Matokeo chanyA+ online




Thursday, September 16, 2021

NAIBU KATIBU MKUU WA CCM (BARA), CHRISTINA MNDEME, AMESEMA MWAKANI NI MWAKA WA UCHAGUZI NDANI YA CHAMA NI VYEMA WANACHAMA KUJIPANGA IPASAVYO

 


 

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (Bara), Christina Mndeme, amesema mwakani ni mwaka wa uchaguzi ndani ya chama ni vyema wanachama kujipanga ipasavyo

Amesema chaguzi hizo za Chama ni muhimu, ili kupata viongozi watakaomsaidia Rais Samia Suluhu Hassan, katika kusimamia utekelezaji wa Ilani.

Mama Mndeme amesema hayo jana katika viikao vya shina namba moja na mbili Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi katika ziara ya Wajumbe  wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama Daniel Chongolo.

Ziara hiyo imelenga kuhamasisha uhai wa Chama kwa umma na kusimamia  utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020/2025.

Mama Mndeme alisema wanachama wajiandae na uchaguzi bila kuwapo na mpasuko.

"Leo Rais amesema tumepata Rais mwanamke kwa kudra za Mungu na mfumo wa Katiba yetu mwaka 2025 ndio tunaenda kuchagua Rais mwanamke maandalizi yanaanza sasa ndani ya CCM, ikiwemo kuchagua viongozi wazuri uchaguzi wa mwakani,"alisema.

Alisema ni muhimu kamati za siasa na viongozi wa mashina kukemea kuchafuana na kuweka mazingira rafiki ya ushindi wa CCM.

"2025 tunaenda na Rais Samia tusikubali kupasuka,  sumu haijaribiwi tusiweke mazingira ya kuwapa wenzetu nafasi,"alisema.

Aliongeza kuwa "Hakuna haja ya kusikiliza wenye nia mbaya na taifa, serikali ikisema hivi wao wanageuka na kusema hivi hawaridhiki,"alisema.

Pia alisema ni vyema viongozi wa CCM wasifunge milango katika kusikiliza wananchi, kwa kutambua kuwa  Ruangwa ina heshima yake ni Jimbo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Mama Mndeme alisema ni wakati wa CCM kuhakikisha Chama, kinaheshimiwa na kutekeleza Ibara ya 251 ya Ilani, inayoelekeza kuwapo kwa ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ipasavyo.

Alihimiza haja ya kupokea wanachama wapya na kulipa ada, kuimarisha amani na kuwapo huduma muhimu kwa wananchi ikiwemo huduma bora za afya hususani kwa wazee.

Alisema Ibara ya 83 ya Ilani ya CCM inaeleza umuhimu wa kuwapo afya bora na kuwa na dirisha la wazee kwakuwa mchango wao ni mkubwa katika kutumikia taifa.

Mama Mndeme alisisitiza wanachama na wananchi kujipanga kwa ajili ya maandalizi ya sensa ifikapo mwakani, kwakuwa maendeleo yanahitaji watu wake kuhesabiwa.

"Rais amezindua sensa, wakati ukifika tujitokeze huwezi kusonga ugali wa watu watatu ndani kuna watu watano hawatashiba, ni lazima kujua idadi na mahitaji yaliyopo na tujiepushe na wapotoshaji tukahesabiwe,"alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ruangwa Saidi Kaondo alisema chaguzi nyingi zimepita hivyo Chama kisiwe na wasiwasi aliyeamuliwa na Mungu ndio atakayepita.

Alisema CCM Ruangwa haina mwenyewe wala mwenye hati miliki bali Chama kwanza mtu baadaye hivyo hakutakuwa na makundi wala migogoro.

"Tufikishie salamu kwa Rais Samia tumepata viatilifu bure vya korosho, haijawahi kutokea tutampa heshima kwa kuweka maslahi ya Chama mbele,"alisema.


No comments:

Post a Comment