Matokeo chanyA+ online




Thursday, June 4, 2020

DKT. ZAINAB CHAULA AZIKUMBUSHA TAASISI ZA SERIKALI KUTUMIA HUDUMA ZA POSTA KUSAFIRISHA BIDHAA NA VIFURUSHI KWA USALAMA ZAIDI


Na Prisca Ulomi - WUUM,  Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula amezikumbusha taasisi za Serikali kutumia huduma za Shirika la Posta Tanzania (TPC) kusafirisha bidhaa, vifurushi na vipeto kwa usalama zaidi

Dkt. Chaula ameyasema hayo wakati wa kikao cha Menejimenti ya Wizara yake na viongozi wa TPC wakiongozwa na Posta Masta Mkuu wa TPC, Hassan Mwang’ombe kilichofanyika jana kwenye ukumbi wa Wizara hiyo uliopo Mtumba, Mji wa Serikali, Dodoma ambapo Shirika hilo lilifika ofisini hapo kwa lengo la kujitambulisha na kuwasilisha taarifa ya Shirika hilo kwa Dkt. Zainab Chaula, Katibu Mkuu mpya wa Wizara hiyo


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainab Chaula

Dkt. Chaula alisema kuwa TPC imepewa dhamana kisheria kuwa msafirishaji mkuu wa barua, vifurushi, vipeto na bidhaa mbali mbali kwa mujibu wa sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Na. 19 ya mwaka 1993 iliyoanzisha Shirika hilo nan i Shirika la umma ambapo Serikali imewekeza

Ameongeza kuwa TPC imefanya kazi kubwa ya kusafirisha sampuli kutoka hospitali mbali mbali nchini kwenda Maabara Kuu ya Serikali wakati wa kipindi cha janga la virusi vya Corona pamoja na kusafirisha nyaraka za mahakama zote nchi nzima, benki, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Mifuko ya Hifadhi za Jamii, hisa za kampuni mbali mbali na kutumia usafiri wa ndege kwenda ndani na nje ya Tanzania

Ameitaka TPC kuunganisha huduma za posta na anwani za makazi na postikodi na simu za mkononi ili kuhudumia wananchi katika kufanikisha azma ya Serikali ya kurahisisha na kufanikisha usambazaji na usafirishaji wa barua, vifurushi, vipeto na bidhaa kwa wananchi

“Tunataka mwananchi afikishiwe nyanya nyumbani kwake na sio atumie piki piki kuzunguka kwa muda mrefu na kupiga simu bila kufika kwa mteja kwa wakati,” amesisitiza Dkt. Chaula

Naye Posta Masta Mkuu wa TPC, Hassan Mwang’ombe ameziomba taasisi za Serikali kutumia Shirika hilo kusafirisha barua, vifurushi na vipeto kwa kuwa bidhaa zao zitafika kwa usalama na uhakika kwa kuwa Shirika hilo linatumia huduma ya mtandao wa TEHAMA kutoa huduma zake kwa wateja kwa kuunganisha ofisi zake 202 zilizopo maeneo mbali mbali nchi nzima; wana wataalamu wa lojistiksi; na wanatumia anwani za makazi na postikodi kuhudumia wateja.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amelishauri Shirika hilo kuwa pamoja na kuboresha huduma zake ndani ya nchi pia amelitaka kufungua milango yake na kufanya biashara na nchi nane za jirani zinazopakana na Tanzania  kwa kuongeza huduma za lojistiksi kwenda nchi za jirani za usafirishaji wa bidhaa, biashara mtandao, uwakala na maduka ya kubadilisha fedha ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti mara kwa mara ili kuendeleza biashara za Shirika hilo

Naye Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara wa Shirika hilo, Mwanaisha Ally Said, ameiomba Wizara kuhakikisha kuwa watoa huduma za usafirishaji wa nyaraka, vifurushi na vipeto wasio na leseni ya kuendesha biashara hiyo inayotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ili kuhakiisha kuwa wananchi wanapata huduma za sekta ndogo ya posta na Serikali inapata mapato yake

MBUNGE MATTEMBE ATOA MSAADA WA KOMPYUTA SHULE YA SEKONDARI ILONGERO

 Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe (wa pili kushoto) akikabidhi msaada wa kompyuta tano na printa moja zenye thamani ya Sh.milioni 9.7 katika Shule ya Sekondari ya Ilongero iliyopo Wilaya ya Singida  mkoani Singida. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida,  Eliya Digha, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri,  Diwani wa Kata ya Ilongero,  Issa Mwiru na Mkuu wa shule hiyo, Ramadhan James.
 Vifaa hivyo vikikabidhiwa. Wengine ni viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo.


Hapa wakionesha ishara ya mshikamano.




Na Dotto Mwaibale, Singida

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe ametoa msaada wa kompyuta tano na printa moja zenye thamani ya Sh.milioni 9.7 katika Shule ya Sekondari ya Ilongero iliyopo Wilaya ya Singida  mkoani Singida.

Mattembe akizungumza juzi wakati akitoa msaada huo alisema umelenga kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. John Magufuli za kuhakikisha mpango wa utoaji elimu bure kwa kila mtoto hapa nchini unaendelea kufanikiwa.

" Niliona ni muunge mkono Rais wetu kwa kutoa msaada huu kwa wanafunzi wetu hawa wa Sekondari ya Ilongero kusoma masomo ya ICT  kwa njia ya vitendo ili waendane sanjari na ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia." alisema Mattembe.

Mattembe alisema dunia hivi sasa imepiga hatua kubwa ya maendeleo hasa katika matumizi ya teknolojia hivyo wanafunzi wetu wasipojifunza masomo ya ICT watachelewa kuyafikia mafanikio.

" Hivi sasa kila jambo linalofanyika linafanyika kwa njia ya mtandao ambapo ni lazima muhusika ajue kutumia kompyuta au simu sasa tukiacha kuwekeza katika masomo hayo itakuwa changamoto kubwa kwa watoto wetu." alisema Mattembe.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri ambaye alikuwa mgeni rasmi katika makabidhiano hayo akizungumza wakati akimkabidhi msaada huo mkuu wa shule hiyo,  Ramadhan James, alisema msaada huo umekuja wakati muafaka ambao utawasaidia wanafunzi kujifunza masomo kwa ufasaha hasa kipindi hiki ambacho dunia inaunganishwa na mitandao.

"Pamoja na yote katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona kompyuta hizi zitasaidia wanafunzi wetu kujifunza kwa njia ya mtandao bila ya kuwa darasani hivyo napenda kumshukuru Mhe.Mattembe kwa kuona mbali na kutoa msaada huu ambao umefika kwa wakati muafaka"  alisema Mulagiri.

Wageni waalikwa wengine katika  makabidhiano ya kompyuta hizo walikuwa ni  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida,  Eliya Digha, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Wilaya ya Singida,  William Nyalandu,  Diwani wa Kata ya Ilongero,  Issa Mwiru,  Diwani Viti Maalumu wa kata hiyo, Mwanamosha Bakari, Diwani Viti Maalumu, Salma Kundya na Katibu Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Singida, Naomi David.

Wengine walioshuhudia makabidhiano hayo ni walimu wa shule hiyo,wenyeviti wa Serikali za mitaa wa Ilongero  na baadhi ya wazazi.

MBUNGE MAVUNDE AKABIDHI GARI LA KUSAFIRISHA WAGONJWA KITUO CHA AFYA CHA MKONZE



Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde leo amekabidhi gari la wagonjwa(Ambulance) kwa ajili ya kituo cha Afya cha Mkonze Jijini Dodoma.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo katika kituo cha Afya cha Mkonze ambapo gari hili litatoa huduma ya usafirishaji wa wagonjwa wa rufaa kutoka katika kituo hicho ikiwa ni ahadi aliyoitoa Mbunge Mavunde wakati wa kuweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Kituo hicho cha Afya wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018.



"Namshukuru Rais Magufuli kwa ujenzi wa Vituo vya Afya nchini kikiwemo hichi cha Mkonze.Tulikuwa tumebakiza gari tu la wagonjwa na leo tumepata,ni furaha kubwa sana kwamba wananchi wangu sasa watapata fursa ya huduma ya usafirishaji wa wagonjwa tofauti na ilivyokuwa pale awali"

Diwani wa Kata ya Mkonze Mh David Bochela amemshukuru Rais Magufuli kwa ujenzi wa kituo cha Afya cha kisasa ambacho kimerahisisha utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi na pia amemshukuru Mbunge Mavunde kwa ufuatiliaji na upatikanaji wa gari hilo ambalo litasaidia kutatua changamoto ya namna ya kuwasifirisha wagonjwa kutoka kituoni hapo kwenda Hospitali ya Rufaa.

HATUTAKI MANENO TUNATAKA WANUNUZI WENYE FEDHA, RC KAGERA AWATAKA WANUNUZI WA KAHAWA KUINGIA SOKONI

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti akisisitiza jambo wakati akizungumza na Uongozi wa Bodi ya Kahawa Ofisini kwake Mjini Bukoba, leo tarehe 4 Juni 2020. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti akisisitiza jambo wakati akizungumza na Uongozi wa Bodi ya Kahawa Ofisini kwake Mjini Bukoba, leo tarehe 4 Juni 2020. 
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam akiteta jambo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg Emmanuel Sherembi wakati wa ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe Richard Ruyango akisisitiza umuhimu wa elimu kutolewa kwa vyama vya Ushirika kuhusu kuimarisha ubora wa kahawa wakati wa kikao kazi na watendaji wakuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania pamoja na vyama vya Ushirika vya Wilaya hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi na wanunuzi binafsi wa Kahawa katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa ELCT Mjini Bukoba leo tarehe 4 Juni 2020. Wengine pichani ni Afisa Biashara wa Mkoa wa Kagera Ndg Isaya Tendega akimuwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa (Kushoto), Meneja wa Bodi ya Kahawa kanda ya Kagera Ndg Melkiad Masawe (Wa pili kutoka Kulia) na Kaimu Mwonjaji wa kahawa na Dalali Mkuu Bodi ya Kahawa Tanzania Ndg Rogatus Meela (Wa kwanza kulia) 
Sehemu ya wanunuzi binafsi wa Kahawa wakifatilia maelekezo ya serikali yaliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam kuhusu ununuzi wa Kahawa katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa ELCT Mjini Bukoba leo tarehe 4 Juni 2020. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Kagera

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti amesema kuwa serikali inaunga mkono wanunuzi binafsi kwenye zao la Kahawa japo wamechelewa sana kuingia sokoni kuanza kununua kahawa za wakulima.

Gaguti ameyasema hayo leo tarehe 4 Juni 2020 wakati akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam ofisini kwake Mkoani mjini Bukoba na kuwataka wanunuzi hao kuingia sokoni.

"Serikali haitaki maneno inataka wakulima wapate fedha kwa wakati, wanunuzi binafsi wamechelewa sana kuingia sokoni tulitegemea waingie sokoni tangu mwezi wa pili waanze kuingia makubaliano na Vyama vya Ushirika, lakini hawajachelewa sana waje ofisini kwangu waeleze wazi wanataka kahawa kiasi gani kisha tuingie makubaliano ya awali" Alikaririwa Rc Gaguti

Ameongeza kuwa Wanunuzi binafsi wanapaswa kujitokeza hadharani watoe ofa yao ikieleza kuwa wanataka kununua kiasi gani cha kahawa ili kuhuisha maneno yao kwa matendo.

Awali katika mkutano uliofanyika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Richard Ruyango alisisitiza kuwa serikali itaendelea kusimamia mipango yake katika zao la Kahawa hususani kuimarisha usimamizi madhubuti ili kuwa na kahawa Bora kwa kuongeza tija na Uzalishaji.

Kuhusu wanunuzi binafsi amesema kuwa wanapaswa kutekeleza sheria, na taratibu za ununuzi wa zao hilo ikiwa ni pamoja na kuwa na kibali cha ununuzi kinachotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halamshauri husika pamoja na kuwa na leseni ya Biashara inayotolewa na Bodi ya Kahawa Tanzania.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania Prof Jamal Adam akizungumza na wanunuzi wa Kahawa katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa ELCT Mjini Bukoba ameweka bayana utaratibu wa ununuzi wa kahawa ya wakulima katika Mkoa wa Kagera ambapo Wanunuzi watakaoruhusiwa kununua kahawa ni wale waliopata leseni za kununua kahawa kwa mujibu wa kanuni ya 26 ya Kanuni za Kahawa 2013.

Ameongeza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri watapaswa kutoa vibali kwa haraka kwa wanunuzi wenye sifa ili kuiwezesha Bodi kutoa leseni kwa wakati.

Kadhalika, Prof Jamal amesisitiza kuwa Wakurugenzi wanapaswa kuwajulisha kwa maandishi waombaji watakaonyimwa vibali wakiweka bayana sababu za kutowapatia vibali na nakala ya barua hiyo iwasilishwe Bodi ya Kahawa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Kwa upande wao wanunuzi wa kahawa wamepongeza uamuzi huo wa serikali kuwaruhusu kununua kahawa kwenye vyama vya Ushirika huku wakiahidi kutekeleza taratibu na sheria za ununuzi wa Kahawa.

Akizungumza kwa niaba ya wanunuzi hao Afisa Masoko wa Kampuni ya Karagwe Estate Ltd Ndg Kamanzi Mombeki amesema kuwa Kampuni hiyo imejipanga kurejea tena katika ununuzi wa kahawa baada ya kusimamia kwa zaidi ya miaka miwili kufanya Biashara hiyo.

"Sisi kama Kampuni tunampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kwa kurejesha wanunuzi binafsi kununua kahawa hivyo nasi tumerejea kwa nguvu na Ari kubwa katika ununuzi wa kahawa" Alisema Mombeki

Amesema kuwa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kuhusu wanunuzi binafsi wakati akizungumza na wananchi wa Kyaka, Rwamisheye, Kemondo Muleba, Nyakabango na Kyamyorwa mkoani Kagera tarehe 11 Julai 2019 yalilenga kuongeza ushindani wa kibishara jambo ambalo linamnufaisha zaidi mkulima mwenyewe.

Mombeki ameonyesha kuwashangaa watu wanaopinga maelekezo ya Mhe Dkt Magufuli yenye lengo la kumkomboa mkulima.


WATUMISHI WALIOKWAMISHA MAENDELEO YA MIAKA MITATU YA HALMASHAURI KUWAJIBISHWA

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuwawajibisha watumishi wote walioisababishia halmashauri hiyo kupata hati yenye shaka na kumpatia taarifa ya hatua alizochukua kwa watumishi hao ndani ya siku saba kabla ya mabaraza ya madiwani kuvunjwa.

Amesema kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) yaliyotolewa tarehe 24, April, 2020 kuhusu kushughulikia hoja na mapendekezo ya CAG, pamoja na mambo mengine imeelekezwa kuwa Halmashauri zilizopata Hati yenye Shaka zimepoteza sifa za kupatiwa fedha za utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika kipindi cha miaka mitatu ijayo na hivyo kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo

Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo

“Kwa kupata hati yenye shaka, halmashauri ya wilaya ya Nkasi inapoteza sifa za kupatiwa fedha za utekelezaji wa miradi ya kimkakati ambayo lengo lake ni kupoteza mapato katika halmashauri, hii ni adhabu kubwa sana katika halmashauri yetu, haipendezi, pengine wengine walikuwa wanaichukulia kijuu juu, miradi ya kimkakati ni miradi mukubwa ambayo halmashauri zimepewa nafasi ya kubuni na kupatiwa fedha ya kutekeleza, kama ni stendi za mabasi, maghala au kumbi zamikutano,” Alisema.

Na kuongeza kuwa ,” Hawa waliotufikisha hapa, hawawezi kuachwa hivi hivi, ni lazima wachukuliwe hatua kali za kinidhamu na Mkurugenzi nimekupa siku saba, uwe umetoa adhabu hii, nipate taarifa ndani ya siku saba, iwe nimepata taarifa ya namna hawa watu watakavyoshughulikiwa kinidhamu, hatuwezi kuendelea namna hii watu wanafanya mzaha, wanafanya uzembe, halafu halmashauri inabeba mzigo wa hawa watu wachache wazembe kwanini?” Alikemea.

Wakati akieleza miongoni mwa sababu zilizosababisha halmashauri hiyo kupata Hati ya Mashaka kwenye hesabu za kuishia tarehe 30, Juni 2019 Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo alisema kuwa Ukaguzi wa mtiririko wa fedha (Cash Flows Statements) kwenye kitabu cha hesabu ulionesha kuwa na upungufu wa shilingi 2,528,347,000/=.

“Ukaguzi wa Mtiririko wa fedha kwenye kitabu cha hesabu ilibainika kuwa Halmashauri imeonesha mtiririko wa fedha uliotoka kuwa Shilingi 16,827,818,000 ikiwa ni mishahara, malipo ya vibarua na haki mbalimbali za watumishi, hata hivyo kwenye mchanganuo ilionekana madai ya watumishi yamepungua kwa Shilingi 383,690,000 hivyo kufanya madai ya watumishi kuoneshwa pungufu kwa jumla ya Shilingi 2,528,347,000/=,” Alifafanua.

Aliongeza kuwa kwa upande wa magari na pikipiki, mali za halmashauri, halmashauri ilionesha jumla ya Shilingi 554,292,000/= lakini baada ya daftari la mali za kudumu kupitiwa ilionesha jumla ya shilingi 612,940,420 na khivyo kuonesha upungufu wa Shilingi 58,648,420/=.

Kwa upande wake Afisa Serikali za Mitaa mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya alisema kuwa kati ya Halmashauri 185 zilizokaguliwa kwa hesabu zilizoishia 30 Juni 2019, Halmashauri 176 zilipata Hati Inayoridhisha na Halmashauri 9 zilipata Hati yenye Shaka ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi huku hoja zilizoibuliwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 ni hoja 32 na hoja za nyuma zilizokuwa bado hazijafungwa ni 52.

COVID 19 ILIVYO WAATHIRI WAFANYABIASHARA KATIKA SEKTA ISIYO RASMI HASA WANAWAKE NCHINI

Mkurugenzi Mtendaji wa, Taasisi  isiyo ya Kiserikali ya Equality for Growth (EfG), Jane Magigita (katikati) akizunguma na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu ugonjwa wa Corona ulivyo waathiri wafanyabiashara wa sekta isiyo rasmi hasa wanawake. Kulia ni Mwenyekiti wa muda wa Kitaifa wa Umoja wa Wafanyabiashara Wanawake Masokoni hapa nchini,  Betty Mtewele na Mwezeshaji wa Sheria kutoka Shirika la EfG, Aisha Juma ambaye ni Mfanyabiashara wa Tabata Muslim. 
 Afisa mradi wa EfG , Susan Sitta (katikati) akizungumza katika mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.

Na Dotto Mwaibale

Taasisi  isiyo ya kiserikali ya Equality for Growth (EfG) imesema wafanyabiashara wa sekta isiyo rasmi hasa wanawake, wachuuzi wa sokoni ni miongoni mwa watu walio pata athari za ugonjwa wa COVID 19 . 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Jane Magigita alisema wafanyabiashara hao kutoka katika sekta hiyo ni miongoni mwa watu walioathiriwa na Covid-19.


" Katika kipindi hiki cha Ugonjwa wa COVID 19 tulitumia nafasi hii kukusanya maoni ya wanawake kupitia “Vitendawili vya Corona- Simulizi za wanawake sokoni” ambazo zimetuwezesha kuibua changamoto zinazowapata wanawake wafanyabiashara zikiwemo kupungua kwa wateja, kushuka kwa mapato ya biashara, kushindwa kumudu gharama za barakoa na vitakasa mikono na mazingira kutoruhusu kukaa umbali unaotakiwa katika kujikinga kutokana na miundombinu masokoni." alisema Magigita.

Alisema Covid 19 imekua na madhara makubwa katika ajira hasa katika sekta isiyo rasmi hivyo kupelekea kuyumba na kuwa ajira imeathirika kutokana na kupunguzwa kwa masaa ya kufanya kazi, kufanyia kazi nyumbani na hitaji la kupunguza gharama za uendeshaji. 

Alisema ripoti iliyotolewa na UNDP Tanzania, Economic and Social Research Foundation (ESRF) imeonyesha madhara ya COVID 19 katika makusanyo ya kodi, kuongezeka umaskini na utofauti wa kipato kwa Tanzania. 

Aliongeza kuwa ripoti hiyo imekisia madhara makubwa katika sekta ya hoteli na utalii, uuzaji wa mazao nje ya nchi, usafirishaji na sekta ya fedha pia. Bila kuwa na hatua madhubuti za kukabiliana na COVID 19 itapelekea ugumu kuyafikia malengo endelevu ya dunia (SDGs).

Aidha ripoti nyinginezo nchini zimeonyesha maeneo ambayo yameadhirika sana na COVID 19 ni pamoja na kupungua kwa idadi ya watalii, mapato ya usafiri wa ndege, kufungwa kwa biashara karibu na mashule pamoja na vyuo, biashara za kimataifa, ukwasi wa kifedha, matumizi makubwa kwenye afya, elimu na wingi wa sintofahamu katika biashara. 


Alisema sekta hiyo inaajiri watu wengi zaidi kwani inatoa ajira kwa takribani asilimia 90% ya Watanzania na kuwa takwimu zinaonesha katika sekta isiyo rasmi wanawake ni 74% ya nguvu kazi nchini; 15% ya wanawake pia wamiliki wa biashara; 54% ni wajasiriamali wadogo na wa kati na kuwa wako katika nyanja mbalimbali za uzalishaji na mnyororo wa thamani ikiwemo kilimo, huduma na biashara.

Alisema EfG imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na jamii na kwa kushirikiana na Serikali, katika kuwawezesha wanawake wa sekta isiyo rasmi kuwa na sauti ya pamoja na kuweza kusimamia haki zao za kibiashara na kiuchumi kwa kupinga ukatili pamoja na vikwazo vya kijinsia. 

"Tumewafikia wanawake kwa kutoa mafunzo ya biashara, uwekezaji, ugawanyaji wa mapato, kuweka akiba na sera za ujasiriamali. Pia kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi na kushiriki katika nafasi na vyombo vya maamuzi." alisema Magigita.


Magigita alitaja baadhi ya mapendekezo yao juu ya hatua za kuchukuliwa na wadau mbalimbali kuhusu maendeleo katika majanga ya namna hiyo ni Taasisi za fedha ziangalie namna bora ya kupunguza makali ya marejesho kwa wafanyabiashara wadogo na walio katika sekta isiyo rasmi. Kipaumbele kitolewe kwa wanawake, watu wenye ulemavu, na vijana.

Mapendekezo mengine ni Taasisi za mbalimbali za fedha zinazotoa mikopo midogo ambazo hazisimamiwi moja kwa moja na Benki Kuu kama vikundi vya VICOBA, SACCOS na wakopeshaji binafsi kufikiria namna ya kupunguza riba kubwa zinazotozwa kwa wafanyabiashara wadogo.

Elimu ya Ujasiriamali na usimamizi wa fedha itolewe na taasisi mbalimbali kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini  kwa wafanyabiashara ambao wapo kwenye sekta isiyo rasmi ambao tayari wameathirika na COVID 19.

Kwa kuwa wafanyabiashara wa sekta isiyo rasmi wengi wao hutumia simu kama benki, tunashauri wanaotoa huduma za kibenki kupitia mitandao kupunguza gharama za kutuma na kupokea pesa kutumia mitandao ya simu, na kiwango cha kutuma pesa kiongezwe. 

Halmashauri zote nchini ziendelee kuwezesha vikundi vya wanawake na vijana katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10% ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya miradi na biashara, ambazo zinachangia kumuinua mwanamke kiuchumi.

Benki Kuu imedhamiria kuziwezesha taasisi za kifedha kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha (ukwasi), ili zitoe mikopo yenye riba nafuu kwa wananchi. Kwa kufanya hivyo watanzania walio wengi wataweza kukopa kwa riba nafuu hivyo kuboresha shughuli zao za kuichumi.

Magigita alisema wanatumia fursa hiyo kuwasilisha mapendekezo kwa wafanyabiashara ndogo ndogo wa sekta isiyo rasmi waliochukua mikopo kutoka taasisi za fedha na wameshindwa kuzitumia hizo fedha kutokana na wateja waliokuwa wanatarajia kuwafikia hawapo tena kutokana na COVID 19, wasizitumie hizo fedha kwa shughuli mbadala. Wazirudishe kwa mkopeshaji na wajadiliane kuhusu punguzo la riba.

Biashara zisibadili matumizi ya fedha wakati huu wa COVID 19, ikibidi kufanya hivyo basi watafute ushauri kutoka kwa wataalamu au kwa walio wakopesha/waliowapa fedha.

Wafanyabishara wawe makini sana katika kutafuta vyanzo vya mitaji katika wakati huu ili wasije wakaingia katika mitego ya wakopeshaji wenye riba na masharti yasiyostahimilika. 

Kuchangamkia fursa ama unafuu unaotolewa na serikali pamoja na taasisi nyingine wakati huu wa COVID 19 kukuza biashara zao. 

Maoni ya wanawake wafanyabiashara sekta isiyo rasmi masokoni wakitoa maoni yao kuhusu shughuli zao za kiuchumi kuathiriwa na ugonjwa huo wamesema kutokana na mapato kupungua sana katika biashara zetu kwani na watu hawatembelei masokoni na kukaa nyumbani zaidi. Hii imetokana na kupungua kwa wateja ikiwemo katika mahoteli ambao ndio watumiaji wakubwa wa mbogamboga na matunda tunayouza sokoni.

Kuwepo kwa miundo mbinu inayoweza kuimiri majanga, kwani wanawake wengi waliamua kusimama biashara kwa kuhofia maambukizi ya COVID 19.

Changamoto ya kushindwa kulipa mikopo kutokana na kipato duni, tunaomba taasisi za fedha zilizotupa mikopo, ambazo kwa sasa zinapata unafuu kutoka Benki Kuu zitufikirie zaidi wanawake wa sekta isiyo rasmi.

Sekta isiyo rasmi tunaomba tufanyiwe tathmini ya athari za COVID 19 na kuchukua hatua ili kuwezeshwa kwa kupewa mikopo yenye riba nafuu kama walivyopewa Sekta rasmi nchini. 

Wanawake hao wameipongeza serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania kwa jitihada kubwa na za kimkakati kuunusuru uchumi hususani wakati wa janga la COVID 19. Sanjari na pongezi zetu tumeamua kama shirika kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha athari za COVID 19 zinapunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa wafanyabiashara wadogo hususani wanawake nchini. 

"Kama alivyosema Raisi wetu Dkt. John Magufuli hivi virusi vinaweza kuwa kama majanga mengine na tukalazimika kuishi navyo katika maisha yetu yote, hivyo sera dhabiti zinahitajika kuwasaidia watu wanaoendesha shughuli zao katika sekta isiyo rasmi waweze kujikwamua. Tunaamini kwa kushirikiana, nchi yetu itaendelea kuishinda vita dhidi ya COVID 19, na uchumi wetu kuendelea kuimarika." alisema Mwenyekiti wa muda wa Kitaifa wa Umoja wa Wafanyabiashara Wanawake masokoni hapa nchini,  Betty Mtewele. 


Wednesday, June 3, 2020

IDARA YA UHAMIAJI YAKABIDHIWA NYUMBA 103 ZA MAKAZI KWA MAOFISA NA ASKARI WA IDARA YA HIYO ENEO LA IYUMBU, JIJINI DODOMA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Wa kwanza kushoto) akisalimiana na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (Wa pili kulia) baada ya kuwasili katika eneo la Iyumbu, ilipofanyika hafla ya makabidhiano ya Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, Jijini Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Wa kwanza kushoto) akipokea salamu kutoka kwa Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji Nchini, Dkt. Anna Makakala (Wa kwanza kulia) alipokuwa akiwasili eneo la Iyumbu katika hafla ya kukabidhiwa Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, Jijini Dodoma. 

 Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (Wa tatu kushoto) akiwasili katika  katika eneo la Iyumbu, ilipofanyika hafla ya makabidhiano ya Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, Jijini Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Aliyesimama) akizungumza na Viongozi mbalimbali, Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, eneo la Iyumbu ilipofanyika hafla ya makabidhiano ya Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya hiyo, Jijini Dodoma

Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (Wa kwanza kulia) akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, iliyofanyika eneo la Iyumbu, Jijini Dodoma. 
Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji Nchini, Dkt. Anna Makakala akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji ambapo ametoa salamu za shukurani kwa Rais Dk. John Magufuli na Viongozi wote wa Serikali wa Awamu ya Tano kwa kuwezesha kujengwa Nyumba hizo, Jijini Dodoma


Baadhi ya Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji wakifuatilia hafla ya kukabidhiwa Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya hiyo, yaliyofanyika eneo la Iyumbu, Jijini Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Wa kwanza kushoto) akimkabidhi ufunguo Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (Wa pili kulia) katika hafla ya kukabidhiwa Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, eneo la Iyumbu iliyofanyika leo Jijini Dodoma.

Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (Wa kwanza kulia) akimkabidhi ufunguo Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji Nchini, Dkt. Anna Makakala (Wa kwanza kulia) katika hafla ya kukabidhiwa Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, iliyofanyika eneo la Iyumbu, Jijini Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Wa tatu kulia), Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (Wa pili kulia), Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji Nchini, Dkt. Anna Makakala (Wa kwanza kulia) pamoja na Viongozi mbalimbali wakikata utepe kuashiria Uzinduzi wa kukabidhiwa Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, katika eneo la Iyumbu Jijini Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (katikati), Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (Wa pili kulia), Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji Nchini, Dkt. Anna Makakala (Wa kwanza kulia), Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (Wa pili kushoto) pamoja na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, katika eneo la Iyumbu Jijini Dodoma

Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (katikati), Mkuu wa Majeshi Nchini, Jenerali Venance Mabeyo (Wa kwanza kushoto) pamoja na Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji Nchini, Dkt. Anna Makakala (Wa kwanza kulia) wakiagana baada ya kumalizika hafla ya kukabidhiwa Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, iliyofanyika eneo la Iyumbu, Jijini Dodoma.

Bendi ya Idara ya Uhamiaji, ikitoa burudani kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na Viongozi mbalimbali (hawapo pichani) waliofika katika hafla ya kukabidhiwa Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, eneo la Iyumbu, Jijini Dodoma.

Baadhi ya Nyumba 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, zilizopo eneo la Iyumbu ambazo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amezindua na kukabidhiwa Nyumba hizo 103 za Makazi kwa Maofisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji, Jijini Dodoma leo.

Monday, June 1, 2020

NDEGE YA MIZIGO KUIMARISHA USAFIRISHAJI SAMAKI NJE YA NCHI

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema mipango ya Serikali kununua ndege ya mizigo utaimarisha usafirishaji wa minofu ya samaki moja kwa moja kwenda nje ya nchi kutokea uwanja wa ndege wa Mwanza.

Waziri Kamwelwe ameyasema hayo Jumatatu Juni Mosi 2020 jijini Mwanza wakati akifungua mkutano wa kupokea mikakati ya pamoja kuondoa vikwazo na kufanikisha biashara ya usafirishaji minofu ya samaki kwenda nje ya nchi hususani mataifa ya Ulaya ambako kumekuwa na soko la uhakika.

Kikao hicho kimewajumuisha pia Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara za Mifugo na Uvuvi, Viwanda na Biashara pamoja na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Na George Binagi-GB Pazzo, Mwanza
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (katika) akizungumza kwenye kikao hicho. Kushoto ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa na kulia ni Mkuu wa Mkoa Mwanza, John Mongella.
Tazama Video hapa chini
Attachments area Preview YouTube video Ndege ya mizigo kuimarisha usafirishaji samaki nje ya nchi