Matokeo chanyA+ online




Sunday, April 24, 2022

WAZIRI MCHENGERWA ATOA SIKU TATU KWA BODI YA FILAMU TANZANIA KUTEKELEZA MAELEKEZO YAKE

 Na. John Mapepele



Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe Mohamed Mchengerwa leo Aprili 23, 2022 amefanya ziara ya kikazi kwenye taasisi ya Bodi ya Filamu nchini (TFB) na kujadili mikakati mbalimbali ya kuboresha na kuleta mapinduzi kwenye tasnia Filamu nchini ambapo ametoa siku tatu za kufanyia kazi maelekezo kadhaa aliyoyatoa.

Mhe. Mchengerwa amesema tasnia ya filamu inazalisha ajira na kutoa mchango mkubwa kwenye taifa hivyoTFB inatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na kasi ili kuleta mapinduzi yanayositahili kwenye sekta hiyo hapa nchini.

Akiwakilisha baadhi ya mikakati ya TFB, kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi hiyo, Mtendaji Mkuu wa Taasisis hiyo, Dkt. Kilonzo Kiagho amesema taasisi hiyo imejiwekea mikakati kabambe ambayo inaendana na miongozo mbalimbali ya Serikali ikiwa ni pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Ameitaja baadhi ya mikakati itakayoleta mageuzi makubwa kwenye tasnia hiyo kuwa ni pamoja na kuanzisha tozo la filamu kwenye visimbuzi, kuandaa mafunzo kwa wadau wa Filamu, mikakati mingine ni kuandaa filamu za kimkakati kwa taifa ambapo amefafanua kuwa “filamu zitakazosaidia kutunza na kuenzi utamaduni wa nchi yetu kwa vizazi vijavyo.

Filamu za aina hii zitafanya mageuzi makubwa hapa nchini na kuondoa dhana ya kutokuwa na filamu za kizalendo kama wanavyofanya mataifa yaliyoendelea kifilamu duniani, na kutunza kumbukumbu za kihistoria kwa kuhusisha hadithi za viongozi mbalimbali waliopigania uhuru kama vile Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye alisaidia ukombozi wa nchi mbalimbali barani Afrika”

Kufanya Tamasha kubwa la kitaifa la Tuzo za Filamu nchini na kuanzisha kwa ujenzi wa eneo changamani la kuzalisha Filamu pamoja na Jumba Changamani ambapo ameongeza kuwa Mradi huu ni wa kimkakati ambao ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025 unaotarajiwa kuwa na miundombinu ya kisasa itakayowezesha kuwa na uzalishaji wa mazao bora ya filamu kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Baadhi ya miundombinu inayotarajiwa kujumuishwa katika mradi huu ni pamoja na maeneo ya kisasa ya uzalishaji wa picha jongevu, Kumbi za kuoneshea Filamu, Ofisi za kampuni za Filamu, Vituo au Vyuo vya mafunzo ya uzalishaji wa Filamu, Maeneo ya kibiashara; na Miundombinu kwa ajili ya mikutano na matukio mbalimbali.

Aidha, Dkt Kilonzo amesema Bodi ya Filamu Tanzania imeona kuna umuhimu mkubwa wa kuitangaza nchi kama sehemu yenye utajiri wa mandhari bora na nzuri duniani inayofikika kirahisi zaidi kwa ajili ya kupiga picha za filamu.

Baada ya mawasilisho hayo ambayo kwa kiasi kikubwa Mhe. Mchengerwa amekubaliana nao na kutoa maboresho na maelekezo mahususi ambayo ametoa siku tatu kuhakikisha kuwa yametekelezwa.

Wakati huohuo Mhe. Mchengerwa amekutana na Rais wa Shirikisho la Filamu nchini bwana Eliya Mjatta na kufanya mazungumzo ambapo Mjatta ametumia nafasi hiyo kueleza pia mikakati ya shirikisho hilo nchini.




No comments:

Post a Comment