Matokeo chanyA+ online




Thursday, August 6, 2020

SERIKALI YASHINDA KESI YA RUFAA YA KUFUTWA KWA KIFUNGU CHA 148 (5) CHA SHERIA YA MWENENDO WA MASHAURI YA JINAI


Serikali imeshinda kesi ya rufaa ya kufutwa kwa kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Sura ya 20 ya Sheria za Tanzania inayozuia dhamana kwa makosa makubwa. Kifungu hicho kinazuia dhamana kwa makossa  ya jinai yakiwemo ya utakatishaji fedha haramu, mauaji, uhaini, unyang’anyi wa kutumia silaha na usafirishaji haramu wa binadamu.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Wakili Mkuu wa Serikali Bwana Gabriel Malata, amesema kuwa Mahakama ya Rufaa mnamo tarehe 5 Agosti 2020, imekubaliana na rufaa ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo ilikuwa ikipinga maamuzi ya Mahakama Kuu yaliyotolewa na jopo la majaji watatu kwa kutamka ya kuwa kifungu cha 148 (5) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai kinakinzana na matakwa ya Sura ya 13 (6) (b) na 15 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa.


Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu katika kesi namba 29 ya 2019 iliyofunguliwa na wakili wa kujitegemea Bwana Dickson Paulo Sanga dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Katika kesi hiyo Bwana Sanga alitaka Mahakama Kuu kufuta kifungu cha 148 (5) kwa kuwa kinakinzana na Sura ya 20 ya Sheria za Tanzania ambapo mahakama Kuu iliridhia maombi yake.

 

“Katika rufaa iliyokatwa na Serikali ilipinga maamuzi ya Mahakama Kuu. Mahakama ya Rufaa ambayo iliketi tarehe 6 Julai 2020, pamoja na mambo mengine ilisikiliza hoja za Serikali, kwamba Kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20 ya Sheria za Tanzania haikinzani na Ibara ya 13 (6) na 15 (1) (2) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema Bwana Malata.

 


 

“Serikali ilieleza kuwa kifungu hicho cha Sheria kinalenga kutekeleza Ibara ya 13 (3) inayofafanua juu ya misingi ya haki, uhuru na wajibu wa mtu na kwamba haki, uhuru na wajibu unatekelezwa kwa kuzingatia Sheria zingine za nchi na haki, uhuru na haki ya watu wengine”.

 

Amesema kwa kuzingatia hayo, Mahakama ya Rufaa imefuta hukumu ya Mahakama Kuu na kueleza kuwa Kifungu cha 148 (5) (a) (i), (ii), (iii), (b), (c), (d) na  (e) Sheria ya Mwenendo wa Jinai Sura ya 20 ya Sheria za Tanzania hakikinzani na Ibara ya 13 (3) na 15(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania badala yake kinalenga katika kuwezesha utekelezaji mzuri wa Ibara ya 30 (2) inayolenga katika kuhakiksha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru na haki za watu binafsi na pia kuhakikisha ulinzi, usalama wa jamii, amani katika jamii, maadili ya jamii, afya ya jamii na utekelezaji mzuri wa mipango ya maendeleo ya jamii.

BASHUNGWA AMEIPONGEZA NMB KWA KUTOA ELIMU YA KIFEDHA BURE


Waziri wa viwanda na biashara Mhe.Innocent Bashungwa ameipongeza Benki ya NMB kwa utoaji wa elimu ya kifedha bure kwa wajasiriamali mbalimbali kwenye maonesho ya Nane Nane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

 

Bashungwa alisema kuwa jambo ambalo linalofanywa na benki hiyo kwenye maonesho hayo ni muhimu sana hasa kwa wakulima, wavuvi na wafugaji ambao wana uhitaji mkubwa wa elimu ya usimamizi wa fedha.

 



Waziri huyo alisema hayo jana baada ya kutembelea banda la Benki hiyo wakati wa maonesho hayo, ambapo alifurahishwa kukuta wakulima, wafugaji na wavuvi wamejitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo.

 

Alisema kuwa lengo kubwa la serikali kuanzisha maonesho hayo ni kutaka wananchi walioko kwenye sekta ya kilimo kuweza kupata teknolojia za kuwawezesha kuongeza tija kwenye uzalishaji wao pamoja na mikopo.

 

“ Wamekuwa wakipata hizi teknolojia lakini bado tatizo lipo kwenye kujua wapi wapate mikopo, lakini pia jinsi ya kusimamia pesa zao, nimefurahishwa sana kuona hili NMB mnalitekeleza kwa ufanisi hapa Nanenane,” alisema Bashungwa.

 

Hata hivyo Waziri huyo aliiomba benki hiyo kutoa elimu kama hiyo kwenye vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) ambavyo vimekuwa na matatizo ya ubadhilifu wa fedha za wanachama.

 

 “ Niwaombe NMB kuweza kuisadia serikali kutoa elimu hii kwa Amcos, baadhi yake bado zina matatizo kwenye usimamizi wa fedha, ingawa serikali tumeendelea kupambana nalo lakini elimu hii ni muhimu sana kwao,” alisema Bashungwa.

 

Kwa upande wake Meneja wa Benki hiyo Kanda ya Magharibi Sospeter Magesse, alisema kuwa benki hiyo imeweza kutoa kiasi cha sh. Bilioni 161 kwenye mazao ya Tumbaku, Kahawa na Pamba tangu mwanzoni mwa mwaka katika kanda hiyo.

 

Magesse alisema kuwa kiasi hicho cha pesa kimepelekwa kwenye mazao hayo kama mkopo ambapo wanufaika wakuu ni wakulima kupitia vyama vyao vya msingi (Amcos) takribani 700.

Tuesday, August 4, 2020

WAZIRI WA KILIMO JAPHET HASUNGA AONGEZA SIKU MBILI MAONESHO YA NANENANE

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati alipotembelea Banda la Chama Cha Wanawake wafanyabiashara Tanzania (TABWA) kwenye viwanja vya Maonesho ya wakulima (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika Nyakabindi Mkoani Simiyu Leo tarehe 4 Agosti 2020. (Picha Zote Na Matjias Canal, Wizara ya Kilimo)
 
Kulingana na kuchelewa kuanza kwa maadhimisho ya wakulima (Nanenane) Mwaka 2020 katika baadhi ya Kanda kutokana na ugonjwa wa homa ya Mapafu (Corona) serikali imetangaza kuongeza siku mbili za maadhimisho ya sherehe hizo.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea Banda la Chama Cha Wanawake wafanyabiashara Tanzania (TABWA) kwenye viwanja vya Maonesho ya wakulima (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika Nyakabindi Mkoani Simiyu.


Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati alipotembelea Banda la Chama Cha Wanawake wafanyabiashara Tanzania (TABWA) kwenye viwanja vya Maonesho ya wakulima (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika Nyakabindi Mkoani Simiyu Leo tarehe 4 Agosti 2020. Mwingine pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe Festo Kiswaga.

Amesema kuwa kulingana na mahitaji ya sherehe za wakulima kujifunza mbinu bora za kilimo wananchi ambao hawakupata fursa awali watatumia nafasi hiyo kujionea mbinu bora za kilimo, mifugo na uvuvi.

Amesema kuwa malengo makubwa ya sherehe hizo ni pamoja na kuwaunganisha wakulima, wafugaji, wavuvi na wanaushirika kusherehekea kwa pamoja ikiwa ni pamoja na kuonesha teknolojia ya zana bora za kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Kadhalika Waziri Hasunga amesema kuwa maonesho hayo yanatoa fursa ya kuwakutanisha wakulima, wavuvi na wafugaji na watoa huduma za fedha, bima, mawasiliano, taasisi za umma na binafsi.


Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari wakati alipotembelea Banda la Chama Cha Wanawake wafanyabiashara Tanzania (TABWA) kwenye viwanja vya Maonesho ya wakulima (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika Nyakabindi Mkoani Simiyu Leo tarehe 4 Agosti 2020. Mwingine pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe Festo Kiswaga.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu


Maonesho ya sherehe hizo yanafanyika katika kanda mbalimbali ikiwemo kanda ya Mwanza, Tabora, Simiyu, Mbeya, Dodoma, Morogoro, Arusha na Lindi

Katika maonesho hayo wakulima, wafugaji na wavuvi wanahamasishwa kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambapo wametakiwa kuchagua viongozi bora wenye uwezo wa kuendeleza kilimo.

“Maonesho hayo yanachagizwa na Kauli mbiu isemayo “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Chagua Viongozi Bora 2020” hivyo Wakulima, wafugaji na wavuvi nchini wapo tayari kwa Uchaguzi Mkuu na kutokana na mafanikio ambayo serikali ya Awamu ya Tano imepata katika sekta hizi, watakipatia Chama cha Mapinduzi ushindi mnono" Amesisitiza Waziri Hasunga


Monday, August 3, 2020

WAZIRI KAIRUKI AHIMIZA MATUMIZI YA MITANDAO YA KIJAMII KUFIKISHA TAARIFA ZA FEDHA NA UCHUMI KWA WANANCHI

Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Simiyu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki amehimiza kutumia lugha rahisi na mitandao ya kijamii kufikisha taarifa za masuala ya uchumi na fedha kwa wananchi.

Rai hiyo ameitoa alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki, akizungumza jambo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa, viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.


Mhe. Kairuki alisema kuwa ni vema Kampuni za simu za mikononi, tovuti na mitandao mingine ya kijamii ikatumika kupeleka toleo la Bajeti ya Wananchi kulingana na mahitaji husika ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Pia ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kusimamia taasisi za umma kuhakikisha zinatoa fursa kwa makundi maalum kushiriki katika zabuni za umma kama ambavyo sheria ya ununuzi wa umma inavyoeleza.

Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana wametakiwa kuongeza kampuni zilizo jiorodhesha kwenye Soko la Hisa kutoka kampuni 27 ili idadi hiyo ilingane na idadi ya kampuni zilizosajiliwa kwenye Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni-BRELA, zinazofikia zaidi ya elfu nane ili sekta ya masoko ya mitaji na dhamana yawe chachu ya kukuza uchumi wa nchi.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki (kulia), akiangalia machapisho mbalimbali kuhusu Deni la Serikali, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa, viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

Ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kazi nzuri ya kuandaa mipango ya kitaifa na usimamizi wa Sera za Bajeti na Fedha na kuwataka wataalam wa Wizara hiyo kuongeza juhudi zaidi ili kuiwezesha nchi kufanikisha malengo yake ya kuwahudumia wananchi wake.

Akimwongoza kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango katika Viwanja vya Nyakabindi, Bariadi, mkoani Simiyu, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara hiyo, Bw. Benny Mwaipaja, alimweleza Waziri Mheshimiwa Angellah Kairuki, kwamba Wizara ya Fedha na Mipango inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika kukuza pato la Taifa.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki, (kulia) akisoma chapisho la Bajeti ya Wananchi alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

Aidha alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imefuta kodi zenye kero zipatazo 105 katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza tija kwa wakulima na kuwawezesha kuzalisha mazao kwa wingi.

Aidha alisema kupitia taasisi zake za Wizara imetoa mchango mkubwa katika kukuza masuala ya ushirika na mikopo kwa wananchi ambapo amesema Taasisi yake ya Self Microfinance pekee, imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 36.3 kwa vikundi vya wajasiliamali nchini kote.


Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) Bw. Mcharo Mrutu (kulia) akielezea mchakato wa Zabuni za Umma wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki (kushoto), alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu, katikati ni Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga.

Bw. Mwaipaja alibainisha kuwa taasisi za elimu ya juu zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango kikiwemo Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) zimetoa mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa tafiti zinazofanywa na vyuo hivyo zinakidhi mahitaji ya kuisaidia jamii hususani katika kuandaa maandiko ya miradi pamoja na huduma za ushauri.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mheshimiwa Angellah Kairuki, alikuwa amemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, kwenye siku ya Ushirika, wakati wa Maonesho ya siku ya Wakulima Nanenane katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki (katikati), Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa, viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.

WAZIRI ANGELLAH KAIRUKI AUPONGEZA MFUKO WA FIDIA KWA WAFANYAKAZI WCF


Na mwandishi wetu, Simiyu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kutokana na huduma ambazo imekuwa ikitoa kwa wafanyakazi walioumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi.

Waziri Kairuki ametoa pongezi hizo jana (leo Agosti 3, 2020) wakati alipotembelea katika banda la Mfuko huo kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi nje kidogo ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

Waziri Kairuki alitoa pongezi hizo baada ya kupata maelezo ya shughuli za Mfuko yaliyokuwa yakitolewa na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko huo, Sebera Fulgence ambapo Waziri alivutiwa na majibu ya namna fidia inavyolipwa kwa mfanyakazi aliyeumia au kufariki kutokana na kazi.

“Mwisho wa siku mtu amepata ulemavu wa kudumu angalau consolation (faraja) anayopata ni kuona wanae wanaendelea vizuri au kama amefariki walau fidia isaidie watoto na mjane pia, lengo la serikali ni ku- support for real, ninawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayofanya.” Alisema Waziri Kairuki ambaye alikuwa amefuatana na Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga.

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi unashiriki katika maonesho hayo ili kukutana na wadau wote na wananchi kwa ujumla wakiwemo wafanyakazi kutoka sekta ya Umma na Binafsi

Kauli mbiu ya mwaka huu ya maonesho hayo yanayofanyika mkoani Simiyu kwa mwaka wa tatu mfululizo ni “Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020.”.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia uwekezaji Angellah Kairuki (wapili kushoto), akifuatana na Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (wa kwanza kushoto), akizungumza jambo wakati alipotembelea banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kwenye viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani Simiyu jana. Wapili Kulia ni Afisa Uhusiano Mwandamizi wa WCF, Sebera Fulgence akiwa na Afisa kutoka ofisi ya utawala Neema Mushi. 

 Afisa kutoka ofisi ya utawala WCF, Neema Mushi.
 Wananchi wakipata maelezo kuhusu masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi kwenye banda la WCF viwanja vya Nyakabindi.
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa WCF, Sebera Fulgence (kulia), akimfafanulia jambo mfanyakazi huyu aliyetembelea banda la WCF viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu Agosti 3, 2020.

RC KUNENGE AKABIDHIWA RASMI OFISI LEO

 Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Abubakar Kunenge (kushoto) akipokea sehemu ya vitendea kazi kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda, katika hafla fupi ya mahabidiano ya ofisi yaliyofanyika leo jijini Dar es salaam. 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Abubakar Kunenge (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es salaam leo, baada ya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Mtangulizi wake, Paul Makonda.

SHIRIKA LA MIKO YETU LATAMBULISHA MRADI WA “MSICHANA NI TAI”

 Shirika la Mikono Yetu ambalo limejikiza kuwawezesha wasichana kielimu na kiuchumi limetambulisha rasmi mradi wake wa "Msichana Ni Tai" kwa lengo la kuwajengea uwezo wasichana kutimiza ndoto zao.

Akizungumza kwenye utambulishoi wa mradi huo, Mkurugenzi wa Shirika hilo, Maimuna Kanyamala alisema jumla ya wasichana 300 kutoka Kata ya Buswelu  wilayani Ilemela watajengewa uwezo kupitia simulizi za wanawake waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo siasa na uongozi.

Alisema baada ya wasichana hao pamoja na wazazi wao kujengewa uwezo, watakuwa chachu ya mabadiliko kwa wasichana wengine na hivyo kuleta mabadiliko katika jamii tofauti na ilivyo sasa ambapo wasichana wanapitia changamoto kadhaa za usawa katika kutimiza ndoto zao ikilinganishwa na wavulana.
"Dhana ya Msichana ni Tai inatokana na moja ya hotuba za Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere aliyewahi kusema "mwanamke ni tai, si kuku" akimaanisha wanawake wana uwezo mkubwa wa kutimiza malengo yao kama tai anavyoweza kupaa umbali mrefu na si kuku ambaye anafugwa ndani akisubiri kuletewa chakula" alibainisha Afisa Mradi kutoka Shirika la Mikono Yetu, Halima Juma.
Kwa sasa mradi wa "Msichana Ni Tai" unawashirika wasichana 300 walio nje ya shule pamoja na wazazi wao katika Kata ya Buswelu wilayani Ilemela ukitarajiwa kudumu kwa muda wa miaka mitatu baada ya mradi wa majaribio uliozinduliwa mwaka 2018 kufanikiwa.
Tazama video hapa chini

Sunday, August 2, 2020

WAZIRI HASUNGA ATOA SIKU 14 KWA MKURUGENZI WA BODI YA NAFAKA NA MAZAO MCHANGANYIKO KUKAMILISHA MALIPO YA WAKULIMA WA KOROSHO

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akikagua bidhaa zinazozalishwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko wakati alipotembelea na kukagua ufanisi wa kinu cha kukoboa nafaka wakati akiwa katika ziara ya kikazi Jijini Arusha hivi karibuni.
Muonekano wa vihenge vya kuhifadhia nafaka vya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Jijini Arusha pamoja na baadhi ya ofisi zikiwa katika uchakavu 
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akizungumza na Meneja wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Kanda ya Arusha Ndg Idd Mkomalasa wakati alipotembelea kukagua bidhaa zinazozalishwa na Bodi hiyo akiwa katika ziara ya kikazi Jijini Arusha hivi karibuni.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akiongozana na Meneja wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Kanda ya Arusha Ndg Idd Mkomalasa wakati alipotembelea CPB kukagua bidhaa zinazozalishwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko wakati alipotembelea na kukagua ufanisi wa kinu cha kukoboa nafaka wakati akiwa katika ziara ya kikazi Jijini Arusha hivi karibuni.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ametoa siku 14 kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko Dkt Anslem Moshi kukamilisha malipo ya wakulima wote waliouza korosho msimu wa mwaka 2018/2019.

Waziri Hasunga ametoa agizo hilo wakati alipotembelea na kukagua shughuli za utendaji kazi zinazofanywa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Jijini Arusha.

Amesema kuwa Bodi hiyo ilipewa dhamana la kununua korosho mwaka 2018 kwa niaba ya serikali na tayari serikali imeshatoa fedha zote kwa ajili ya wakulima lakini bado CPB haijakamilisha malipo hivyo ni lazima malipo yakamilike ndani ya siku hizo.

“Ndani ya siku 14 sitaki kusikia malalamiko ya wakulima lazima wakulima wote wawe wamelipwa fedha zao haraka iwezekanavyo” Alisisitiza

Katika ziara hiyo pia Waziri Hasunga amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na mazao mchanganyiko kuwasilisha haraka mpango kazi wa namna viwanda hivyo vitakavyofanya kazi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa zitakazohitajika na wateja na kukidhi matarajio ya serikali ikiwa ni pamoja na kuainisha idadi ya watumishi wanaohitajika.

Hasunga ameiagiza kampuni ya Monaban ambayo ilikuwa imekodisha kiwanda hicho kutekeleza maagizo ya serikali yaliyotolewa mwaka jana ya kuhamisha mali zao zote zilizopo katika eneo hilo la serikali kwani kesi mahakamani na notisi ilishaisha.

Akiwa kiwandani hapo Waziri Hasunga amebaini uchakavu wa mitambo iliyopo pamoja na uchache wa watumishi wanaofanya kazi katika kiwanda hicho hivyo ameagiza kufanyika ukarabati wa majengo hayo kuanzia mwezi Agosti badala ya Octoba kwa taasisi hiyo ilivyopanga.

“Tukisubiri mpaka mwezi wa kumi tutakuwa tumechelewa kwa kuwa mvua zitaanza kunyesha jambo ambalo litapelekea kushindikana kufanyika ukarabati” Amesema

Amesema kuwa Lengo la serikali ni kufufua viwanda kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao ya nafaka nchini ili kuzalisha bidhaa mbalimbali kama unga N,k na kuuza katika masoko ya ushindani ndani na nje ya nchi.


ASDP II IKISIMAMIWA IPASAVYO TANZANIA ITAZIDI KUPAA KIUCHUMI

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu  tarehe 1 Agosti 2020. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Serikali Imesema kuwa endapo Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) itatekelezwa kama ilivyopangwa, Tanzania itakuwa kiuchumi zaidi ya sasa.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameyasema hayo leo tarehe 1 Agosti 2020 mbele ya mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu.

"Tunayo furaha na tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha Nchi yetu Mwaka huu kuingia kati ya nchi zenye uchumi wa kati mapema kabla ya lengo lililokuwa limewekwa yaani Mwaka 2025. Jitihada hizo zimechangiwa kwa Sehemu kubwa na wakulima, wafugaji na wavuvi wa nchi yetu kwa kufanya kazi kwa bidii" Amesema

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga  wakikagua mabanda ya maonesho ya Mifugo, Uvuvi na Kilimo kabla ya uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu tarehe 1 Agosti 2020.

Waziri Hasunga amemuhakikishia Makamu Rais kuwa Wizara za Kisekta zimejipanga kuhakikisha panakuwepo na upatikanaji wa uhakika wa malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu vya ndani jambo litakaloimarisha uwezekano wa viwanda vya ndani kuwa na uwezo wa kuchaka Mazao wakati wote.

Kadhalika amesema kuwa Wizara ya Kilimo imeendelea kutekeleza maeneo ya kipaumbele ya kuongeza uzalishaji na tija kwenye kilimo kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, udhibiti wa visumbufu, matumizi ya zana bora za kilimo na huduma za ugani; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji; ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo na masoko; kufanya utafiti wa kilimo na kuzalisha teknolojia kwa mazao ya mahindi, muhogo, ngano, michikichi, ufuta, alizeti, pamba na mpunga.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akionyesha vitabu vya Mwongozo wa Kitaifa wa Uongezaji virutubisho Kibiolojia katika mazao ya chakula wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu leo tarehe 1 Agosti 2020. Wengine pichani ni Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga (Kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka (Kulia).

Ameitaja Mikakati mingine  ambayo Wizara inaendelea nayo kuwa ni pamoja na kuhakikisha mbolea zinapatikana kwa wingi, kwa bei nafuu na kwa wakati, Pamoja na kuhakikisha kuwa inafugwa mifugo kitaalam zaidi ili kupunguza mifugo kuhamahama kwa ajili ya kutafuta malisho na maji. 

Hasunga amesema kuwa Serikali kupitia Wizara za Sekta ya Kilimo imedhamiria kuboresha zaidi sekta ya uvuvi ili kuongeza uzalishaji na tija, ikiwa ni pamoja na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa. Aidha, tumejipanga kuhakikisha kuwa kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) sekta ya uvuvi inaongeza ufugaji wa samaki wenye tija na endelevu katika mabwawa ili tuweze kuzalisha samaki wengi zaidi na kuondoa kabisa uvuvi haramu.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe adam Malima wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu  tarehe 1 Agosti 2020.

"Wizara inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele na miongozo ya Kitaifa ili kilimo kichangie kutoa malighafi za viwanda. Amesisitiza

Pia ameyataja maeneo machache, maalum na ya kimkakati katika kilimo ambayo yanafanyiwa maboresho ili kuimarisha usimamizi wa kilimo na kuwapatia Wakulima huduma kwa urahisi zaidi ambayo ni pamoja na usajili wa wakulima, mapitio ya sera ya kilimo kwa lengo la uanzishaji wa Sheria ya Kilimo, uanzishwaji wa bima ya mazao, uimarishaji wa masoko ya mazao ya kilimo, uimarishaji wa mfumo wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo sahihi na kwa wakati.

Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya uzinduzi wa maadhimisho ya sikukuu ya wakulima Nanenane kitaifa Mkoani Simiyu tarehe 1 Agosti 2020.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu

Kauli mbiu katika maonesho ya mwaka huu inasema “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Chagua Viongozi Bora 2020. Wakulima, wafugaji na wavuvi wa nchi hii wapo tayari kwa Uchaguzi na kupitia kwako wanatoa salamu zao kuwa kwa mafanikio amabayo serikali ya Awamu ya Tano imepata katika sekta hizi, Ushindi kwa Chama Tawala upo pale pale na utakuwa wa kishindo kikubwa.

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga Kupitia maadhimisho hayo amesema kuwa Wakulima, Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika na Wadau wengine wanapata nafasi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu ili hatmae sekta hizi ziweze kuongeza uzalishaji na tija zaidi.  Uwekezaji katika sekta ya kilimo ukiwa wenye tija uzalishaji utaongezeka katika eneo dogo na upatikanaji wa malighafi za kutosha utakuwa wa uhakika zaidi.

SUA IMEJIANDAA KUFIKISHA MATOKEO YA TAFITI KWA WAKULIMA


 Profesa Gerald Misinzo (kulia) akitoa maelekezo kuhusu udhibiti wa panya kwa kutumia mkojo wa panya katika banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wakati wa Maoneshoya NaneNane, Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

 Mtaalam wa Maabara ya Udongo katika Idara ya Sayansi za Udongo na Jiolojia (SUA), Stevenson Pelegy akitoa elimu ya jinsi ya kupima udongo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dutwa, mkoani Simiyu.

Baadhi ya Washiriki kutoka SUA katika Maonesho ya NaneNane mkoani Simiyu wakiwa katika picha ya pamoja katika banda.


Na Mariam Mwayela, Simiyu

NAIBU Makamu   Mkuu  wa Utawala wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Maulid Walad Mwatawala amesema SUaina Mkakati wa kuhakikisha matokeo ya Tafiti zote zinazofanywa na watafiti zinawafikiakwa wakati.

Akizungumzia kuhusu maelekezo ya Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alipokuwa akifungua Maonesho ya NaneNane Kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu Prof. Mwatawala alimesema kuwa SUA imeanzisha stashahada mpya ya Tejnolojia na Uzalishaji wa Mbegu (Diploma in Seed Technology and Production) ambayo ni maalumu kwa Maafisa Ugani ili kuwaongezea uwezo katika masuala ya mbegu. 

“Stashahada hii itasaidia Mafisa Ugani kusambaza matokeo ya tafiti mbalimbali kwa wakulima ili kuweza kusaidia wakulima hao kulima kilimo chenye tija”, alisema Prof.Mwatawala.

Aidha aliongeza kuwa mbali na kuanzishwa kwa stashahada hiyo inayotarajiwa kuanza mwaka huu pia SUA imekuwa ikifanya mafunzo mbalimbali kuhusu mbegu kwa Maafisa ugani na wakulima kutoka katika Halmashauri na Taasisi mbalimbali nchini.

“Mpakasasa Halmashauri na Asasi au Taasisi za binafsi zimekuwa zikileta Maafisa Ugani na wakulima kwa ajili ya mafunzo mbalimbali juu ya ubebeshaji miche ya matunda na jinsi ya kusimamia kitalu cha miche na Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) imekuwa ikiandaa mafunzo mbalimbali kutokana na uhitaji na kwa sasa chuo kiko katika maandalizi ya kuandaa kalenda ya Mafunzo kwa mwaka mzima itakayokuwa inasambazwa kwa wadau mbalimbali ili kuweza kuja na kujifunza.” alisema Prof.Mwatawala.

Kuhusu suala la kutumia kilimo cha kunyunyiza na kuachana na Kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza gharama za kutengeneza miundombinu Prof. Mwatawala alisema SUA ina Shahada ya Masuala ya usimamiaji wa Rasilimali Maji hivyo kuna haja ya kuangalia ni namna gani watabadilisha ili kuweza kusaidia kutoka katika kilimo hicho cha umwagiliaji.

Mapema juzi mkoani Simiyu Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan aliwaelekeza watafiti wa Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kuhakikisha wanasambaza matokeo ya tafiti wanazofanya kwa Maafisa Ugani na wadau ili ziweze kuwafikia wakulima.

“Naelekeza watafiti watoe matokeo ya tafiti zao kwa maafisa Ugani ili ziweze kuwafikia wakulima na kunufaika na tafiti hizo,” alisema Mama Samia

Aidha ameiagiza Wizara ya Kilimo kutoa elimu ya utunzaji na uendeshaji endelevu wa miundombinu ya umwagiliaji hususan kujikita katika unyunyizaji na si umwagiliaji ili kupunguza gharama kubwa inayohitajika katika ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji pamoja na kuelekeza kila mkoa, wilaya na Halmashauri kutekeleza agizo la kupanda miti na kuhakikisha inamea.

Chuo Kikuu cha Sokoine kinashiriki Maonesho ya NaneNane Kanda ya Mashariki mkoani Morogoro na Kitaifa mkoani Simiyu ambapo Kauli Mbiu ya mwaka huu ni “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo naUvuvi chagua Viongozi Bora 2020”.

TANESCO: WANANCHI CHANGAMKIENI FURSA FURSA ZA UMEME WA KUTOSHA KUJILETEA MAENDELEO


NA MWANDISHI WETU, NYAKABINDI

Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) limeendelea kuwahimiza wananchi wote wakiwemo, wakulima, wafugaji na wavuvi kutumia fursa za uwepo wa umeme wa kutosha na wa uhakika ili kujiletea maendeleo.

Hayo yamesemwa Agosti 2, 2020 na Meneja wa TANESCO mkoa wa Simiyu, Eng. Khadija Abdallahmed kwenye banda la TANESCO katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi nje kidogo ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

“Naomba kutoa wito kwa watanzania wote kwa ujumla wachangamkie hizi fursa za umeme na maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi Tanzania nzima, umeme upo wa kutosha Tanzania nzima, TANESCO tupo tunaaangaza maisha.” Alisisitiza Eng. Khadija

Alisema TANESCO inashiriki maonyesho haya kwa vile wao ni wadau wakubwa wa shughuli za kilimo, mifugo pamoja na uvuvi na kwa huduma ya umeme itolewayo na shirika hilo ni sehemu ya kufanikisha maonesho hayo.

Aliwakaribisha wananchi wote wanaopata fursa ya kufika kwenye viwanja vya Nyakabindi yanakofanyika maonesho hayo kutembeela katika banda la TANESCO kwani watafaidika na kupata elimu kuhusu matumizi bora na sahihi ya umeme.

“Lakini wananchi watakaofika kwenye banda letu watakutana na mtaalamu mbobezi ambaye atawaeleza kuhusu mradi mkubwaj wa kimkakati wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme Julius Nyerere (JNHPP 2115) kwenye bonde la mto Rufiji.” Alisema.

 Eng.Mwanji Y Mhaka, Mhandisi mradi wa umeme wa maji Julius Nyerere (JNHPP-2115) akitoa maelezo kwa wananchi waliofika kwenye banda la TANESCO kwenye maonesho ya Nanenane kwenye viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi mkoani Simiyu Agosti 2, 2020.
 Elimu kuhusu matumizi bora ya umeme ikitolewa na mtaalamu huyu wa TANESCO kwa wakazi wa mji wa Bariadi mkoani Simiyu waliofika katika banda la Shirika hilo
 Wahudumu wa TANESCO wakiwahudumia wananchi waliofika kwenye banda la shirika hilo katika maonesho ya Nanenane viwanja vya Nyakabindi nje kidogo ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu.
 Wahudumu wa TANESCO wakiwahudumia wananchi waliofika kwenye banda la shirika hilo katika maonesho ya Nanenane viwanja vya Nyakabindi nje kidogo ya mji wa Bariadi mkoani Simiyu.
 Meneja wa TANESCO mkoa wa Simiyu, Eng. Khadija Abdallahmed(Watano kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na timu ya wafanyakazi wa TANESCO katika banda la shirika hilo 
Wakubwa kwa watoto wakielimishwa kuhusu madhara yanayoweza kutokea endapo mtu atashika waya wa umeme uliokatika