ya Kata ya Issuna, ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha VETA na ukamilishaji wa ujenzi wa maabara Shule ya Sekondari Ikungi.
Friday, August 20, 2021
VYAMA VYA SIASA 11 VYATOA MSIMAMO KATIBA MPYA, VYAUNGANA NA RAIS SAMIA
Na Said Mwishehe
Viongozi
wa Umoja wa Vyama vya Siasa ambavyo havina wawakilishi Bungeni wamesema
wataendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu kuhusu kuwataka wananchi
kuwa na subira katika mchakato wa Katiba Mpya.
Umoja huo umesema
wao msimamo wao katika mchakato wa Katiba mpya mbali ya kumuunga mkono
wanappendekeza mchakato uanzie ulipoishia awali kwa wananchi kupiga kura
ya maoni kwani mapendekezo ya Katiba mpya yalishafanyika ,hivyo hawaoni
sababu ya kuanza upya kwani ni matumizi mabaya ya fedha za umma.
Mwenyekiti
wa Umoja huo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha DP Abdul Mluya
amesema msimamo wao wanaunga mkono kauli ya Rais lakini hawaoni sababu
mchakato wa Katiba Mpya kuanza upya na badala yake uanzie ulipoishia.
"Kuna
uwezekano wa kuendeleza pale walipoishia katika mchakato wa katiba mpya
kuliko kuanza upya uandishi wa katiba kwa maana utaweza kupoteza
gharama kubwa fedha ambazo zingeweza kuendeleza miradi mingine nchini.
“kwenye
mchakato wa katiba tuliishia kwenye kura ya maoni (katiba pendekezwa)
kwahiyo msimamo wetu tunasema kwamba kutokana na Dunia kuingia kwenye
wimbi la ugonjwa wa korona uliopelekea kuyumba kwa uchumi hatuoni tija
na afya kwa watanzania kama tutakwenda kuwaingiza kwenye suala uandishi
wa katiba mpya kama ile iliyotumia zaidi ya bilioni 200.
"Kuna
haja ya msingi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutuleta kura
ya maoni tupige kura ili kupata katiba ambayo imeshatumia fedha za
wananchi kuliko kuanza uppya mchakato wa kuandika katiba mpya.Haya sisi
ndio maoni yetu na yaheshimiwe kama nasi tunavyoheshimu mawazo ya
wengine,"amesema.
Aidha amesema wanamuunga mkono Rais Samia
katika chanjo ya COVID-19 ambayo ni hiyari sio lazima,lakini vyama hivyo
vinawahamasisha wananchi kupata chanjo hiyo kwa lengo la kukabiliana na
janga la ugonjwa huo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha
ADC, Bw.Doyo Almas amewataka viongozi na wananchi kwa ujumla kuacha
tabia ya kuikosoa chanjo ya kujikinga na Uviko -19 kwani chanjo hiyo
inatolewa kwa hiari na haina madhara yoyote.
Doyo amesema Rais
kwa busara zake ameruhusu kutoa mwanya kwa Watanzania wanaotaka na
wasiotaka lakini yeye alikuwa ni miongoni mwa waliotaka na wakachanja na
sisi viongozi tumemuunga mkono Rais katika chanjo ya Uviko kwasababu
suala la afya linamuhusu mtu mmoja mmoja lakini kama taifa ukipoteza
nguvu kazi ya taifa lazima upoteze harakati za kukuza uchumi.
Kuhusu
Katiba mpya, Doyo amesisiti vyama hivyo 11 wanataka mchakato wa Katiba
uanze ulipoishia ili kuokoa fedha, maana wanaodai Katiba sasa wengine
walikuwepo wakati wa mchakato wa awali wa Katiba inayopendekezwa
ambayo ipo.
"Nchi imeingia gharama kubwa katika mchakato
umekwenda na umefikia hapo.Kama wananchi wanataka Katiba basi twendeni
tukaanzie hapo.Sisi vyama 12 tunaomba serikali sikivu ombi letu
tuendelee na mchakato ambao awali ulikuwa umeishia,"amesema Doyo.
Wednesday, August 18, 2021
CCM SINGIDA YAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO WILAYANI MKALAMA
Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Mkoa wa Singida Yohana Msita akizungumza kwenye ukaguzi huo.
Na Dotto Mwaibale, Mkalama.
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida imefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na kukagua utekelezaji wa Ilani kwenye miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Alhaji Juma Kilimba akiwa ameambatana na wajumbe wake aliipongeza Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa utekelezaji wa miradi.
Miongoni mwa miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba sita za wakuu wa idara, ujenzi wa uzio kuzunguka ofisi za Halmashauri urefu wa mita 750, ujenzi wa madarasa mawili na vyoo ,matundu 12 Shule ya Sekondari Gumanga, ukamilishaji wa vyumba viwili vya maabara Sekondari ya Mpambala, mradi wa maji Kijiji cha Nkungi.
Mradi mingine iliyotembelewa na kamati hiyo ni upanuzi wa wodi ya watoto kwa gharama ya Sh.180 milioni, wodi ya wanawake 160 milioni na wodi ya wanaume 160 milioni katika Hospitali ya Wilaya.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisikitishwa na ukarabati wa vyumba vya maabara katika Shule ya Sekondari Chemchemi ambavyo vimejengwa chini ya kiwango ukilinganisha na vile vilivyokarabatiwa kwa Sh.25 milioni katika Shule ya Sekondari ya Gumanga licha ya kutolewa Sh.35 milioni kwa kila shule kwa ajili ya ukarabati huo.
Alisema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo hivyo kuna kila sababu ya kuzitumia vizuri kwa manufaa ya wananchi.
Katika ziara hiyo viongozi mbalimbali walikuwepo wakiwemo wakuu wa idara wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo ya Mkalama Sophia Kizigo.
Leo kamati hiyo itafanya ziara ya namna hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida
UPANUZI WA HOSPITALI TEULE YA MAKIUNGU MKOANI SINGIDA KUGHARIMU SH.10 BILIONI
Na Dotto Mwaibale, Singida
Upanuzi wa Miundombinu ya Hospitali Teule ya Makiungu ambayo ni msaada mkubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida kwa ujumla mkoani hapa ambao unaendelea unatarajia kugharimu zaidi ya Sh.10. Bilioni.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Stephen Samanii, wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge wakati wa ziara yake ya kukagua hospitali hiyo iliyoanzishwa Novemba 6,1954, na Askofu Patrick Winters, Mmisionari Mpalotini.
Alitaja baadhi ya majengo yanayotarajiwa kujengwa kuwa ni pamoja na jengo la hudumu za nje (OPD),wodi nane zenye uwezo wa kuwa na vitanda 350, jengo kubwa la upasuaji lenye vyumba sita vya upasuaji kwa wakati mmoja, ukumbi wa mikutano na ofisi za utawala.
Alisema ujenzi huo unatarajiwa kufanyika kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.
Katika taarifa yake hiyo Dk.Samanii aliiomba Serikali kuisaidia hospitali hiyo msaada wa dharura wa ‘oxygen concentrator’ 10 zisizopungua zenye uwezo wa kuhudumia watu wawili kila moja kwa wakati mmoja.
Pia ameomba msaada wa mitungi ya gesi 20, kwa maelezo kwamba wagonjwa wenye changamoto za kupumua wanaongezeka kila siku hivyo bila ya kupata mitungi hiyo watashindwa kuwahudumia wagonjwa.
“Tunaomba ofisi yako kupitia kwa mganga mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya ya Ikungi, mtusaidie upatikanaji wa vifaa hivyo ambavyo vitasaidia kunusuru maisha ya wananchi”. alisema.
Aidha,ameomba wapatiwe misamaha ya kodi na kuondolewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), na ushuru wa forodha katika vifaa vya ujenzi, mashine na vifaa tiba.
“Pia vifaa vya usafi (sanitary equipment) vikiwemo vyoo vya kukalia na masinki yake,beseni za pekee,vifaa vya bafuni. na marumaru za square metres 23,000 kwa ajili ya ujenzi unaoendelea. Huo utakuwa mchango mkubwa sana wa serikali yetu katika ujenzi huu wa huduma za afya kwa wananchi wetu”,alisema.
Vile vile Dk.Samanii ameiomba Mamlaka ya Bandari Tanzania (PTA) iruhusu mapema mashine,vifaa tiba na vya ujenzi vilivyokwama bandarini hapo ili kazi hiyo ya ujenzi iweze kuendelea.
“Tunawashukuru kwa namna ya kipekee wafadhili wa nje ya nchi kupitia kwa PD Alessandro Nava na Dk.Manuela Buzzi,.kwa kukubali maombi ya Askofu kufanya kazi hii ya kihistoria,”.alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk.Binilith Mahenge akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo aliwashukru wafadhili wanaofanya upanuzi wa hospitali hiyo na kuwataka washirikiane na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ikungi jambo litakalosaidia kupunguza hama kumaliza kero zitakapokuwa zikijitokeza.
“Jambo jingine nawaomba kabla ya kuagiza vifaa au kitu cho chote kutoka nje ya nchi hakikisheni mnaishirikisha ofisi ya mkuu wa wilaya ili waweze kupewa taratibu za kupata msamaha wa kodi au mwingine wowote. Ninawapongeza kwa uamuzi wenu mzuri wa kuiunga mkono serikali katika kuboresha sekta ya afya”,alisema Dk.Mahenge.
Wakati huo huo,Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,Jerry Muro,alisema milango ya ofisi yake itakuwa wazi kwa ajili ya kushirikiana na wafadhili na wadau wa maendeleo ndani ya wilaya hiyo.
Katika ziara hiyo wilayani Ikungi Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge alikagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Hospitali Teule ya Makiungu na Chuo cha Ufundi VETA.