Tuesday, October 10, 2023
WAPELELEZI NA WAENDESHA MASHTAKA WA SERIKALI WA MKOA WA MARA WAMEKUMBUSHWA KUFUATA WELEDI NA TARATIBU ZA KISHERIA KATIKA KUSHUGHULIKIA MASHAURI YA DAWA ZA KULEVYA ILI KUHAKIKISHA MATOKEO MAZURI.
Kamishna wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Bi. Veronica Matikila, alitoa mada kuhusu upelelezi na uendeshaji wa kesi za dawa za kulevya katika kikundi cha wapelelezi na waendesha mashtaka.
Mada zilizojadiliwa zilijumuisha aina za ushahidi, jinsi ya kuthibitisha makosa ya dawa za kulevya, na maeneo muhimu ya kuzingatia kwa waendesha mashtaka katika kuongoza upelelezi wa kesi za dawa za kulevya.
Mkuu wa Mashtaka mkoa wa Mtwara, Joseph Mauggo, alieleza kuwa mafunzo haya yanafanyika kufuatia maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya. Alisisitiza kuwa mafunzo haya yanalenga kuongeza uelewa wa watendaji wa kesi za dawa za kulevya na kutatua changamoto za kiutendaji. Pia, alitaja kwamba Tume iliyoundwa ilibainisha kuwa Serikali inapoteza kesi nyingi kutokana na kutokuwa na uelewa wa pamoja miongoni mwa watendaji wa kesi za dawa za kulevya.
Lengo kuu la mafunzo haya ni kuimarisha uelewa wa wapelelezi na waendesha mashtaka, kutatua changamoto, na kuonyesha jitihada za Serikali katika kushughulikia tatizo la dawa za kulevya nchini Tanzania.
Mafunzo haya yanaendelea mkoani Mara na yamefanyika awali katika mikoa mingine ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, na Iringa. Jumla ya washiriki 101 wamehudhuria mafunzo haya kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS).
Saturday, October 7, 2023
MAKAMU WA RAIS AKIONGOZA MAPOKEZI YA KARDINALI RUGAMBWA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema serikali itaendelea na kufanya kazi na kushirikiana vema na Kanisa Katoliki pamoja na madhehebu mengine ya dini hapa nchini.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa mapokezi ya Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam akitokea Vatican alipopewa hadhi ya Ukardinali. Amempongeza Kardinali Rugambwa kwa kuendelea kuhubiri amani na umoja wa Watanzania na kumsihi kuendelea kuwa chachu ya amani, upendo na umoja. Makamu wa Rais amesema ni baraka kwa Taifa la Tanzania kupata Kardinali wa tatu.
Kwa upande wake Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa amewaomba watanzania wa kila dini kuendelea kumuombea ili aweze kufanya vema kazi hiyo kwa uaminifu na kuweza kuleta maendeleo ya mwanadamu kwa ujumla kuanzia hapa nchini kimwili na kiroho na baadaye hata nje ya nchi.
Kardinali Rugambwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Kanisa, Serikali na watanzania wote waliomtia moyo na kumtumia jumbe mbalimbali za pongezi zilizompa moyo na kumuimarisha.
SKIMU YA UMWAGILIAJI NSIMBO
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Godfrey Chongolo akikagua Skimu ya Umwagiliaji ya Ugalla katika Kijiji cha Katambike, wilayani Mpanda, ili kuuwekea mpango wa kuukwamua, baada ya mradi huo kukwama tangu 2007. Ndugu Chongolo amefanya ukaguzi wa skimu hiyo iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 800 wakati wa ziara ya kuimarisha uhai wa chama, kusikiliza kero za wananchi na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-25 katika Halmashauri ya Nsimbo, Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi, Ijumaa Oktoba 6, 2023.
WAZIRI MAKAMBA ATUA INDIA KUELEKEA ZIARA YA KIHITORIA YA MHE. RAIS DKT. SAMIA NCHINI HUMO
Picha ya pamoja |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt.Subrahmanam Jaishankar ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atakayoifanya nchini humo kuanzia tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2023. Katika mazungumzo yao yaliyofanyika hivi karibuni jijini New Delhi, viongozi hao pamoja na mambo mengine wamelezea matarajio yao ya kuimarika zaidi kwa ushirikiano kati ya Tanzania na India kupitia ziara hiyo ya kihistoria. Kwa upande wake , Mhe. Makamba amemshukuru mwenyeji wake kwa kumkaribisha nchini humo lakini pia kwa maandalizi mazuri ya ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia nchini humo. Kadhalika, Mawaziri hao walibadilishana taarifa kuhusu ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili na kukubaliana kuongeza jitihada ili kufikia malengo ya pamoja ya kuinua kuwango cha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili na kuhakikisha ushirikiano uliopo unazaa matokeo tarajiwa. Mhe. Rais Dkt. Samia anatarajiwa kuwasili India tarehe 8 Oktoba 2023 kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu. Wakati wa ziara hiyo kutashuhudiwa ubadilishanaji wa mikataba mbalimbali ya ushirikiano katika sekta za uwekezaji, uchukuzi, afya, maji na nyingine nyingi. Ziara hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India hususan kwenye maeneo ya kimkakati na manufaa kwa Tanzania ikiwemo afya, maji, elimu uchumi wa buluu, teknolojia, kilimo, na biashara na uwekezaji. |