Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Mkoa wa Singida Yohana Msita akizungumza kwenye ukaguzi huo.
Na Dotto Mwaibale, Mkalama.
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida imefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama na kukagua utekelezaji wa Ilani kwenye miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Alhaji Juma Kilimba akiwa ameambatana na wajumbe wake aliipongeza Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa utekelezaji wa miradi.
Miongoni mwa miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba sita za wakuu wa idara, ujenzi wa uzio kuzunguka ofisi za Halmashauri urefu wa mita 750, ujenzi wa madarasa mawili na vyoo ,matundu 12 Shule ya Sekondari Gumanga, ukamilishaji wa vyumba viwili vya maabara Sekondari ya Mpambala, mradi wa maji Kijiji cha Nkungi.
Mradi mingine iliyotembelewa na kamati hiyo ni upanuzi wa wodi ya watoto kwa gharama ya Sh.180 milioni, wodi ya wanawake 160 milioni na wodi ya wanaume 160 milioni katika Hospitali ya Wilaya.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisikitishwa na ukarabati wa vyumba vya maabara katika Shule ya Sekondari Chemchemi ambavyo vimejengwa chini ya kiwango ukilinganisha na vile vilivyokarabatiwa kwa Sh.25 milioni katika Shule ya Sekondari ya Gumanga licha ya kutolewa Sh.35 milioni kwa kila shule kwa ajili ya ukarabati huo.
Alisema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo hivyo kuna kila sababu ya kuzitumia vizuri kwa manufaa ya wananchi.
Katika ziara hiyo viongozi mbalimbali walikuwepo wakiwemo wakuu wa idara wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo ya Mkalama Sophia Kizigo.
Leo kamati hiyo itafanya ziara ya namna hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida
No comments:
Post a Comment