Charles James, Michuzi TV
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Gaudentia Kabaka amepokea wanachama 10 kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo amesema kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Samia Suluhu ndio inawavutia wapinzani kujiunga na chama hicho.
Kabaka amesema uwezo wa Serikali ya CCM kushughulikia matatizo na changamoto za watanzania umekua ukiwavutia wapinzani ambapo amesema idadi kubwa ya wanachama wa vyama vya upinzani kujiunga na CCM itaendelea.
Hayo yamefanyika katika ziara ya Mwenyekiti huyo wa UWT Taifa katika Wilaya za Manyoni na Iramba Mkoani Singida ambapo yeye ni mlezi wa kichama wa Mkoa huo.
Akiwa ziarani humo Kabaka amekagua ujenzi unaoendelea wa nyumba ya Katibu wa UWT wilaya ya Iramba wenye gharama ya Sh Milioni 34 ambapo amefurahishwa kasi inayoendelea katika ujenzi pamoja na thamani ya fedha inayotumika kujenga huku yeye mwenyewe akichangia kiasi cha Sh Milioni Moja kufanikisha ujenzi huo.
Pia Kabaka amekagua jengo la lishe lililopo katika hospitali ya Kiomboi wilayani Iramba ambalo limegharimu kiasi cha Sh Milioni 150 ambalo nalo ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo.
Mwenyekiti Kabaka pia ametembelea kikundi cha wajasiriamali kiitwacho JIPEMOYO ambacho kinajishughulisha na kilimo Cha Alizeti chenye ukubwa wa ekari 10 na ufugaji wa nyuki mizinga 45.
Kikundi hiki kimenufaika na mkopo usio na riba ulitolewa na Halmashauri ya wilaya ya Iramba ambapo idadi ya kikundi hiko ni watu 20 na wamekopeshwa kiasi Cha Shilingi Milioni 10.
Aidha Kabaka amewasihi viongozi wa serikali kuhakikisha wanatumia vizuri fedha zinazotolewa na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo.Pia amewakumbusha kuwa makini katika ujenzi wa miradi inayoendana thamani halisi ya Fedha zinazotolewa na Serikali kuu au zile zinazotokana na makusanyo ya vyanzo vya mapato ya Halmashauri husika.
No comments:
Post a Comment