Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amesisitiza umuhimu wa Sensa, mikutano ya Mashina na kuwaacha waliopata dhamana kufanya kazi.
Amezungumza hayo leo tarehe 15 Septemba, 2021 wakati wa Mapokezi ya ziara yake Mkoa wa Lindi akiambatana na Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Akizungumzia suala la Sensa ya Watu na Makazi, Katibu Mkuu amewataka viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali kuhakikisha katika maongezi yao na wananchi wanahamasisha zoezi la Sensa lililozinduliwa na Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Mhe. Samia Suluhu Hassani Jijini Dodoma, ambalo linatarajiwa kufanyika Mwaka 2022, kwani Sensa ndio msingi wa maendeleo ya nchi na uchumi wetu.
"Sensa katika nchi ndio Uchumi na ndio Maendeleo, tukitengeneza mazingira mazuri ya kuhamasishana na kujitokeza vya kutosha katika kushiriki Sensa zoezi ambalo limezinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Dodoma, tutaipa serikali fursa ya kupanga Mipango ya Maendeleo kwa urahisi na kufikia maendeleo yenye usawa na kwa haraka." Katibu Mkuu amesisitiza
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amewaonya watu wanaofuatilia nafasi za ubunge na udiwani wanapaswa kuacha mara moja, kwani Uchaguzi umeshapita na CCM haiwezi kuwa Chama cha Uchaguzi wakati wote badala ya kuwaletea wananchi maendeleo.
"Kama unapenda Ubunge ama udiwani subiri 2025 sasa hivi chokochoko katika majimbo zinatoka wapi,na chokochoko za nafasi zinatoka wapi..?waacheni wabunge wafanye kazi wanazofanya, subirini 2025, tukihangaika kuwafuatilia sasa hivi na kuwazushia uongo tutafika mwaka 2025 na majeraha makubwa." Katibu Mkuu ameeleza
Ameongeza kuwa, "Kila mtu anahaki ya kutumia nafasi yake ya uanachama ndani ya Chama hiki kugombea, lakini hana haki ya kumsumbua aliyeshinda uchaguzi kwa kuwa tuna kazi ya kujenga nchi na kutekeleza Ilani ya Chama chetu."
Akizungumzia Uhai wa Chama Mashinani, Katibu Mkuu amesema, katika uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama unaotarajiwa kufanyika mwakani, mtu akitaka kuchagulia kuwa Kiongozi ndani ya Chama ni lazima awe amehudhuria mikutano ya mashina. Mwanachama hawezi kuwa Kiongozi wa Chama kama hakushiriki mikutano ya Mashina kwa ushahidi wa mihutasari.
Akiendelea na Ziara Wilayani Kilwa Katibu Mkuu ametembelea na kukagua ujenzi wa kituo cha Afya cha Chumo na kuhudhuri mkutano wa Shina namba 3 Tawi la Chumu Kata ya Chumo.
Huu ni muendelezo wa Utekelezaji wa Maelekezo ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa cha tarehe 29 Juni, 2021ikiwa ni kuimarisha Uhai wa Chama katika ngazi za Mashina pamoja na Kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025.
No comments:
Post a Comment