Makamu
wa Pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Hemed Suleiman Abdulla
ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha kuwa
wakati upanuzi wa Bandari ya Tanga ukielekea ukingoni wahakikishe kuwa
wanaitangaza kimataifa ili kuvutia wateja.
Ametoa agizo hilo leo
wakati akifanya ukaguzi wa Bandari ya Tanga ambapo yupo katika ziara ya
kikazi ya siku nne mkoani Tanga,hivyo upanuzi wa bandari hiyo
unaotekelezwa na kampuni ya CHEC kutoka China ukielekea ukingoni ni vema
mamlaka hiyo ikaanza mikakati ya kuitangaza bandari hiyo wakati ujenzi
ukiendelea.
Amesema kuwa katika upanuzi huo, serikali imewekeza
zaidi ya kiasi cha Sh.bilioni 400 hivyo lazima kuwe na tija kuona ni
namna gani serikali itarudisha hiyo fedha."Serikali imetumia zaidi ya
Sh.bilioni 400 katika upanuzi wa bandari hii ambayo ni nguzo muhimu
kiuchumi sio kwa mkoa wa Tanga pekee bali hata mikoa ya kanda ya
Kaskazini.
"Visiwani na nchi za Rwanda na Burundi,hivyo
itangazeni hii bandari kimataifa ili wateja waanze kuja kabla hata
ujenzi haujakamilika ikiwemo kuweka promosheni ili kuwavutia wateja na
pia wekeni mazingira rafiki kwa wafanyabiashara ili walipe kodi kwa
mujibu wa sheria," amesema.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mkuu
wa Bandari,Eric Hamisi amekiri mamlaka hiyo kutoitangaza bandari hiyo na
kuahidi kutelekeza agizo hilo mara moja ikiwemo kutumia ofisi za balozi
za Tanzania zilizopo nje ya nchi kwa kutoa elimu kwa kutumia lugha za
asili za nchi husika ili kuwa na uelewa pamoja na kuimarisha ofisi za
TPA katika nchi hizo.
" Ni kweli bado bandari hii haijatangazwa
sana kimataifa lakini mkakati uliopo ni kuhakikisha tunashirikiana na
ofisi za balozi zetu nje ya nchi kwa kutoa elimu,kuanzaa
vipeperushi,mawasilisho kwa kutumia lugha za nchi husika pamoja na
kuimarisha ofisi zetu katika bandari hizo," alisema.
Wakati huo
huo Ofisa Mradi kampuni ya CHEC, Lyu Wei amesema mradi huo umetekelezwa
kwa awamu mbili,awamu ya kwanza ambayo imekamilika kwa asilimia 100
tangu Mei 2020,imetumia kiasi cha Sh.bilioni 172 na awamu ya pili
imetumia Sh.bilioni 256 , ipo katika hatua ya mwisho ikiwemo kuleta
mashine mbili za bandari.
Kwa upande wake,Meneja wa Bandari ya
Tanga, Donald Ngaile amesema kuwa kukamilika kwa bandari hiyo kutaondoa
msongamano katika Bandari ya Dar es salaam, kupunguza gharama ya kutoa
mizigo mara mbili kati ya meli-tishali na kutoka kwenye tishali- nchi
kavu kwa asilimia 40.
Pia kupunguza gharama za matumizi ya mafuta zinazotumika katika boti za kuvuta tishali ,kufupisha muda wa kuhudumia meli kutoka siku tano mpaka sita hadi kufikia saa 24 pamoja na kuongeza idadi ya kupokea meli nyingi na kuhudumia shehena kutoka tani 700,000 hadi tani milioni 3.
No comments:
Post a Comment