Matokeo chanyA+ online




Thursday, April 14, 2022

KITETO WANUFAIKA NA MILIONI 80 ZA MAJOSHO




Jamii ya wafugaji wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, wanatarajia kunufaika na majosho matano ya kuogeshea mifugo yao baada ya Serikali kuwapatia sh80 milioni za kuwajengea majosho hayo.

Mbunge wa jimbo la Kiteto, Wakili msomi Edward Kisau Ole Lekaita amesema majosho hayo yatajengwa katika vijiji vya Makame, Mwitikira, Loolera, Katikati na Ngabolo.

"Lengo ni kwa ajili ya kuboresha afya za mifugo na tumepatiwa sh80 milioni fedha hizo kutokana na ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega aliyoifanya mwanzoni mwa mwaka huu mifugo ilipokufa kwa ukame," amesema.

Amesema fedha walizopata ni za ujenzi wa josho la kijiji cha Loolera kata ya Loolera sh16 milioni, josho la kijiji cha Mwitikira kata ya Kiperesa sh16 milioni na josho la kijiji cha Katikati kata ya Makame sh16 milioni.

Amesema ujenzi wa josho Kijiji cha Ngabolo kata ya Ndedo ni sh16 milioni na josho la kijiji cha Makame kata ya Makame sh16 milioni.

"Kwa niaba ya wananchi wa jimbo la Kiteto, tunamshukuru sana Rais mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wote Serikalini kwa kugusa maisha yetu wana Kiteto," amesema Ole Lekaita.

Amesema majosho hayo yatasaidia kuboresha sekta ya mifugo kama ilivyoelekezwa kwenye ilani ya CCM 2020-2025 ya kujenga Majosho katika Vijiji vyenye mifugo kama ilivyoelezwa katika ukurasa wa 51 Ibara ya 40 (c) ( ix) ilani CCM ya mwaka 2020/2025.

Amesema ahadi yao kwa Rais Samia ni kuzisimamia Fedha zilizotengewa zionyeshe matokeo makubwa yenye ufanisi na tija kwa wananchi wa Kiteto.

Amesema fedha hizo zimeshalipwa kwa wazabuni na kazi za kujenga majosho zinatarajiwa kuanza wakati wowote hivi karibuni. 

No comments:

Post a Comment