Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.
Philip Mpango amekemea vitendo vya uonevu, unyanyasaji na ukatili katika
maeneo ya kazi ambayo husababisha wafanyakazi kudhalilishwa na kuwa
wanyonge mahali pa kazi hususani manyanyaso ya umri, jinsia, rangi, kabila,
ulemavu pamoja na dini.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Hafla ya Utoaji Tuzo za Mwajiri
Bora wa Mwaka 2022 zinazoratibwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE)
iliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam. Amesema
vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu na vinaathiri utendaji wa kazi
sio tu kwa waathirika, bali kwa viongozi na Taasisi au Mashirika wanayofanyia
kazi. Ameongeza kwamba kila mfanyakazi ana haki ya kutendewa utu,
kuthaminiwa na kuheshimika kazini na kuagiza kuwekwa mifumo
itakayowezesha wafanyakazi kutoa taarifa za kunyanyaswa au kuonewa bila
kuhofia madhara yoyote yanayoweza kujitokeza ikiwemo kupoteza ajira zao.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi waajiri hapa nchini kuzingatia
sheria na kutoa mikataba ya kazi kwa kazi zinazostahili mikataba badala ya
kuwafanyisha watu kazi kama vibarua kwa kazi ambazo wangeweza kupata
mikataba ya kazi. Aidha ameiagiza Wizara ya Kazi kutoa elimu kwa waajiriwa
kujua haki zao na pia kuhakiki aina ya mikataba inayotolewa ili ikidhi vigezo
vyote muhimu ikiwa ni pamoja na kuainisha wajibu na haki za
mwajiri/mwajiriwa kwenye masuala ya afya, likizo, ulemavu, mafao na
migogoro.
Pia amewasisitiza waajiri kuzingatia sheria zilizopo kuhusu ajira kwa wageni
ikiwemo kuhakikisha nafasi zisizo za kitaalamu au ambazo utalaamu wake
unaweza kupatikana hapa nchini hazitolewi kwa wageni. Amesewasihi waajiri
kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kulingana na tija yao katika
uzalishaji ili waweze kujikimu kimaisha kulingana na wakati ikiwa ni pamoja
na kutoa posho, tuzo na motisha mbalimbali ili kutambua mchango mkubwa
wa wafanyakazi bora katika taasisi, kuwapandisha vyeo na kuwapatia stahili
zinazoendana na nafasi zao.
Makamu wa Rais amewataka kutumia tuzo hizo kuwa chachu ya kuboresha
mazingira ya mahali pa kazi na kuhamasisha utendaji wenye tija kwa manufaa
ya taasisi na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Aidha, amewahakikishia kuwa
kupitia Serikali, Vyama vya Waajiri na Vyama vya wafanyakazi kuendelea
kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu Ajira na Kazi nchini ili kuboresha
na kutatua changamoto zilizopo kwa pamoja. Amesema kwa upande wa
Serikali chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan, imejipanga kuhakikisha sheria na sera za nchi zinakidhi mahitaji ya
waajiri na waajiriwa.
Awali akimkaribisha Makamu wa Rais katika hadhara hiyo, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce
Ndalichako ametoa wito kwa waajiri wa sekta binafsi kuzingatia kima cha chini
cha mshahara kilichopangwa kuanza kutumika Januari 2023. Amesema waajiri
wanapaswa kutambua kwamba wafanyakazi ndio nguzo muhimu katika ufanisi
wa shughuli wanazozifanya hivyo hawana budi kuwathamini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Hafla ya Utoaji Tuzo za Mwajiri Bora wa Mwaka 2022 zinazoratibwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) iliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam. |
No comments:
Post a Comment