Matokeo chanyA+ online




Wednesday, May 5, 2021

RAIS WA ZANZIBAR DKT HUSSEIN ALI MWINYI AFUTARISHA WANANCHI MKOA WA KUSINI PEMBA



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika mwendelezo wa ziara za kufutarisha Zanzibar, tarehe  5 Mei 2021 amefutarisha Mkoa wa Kusini katika viwanja vya Tibirizi akiwa na Mke wake Mama Mariam Mwinyi Pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Mhe. Mattar Zahro Masoud.

 

Rais Mwinyi alisema “Niwashukuru nyote mliopokea mwaliko wangu na kujumuika na mimi, pia lengo na madhumuni ni kujumuika na wananchi hususan wenye mahitaji maalum” (Picha na Ikulu Zanzibar)













 

SERIKALI ITAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA KATIKA SEKTA YA HABARI


Na. Beatrice Sanga - MAELEZO

Sekta ya Habari na Utangazaji ni moja ya sekta inayotoa huduma kwa jamii ya watu wengi nchini ambayo ni haki ya msingi ya raia kama inavyoonekana kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Aidha kutoa na kupokea habari kunatambuliwa duniani kote kuwa ni moja ya haki za binadamu ambapo Umoja wa Mataifa, na umoja wa afrika zina matamko rasmi ambayo Serikali imeridhia kuhusu haki ya kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote. haki hii kama zilivyo haki nyingine zote, hutolewa kwa kuzingatia wajibu wa kila raia kwa jamii na uhuru binafsi wa binadamu

Mei 3 kila mwaka Tanzania pamoja na nchi nyingine Ulimwenguni huadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari tangu Umoja wa Mataifa ulipoidhinisha siku hiyo ikiwa na lengo la kuwapatia watu taarifa na elimu za kujenga demokrasia na maendeleo katika sekta ya habari

Mwaka huu 2021 kilele cha maadhimisho haya nchini Tanzania yamefanyika Jijini Arusha na kujumuisha washiriki kutoka sekta ya habari inayojumuisha Serikali kupitia Idara ya Habari MAELEZO, vyombo vya habari binafsi na vya Serikali, Mashirika ya Kimataifa, wadau wa maendeleo na asasi zisizo za kiserikali na wadau wengine mbalimbali wameshiriki kwa kufanya midahalo mikubwa pamoja na waandishi wa habari kutembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kutangaza vivutio vyetu na kuutangaza urithi wa dunia na kwa madhumuni ya kuvutia watalii.

Mwaka huu maadhimisho haya yamekuja na kauli mbiu ya "Habari kwa Manufaa ya Umma" ambayo inasaidia kujua namna ambavyo habari zinamanufaa kwa umma,ikiwemo haki ya kikatiba ya kupata habari na kwa mwaka huu Jamhuri ya muungano wa tanzania katika siku ya uhuru wa vyombo vya habari imejikita katika maeneo makuu matano ya vipaumbele ambavyo ni Uhuru wa vyombo vya habari vinavyofaa, kuendeleza nguvu kazi, mazingira mazuri ya sheria na sera, ikiwa ni pamoja na hali bora ya kazi, ulinzi na usalama wa waandishi na kujua kufanya kazi za kiuandishi, ikiwa ni pamoja na uelewa wa matumizi ya kidijitali

Katika kuhakikisha habari zinanufaisha umma Serikali imedhamiria kuweka mifumo ndani ya vyombo vya habari inayowalazimisha kuleta matokeo chanya hasa ya matumizi ya sheria hususani kwa wahariri na watekeleza sera kama Maafisa Utumishi, ikiwa ni sambamba na kupitia upya sera ya vyombo vya habari ya mwaka 2003.

katika hotuba iliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa alisema kuwa, Serikali itaboresha mazingira katika sekta ya habari ili Waandishi wa Habari watekeleze majukumu yao bila hofu, na kwa kujiamini.

"Serikali itaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya habari ili muweze kutekeleza majukumu yenu bila hofu, na kwa kujiamini huku mkizingatia sheria, kanuni, maadili na weledi ili wananchi waweze kupata habari sahihi kwa ajili ya manufaa na maendeleo yao,"amesema Bashungwa

Waziri Bashungwa alisema ili kuweza kuendana na lengo namba 16 la Maendeleo Endelevu (SDG16), Tanzania itahitaji kuwa na ukusanyaji wa fedha wenye tija na wa kudumu, takwimu zenye ubora zinazozalishwa na kushirikishwa kwa umma, ambapo matokeo yake yanaweza kufanyiwa majaribio na kupimwa maendeleo yake.

"Ni muhimu kuwa na mpango wa maendeleo ili kuviwezeshe vyombo vya habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi. Waandishi wa Habari wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu mbalimbali zikiwemo za matunzo, na mishahara midogo kwa wafanyakazi, mapato yasiyotosheleza, na kukosa kinga bima ya afya kwa waandishi pamoja na wasaidizi wao. Mambo haya yamekuwa ni tatizo na kuleta wasiwasi kwa wanahabari," amesema Bashungwa.

Aliendelea kueleza kuwa, Serikali inahimiza wadau wote wa habari, kuhakikisha wanaweka utaratibu utakaowezesha kufanya ufuatiliaji, na uwajibikaji katika kutekeleza sera na sheria za nchi, pamoja na miongozo kwa umma na jamii kwa ujumla. Miongozo hiyo izingatie kuwepo kwa mazingira na hali bora ya kazi, ulinzi na usalama wa waandishi, kujua kufanya kazi za kiuandishi, ikiwa ni pamoja na uelewa wa matumizi ya kijiditali.

"Serikali ya awamu ya sita inathamini na kutambua uhuru wa vyombo vya habari na katika muktadha huo hivi karibuni Serikali ilivifungulia vyombo vya habari vya kielektroniki vya online TV vilivyokuwa vimefungiwa kwa makosa mbalimbali ili kuhakikisha kuwa vinafanya kazi kwa uhuru na kukuza ajira za vijana nchini,"amesema Bashungwa.

katika kuonesha uhuru wa vyombo vya habari nchini, Waziri Bashungwa alieleza kua Tanzania ni miongozi mwa nchi chache zenye vyombo vingi vya habari Barani Afrika ambapo mpaka sasa kuna jumla ya Magazeti 246, Televisheni 53, Redio 194, Redio za Mtandaoni (Online Radio) 23, Blogs 120 na Televishenio Mtandao (Online TV) 440. ambapo ishara kuwa nchi yetu inathamini na kuenzi vyombo na taaluma ya habari, na kusema Serikali iko tayari kushirikiana kuhakikisha na kunakuwepo na uwazi katika upatikanaji wa habari kwa Watoa Huduma ya Mitandao, kama sehemu muhimu ya habari kwa manufaa ya umma.

“Ni vyema mkatambua kuwa jukumu lenu kubwa kama washiriki katika mjadala huu ni kuhakikisha kuwa mapendekezo mtakayotoa yataleta mafanikio. Mafanikio hayo yatapatikana iwapo wadau wote tutashirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mapendekezo na maazimio. Kwa upande wa Serikali ya Awamu ya Sita (06) inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, tunawahakikishia ushirikiano mkubwa.” Amesema Bashungwa


Pia Waziri ametoa wito kwa Viongozi mbalimbali ndani ya Serikali kuhakikisha anaondoa vikwazo na kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari pale wanapohitaji taarifa muhimu kwa Manufaa ya Umma na maslahi ya Taifa letu kwa ujumla.


Kuhusu changamoto Waziri Bashungwa amesema anazitambua changamoto nyingi zinazowakumba aandishi wa habari wakati wa kutekeleza majukumu ya kila siku, zikiwemo kunyimwa taarifa bila sababu ya msingi hata kama mwandishi anakuwa na kitambulisho kilichotolewa na Serikali kumtambulisha kama ni mwandishi wa habari. na kuahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan inazitambua changamoto hizo na itaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya habari ili kuwawezesha kutekeleza majukumu ya kiuandishi bila hofu, na kwa kujiamini na kwa kuzingatia sheria, kanuni, maadili na weledi ili wananchi waweze kupata habari sahihi kwa ajili ya manufaa na maendeleo ya Taifa.

Sambamba na hilo, waziri bashunga ametoa pongezi nyingi kwa Shirika la Umoja amataifa , elimu sayansi na utamaduni (UNESCO) kwa kuendelea kuiunga mkono na kuendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuendeleza uchumi a nchi yetu na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo"kwa niaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano a Tanzania, ninapenda kuwapongeza na kuwashukuru UNESCO ka kushirikiana na Serikali katika kuendeleza uchumi wa nchi yetu. niwapongeze kwa kusaidia kufanikisha maadhimisho haya, tangu mwanzo hadi mwisho. UNESCO mmekuwa mkiipatia Tanzania misaada ya kiufundi, kwa zaidi ya miaka arobaini na saba (47) sasa. Hivyo sisi kama serikali, hatuna budi kuapongeza, na kuaahidi ushirikiano mkubwa kutoka kwetu" amesema Bashungwa.

TUTASIMAMA NA WAKUNGA KUHAKIKISHA UZAZI UNAKUWA BARAKA, FURAHA TANZANIA – DK. GWAJIMA


 Na. Catherine Sungura-Dodoma


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima amewahakikishia wakunga kwamba Serikali itaendelea kusimama nao vema ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo katika kusimamia akina mama kujifungua salama.

Dk. Gwajima ametoa pongezi hizo mapema leo alipozungumza kupitia kipindi kimoja kinachorushwa na Kituo cha Radio  hapa nchni kilichokuwa na mada kuhusu Siku ya Wakunga Duniani ambayo hufanyika Mei 5, kila mwaka.

Amewapongeza wakunga na wadau wote waliofanikisha maadhimisho ya siku hiyo nchini hususan UNFPA (Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Idadi ya Watu).

“UNFPA wametuunga mkono siku zote kuhakikisha tunakwenda vizuri na agenda hii ambayo wao wanaisimamia vema kuhusu idadi ya watu duniani  na maisha bora ikiwemo masuala ya afya.

“Siku ya leo tutakuwa tunaelekeza nguvu nyingi kuangalia vipaumbele vyote vya Umoja wa Mataifa (UN) na malengo yake 17 (SDGs), lengo namba tatu linahusu watu wa afya na ustawi wa jamii yetu tunavyoihudumia.

Ameongeza “Wakunga wanafahamu siku ya leo kauli mbiu inaeleza tuongozwe na takwimu maana ndiyo eneo muhimu litatufanya tuweze kujipima kama tutafika hayo malengo ya 2030.

“Katika malengo haya ambayo tumejiwekea kwamba vifo vya uzazi vitokomezwe kabisa, isifikie kwamba mama anabeba ujauzito anakwenda kujifungua anapoteza maisha au mtoto anapoteza maisha.

“Mchezo huu unawahitaji wakunga, wao ndiyo Baraka ya kwanza kabisa ya kiumbe hai ambacho mungu amekileta duniani, nini jukumu letu tunatakiwa tuwasaidie, tuwajali, tuwaenzi, wawe na imani.

“Kwa sababu kama wakirudi nyuma kwenye hotuba ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Nchi, Samia Suluhu Hassan, alipokuja bungeni alisema kwamba mradi huu wa masuala ya kuboresha huduma za uzazi wajawazito, wazazi na watoto wasifariki ni mradi wake wa moyoni.

“Kama Rais amesema ni mradi wa moyoni na ameniamini mimi na kunipa dhamana kusimamia sekta hii mimi ndiyo nazama kabisa moyoni mwake kabisa mzima mzima,” amesisitiza.

Dk. Gwajima ameongeza “Kwa hiyo naunga na mheshimiwa Rais. kwamba na mimi mradi huu ni wa moyoni mwangu na nitahakikisha nasimama na wakunga.

“Kuhakikisha kwamba tunawekeza kuwahakikishia wana uwezo wa kitaaluma mahitaji, miundombinu wanayohitaji, dawa zote na wanafanya kazi zao vizuri kuhakikisha wanakuwa Baraka kwa mtoto huyu anayezaliwa mikononi mwao, wao wakiwa wanafungua njia ya maisha bora yenye afya na furaha kwa mtoto huyu ambaye ni Taifa la kesho,” amesema Dk. Gwajima.
 

RAIS SAMIA AHUTUBIA JUKWAA LA WAFANYABIASHARA WA TANZANIA NA KENYA JIJINI NAIROBI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama na mwenyeji wake Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta wakati nyimbo za Mataifa Mawili ya Tanzania na Kenya wakati zikipigwa mara baada ya kuwasili Ukumbini kwa ajili ya kuhutubia Jukwaa la Wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania lililofanyika Jijini Nairobi Kenya leo tarehe 05, Mei, 2021.





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya katika Kongamano hilo la Wafanyabiashara lililofanyika Jijini Nairobi Kenya leo tarehe 05, Mei, 2021.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipongezwa na Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta mara baada ya kuhutubia katika Jukwaa hilo la Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiagana na Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta mara baada ya kuhutubia katika Jukwaa hilo la Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika jijini Nairobi nchini Kenya.


Sehemu ya viongozi mbalimbali pamoja na Wafanyabiashara waliohudhuria Kongamano hilo jijini Nairobi. PICHA NA IKULU.
 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 05 Mei, 2021 amehutubia Bunge la Kenya lililojumuisha Bunge la Taifa na Bunge la Seneti ambapo ametoa wito kwa Wabunge hao kuchochea uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Kenya.

Mhe. Rais Samia ambaye anakuwa Rais wa pili wa Tanzania kuhutubia Bunge la Kenya akitanguliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewashukuru Maspika na Wabunge wa Kenya kwa kukubali awahutubie na amebainisha kuwa huo ni uthibitisho wa udugu, urafiki, ujirani na nia njema ya Wabunge na Mhe. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kukuza zaidi uhusiano uliopo na Tanzania.

Katika hotuba hiyo,  Rais Samia amesema haoni sababu ya Tanzania na Kenya kushindana bali anaona fursa ya kushirikiana zaidi katika uchumi kwa kuwa uhusiano wa nchi hizi ilioanza miaka 56 iliyopita sio wa hiari kutokana na kufungamanishwa uhusiano wa damu kwa jamii zilizopo pande zote, historia kutokana na kuwepo uhusiano hata kabla ya uhuru na jiografia kutokana na kuwa na mpaka mrefu na maeneo yenye rasilimali zilizoungana ikiwemo hifadhi na wanyama.

Ameahidi kuwa katika kipindi chake cha uongozi atahakikisha uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Kenya unaimarika zaidi na ametoa wito kwa viongozi na watumishi wa Serikali kuendana na kasi ya ushirikiano waliyonayo wananchi kwani hivi sasa hali inaonesha wananchi wa Tanzania na wananchi wa Kenya wanashirikiana zaidi ikilinganishwa na namna viongozi na wafanyakazi wa Serikali wanavyoshirikiana.

Pia, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendeleza miradi ya ushirikiano ikiwemo ujenzi wa barabara, ujenzi wa bomba la gesi la Dar es Salaam – Mombasa, ujenzi wa njia ya umeme ya kilovoti 400 kutoka Singida Tanzania kwenda Kenya, kukamilisha vituo vya huduma za pamoja mpakani (One Stop Border Post) na amesisitiza kuwa yeyote anayefikiria kuichonganisha Tanzania na Kenya ajue kuwa uhusiano wa nchi hizi ulikuwepo, upo na utakuwepo sana.

Amewataka Wabunge hao kuwaongoza wananchi katika kuimarisha uhusiano huo badala ya kuudhohofisha na kwamba hata yeye amefanya ziara hiyo ili kurekebisha maeneo yote ambayo yalikuwa yanalegalega jambo ambalo limefanikiwa sana baada ya mazungumzo yake na Mhe. Rais Kenyatta.

“Kuongoza ni kuonesha njia sio kufunga njia” amesisitiza Mhe. Rais Samia na kubainisha kuwa pale kunapotokea tatizo kati ya pande hizi dawa iwe ni kulitatua badala ya kuliendeleza.

Kabla ya kuhutubia Bunge, Mhe. Rais Samia amekutana na wafanyabiashara wa Tanzania na Watanzania waishio Kenya (Diaspora) na amewaambia kuwa katika kipindi chake cha uongozi amedhamiria kukuza uchumi kwa haraka na hivyo ametoa changamoto kwa sekta binafsi kujipanga vizuri kutumia fursa mbalimbali ambazo Serikali ya Awamu ya Sita itazifungua na kuondoa vikwazo mbalimbali vya biashara.

Ametaja baadhi ya fursa hizo kuwa upanuzi wa huduma za bandari zitakazokidhi mahitaji na kwendana na kasi ya kukua kwa uchumi, kuanzishwa kwa maeneo maalum ya viwanda (industrial parks) yatakayozalisha bidhaa na kuajiri Watanzania wengi, kukuza na kuendeleza kilimo na amewaonya wale ambao wameshikilia maeneo makubwa ya mashamba lakini hawayaendelezi kuwa Serikali itayatwaa maeneo hayo na kuwapatia waliotayari kuzalisha mazao.

“Nataka kwenda faster, nataka kufuangua nchi, yeyote anayetaka kuwekeza aje awekeze yeye apate na sisi tupate, najua wawekezaji wengi watakuwa wa nje lakini nawaomba na nyie mchangamke na mtumie vizuri fursa za ndani zitakazojitokeza (local content)” amesisitiza Mhe. Rais Samia.

Mhe. Rais Samia ameitaka sekta binafsi ya Tanzania kumuunga mkono katika dhamira hiyo na amewaomba wafanyabiashara na wawekezaji waliowekeza nje ya Tanzania kurudi kuwekeza Tanzania kwani nyumbani kumenoga. Pia amewataka kuijulisha Serikali pale watakapoona jambo lolote halipo sawa zikiwemo sheria kandamizi ili zifanyiwe kazi.

Mhe. Rais Samia ameagwa na Mhe. Rais Kenyatta na amerejea Jijini Dodoma nchini Tanzania akitokea Jijini Nairobi nchini Kenya baada ya kumaliza Ziara Rasmi ya siku 2 nchini humo.


ROSTAM AZIZ AMWAGA MBOGA NCHINI KENYA ASEMA USHIRIKA WETU LAZIMA UNUFAIS...

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN NA RAIS UHURU KENYATTA WAFUNGUA KONGAMANO LA WA...

Monday, May 3, 2021

WAGONJWA SITA WENYE MATATIZO YA HITILAMU YA MFUMO WA UMEME WA MOYO WAPATA MATIBABU


 Wagonjwa sita wenye matatizo ya hitilamu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yao ya  moyo yanakwenda haraka kuliko kawaida  (Tachyarrhythmia’s) wamepata matibabu katika kambi maalum ya matibabu hayo iliyomalizika hivi karibuni  katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Kambi hiyo ya siku mbili ilifanywa na madaktari wa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mtaalamu mbobezi wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni mratibu wa kambi hiyo Dkt. Yona Gandye alisema katika hali ya kawaida moyo  hupiga kati ya mapigo 60 hadi 100 kwa dakika.

Dkt. Gandye alisema mtu akiwa na tatizo katika mfumo wa umeme wa moyo ambalo anaweza kulipata aidha kwa kuzaliwa nalo au athali ya ugonjwa linapelekea mfumo wa umeme wa moyo kubadili mapigo yake inaweza kuwa chini ya mapigo 60  kwa dakika au kuwa juu ya 100 kwa dakika.


 “Sababu mbalimbali zinaweza kuufanya moyo udunde kwa haraka kuliko kawaida hii ni pamoja na mtu kuzaliwa  na tatizo, kwa kurithi kutoka  kwa wazazi hata kama wao hawakuwa na dalili. Sababu ya pili ni ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, moyo kutanuka na  kuwa na misuli mikubwa ya moyo (Hypertrophy).

“Mgonjwa anakuja kliniki akiwa na dalili za moyo kushindwa kufanya kazi ambazo ni  miguu kuvimba, pumzi kubana, kushindwa kulala vizuri usiku. Ukimfanyia vipimo unakuta moyo wake umetanuka na umefika mahali umeme wake wa moyo haufanyi kazi vizuri”, alisema Dkt. Gandye.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo  Prof. Mervat Aboulmaaty kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri alisema amefurahi kuona taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefunga mtambo wa kisasa wa Cathlab ambao umeungaishwa na mtambo wa  Carto 3 System 3D &  mapping electrophysiology System wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na  kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme  wa moyo.

Prof. Mervat alisema, “Kufungwa kwa mashine hii ya kisasa na yenye teknlologia ya hali ya juu kutaweza kuokoa maisha ya watu wengi wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo nchini Tanzania”,.

Alisema katika katika kambi hiyo licha ya kutibu, wataalamu walibadilishana ujuzi wa jinsi ya kutibu wagonjwa wenye tatizo hilo la moyo unaokwenda kwa haraka.

Aliongeza kuwa kupitia chuo kikuu cha Ain Shams cha nchini Misri wanatoa elimu kwa njia ya mtandao kuhusu matibabu hayo ambapo madaktari wengi wa Afrika wakiwemo wa Tanzania wamekuwa wakishiriki.

“Hii inamaana kuwa baada ya miaka michache ijayo tutakuwa na madaktari wengi wenye utaalamu wa kutoa matibabu ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yake  yanakwenda haraka kuliko kawaida  na kuweza kuokoa maisha ya wagonjwa wenye matatizo haya”, alisema Prof. Shams ambaye pia ni mkufunzi katika chuo hicho.

Naye mtaalamu mbobezi wa magonjwa ya moyo  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Reuben Mutagaiwa ambaye alishiriki  katika kambi hiyo alisema waliandaa wagonjwa ambao walikuwa na  dalili za ugonjwa wa mfumo wa  umeme wa moyo baada ya kuwachunguza kwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Stress Electrocardiography – ECG) waligundulika kuwa na tatizo.

“Ili kuchunguza na kubaini zaidi kuna vipimo ambavyo vinafanyika kwa kitaalamu vinajulikana kama Electrophysiological (EP) studies & ablation ambapo mgonjwa anaingizwa katika  chumba cha upasuaji (Cathlab) kwa ajili ya uchunguzi wa mfumo wa umeme wa moyo (electrophysiology) unasisimua yale matatizo ambayo yalionekana  katika kipimo cha ECG (Induction of Arrhythmias) baada ya kuuleta umeme wa moyo ambao hauna upangilio unaweza kufahamu ni upande gani umeme huo unatoka na kuweza kuudhibiti”, alisema Dkt.Mutagaiwa.

Dkt. Mutagaiwa alisema baada ya kugundua kama  tatizo liko kwenye upande wa kushoto au wa kulia wa moyo kuna kifaa maalum kiitwacho  Ablator ambacho kinatoa joto na ukiliweka sehemu ambayo umeme wa moyo hauna mpangilio unatoka unaweza kumtibu mgonjwa kwa kuziunguza njia hizo.

“Kwa kawaida wagonjwa hawa walikuwa wanawekwa katika dawa za vidonge lakini dawa zinaukomo wake, hadi wanafanyiwa matibabu haya walishashindikana kwenye dawa hivyo basi matumizi ya dawa tuliyasimamisha  na kuwafanyia tiba hii”.

“Faida kubwa ya tiba hii  ni mgonjwa kupona  moja kwa moja na baadaye mgonjwa anashauriwa kutumia dawa na kuendelea na kliniki yake kama kawaida”, alisisitiza Dkt. Mutagaiwa.

Matibabu hayo yamefanyika kwa mara ya kwanza katika maabara ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo (Catheterization Laboratory - Cathlab) mpya ambapo mwanzoni mwa mwaka jana Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya kufunga mtambo huo ambao umeungaishwa na mtambo wa  Carto 3 System 3D &  mapping electrophysiology System  wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na  kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme  wa moyo.

Matibabu ya  tatizo la hitilamu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yake yanakwenda haraka kuliko kawaida  (Tachyarrhythmia’s) yalianza kutolewa hapa nchini mwaka 2019 ambapo hadi sasa wagonjwa 11 wameshapata matibabu.

WAZIRI MKUU MAJALIWA: TUTUMIE MWEZI WA RAMADHANI KUMUOMBA MWENYEZI MUNGU AENDELEE KUIBARIKI TANZANIA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasisiza waislam nchini watumie Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki Tainzania, viongozi na wananchi wake wadumishe amani na mshikamano.

 

Ameyasema hayo (Jumapili, Mei 2, 2021) katika Fainali za Mashindano ya 29 ya Kimataifa ya Qur’an yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo yahusisha washiriki 15 kutoka nchi 11.

 

Pia, Waziri Mkuu ametoa rai kwa waumini wa dini ya kiislam nchini waendelee kuyaishi mafundisho wanayoyapata katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwenye maisha yao ya kila siku.

 

 “Natambua mchango mkubwa wa waumini katika kuienzi na kuitunza amani kwa kufuata miongozo ya viongozi wetu kupitia mafundisho ya Qur’an ambayo hututaka kuepuka kuivuruga amani.”

 

Amesema amani ni matokeo ya msingi imara iliyoachwa na waasisi wa Taifa, hivyo hawana budi kuienzi na kuilinda kwa ajili ya maslahi na mustakabali wa nchi. “Mwitikio mkubwa tunaouona kwenye mashindano haya ni kielelezo cha amani, umoja na mshikamano tulionao.”

 

Pia, Waziri Mkuu amesema ni vema vijana hao waliohifadhi Qur’an wakaendelezwa kitaaluma katika fani zingine za elimu kwani uwepo wao ni muhimu katika kujenga jamii bora na yenye uadilifu.

 

Amesema si jambo rahisi kumuona mtaalamu aliyehifadhi qur’an akienda kinyume na maadili ya taaluma yake kwa sababu Qur’an pekee inatosha kumfanya mwanataaluma huyo aonyeke dhidi ya vitendo vinavyokwenda kinyume na uadilifu.

 

Waziri Mkuu ametoa wito kwa wadau mbalimbali waunge mkono juhudi zinazofanywa na taasisi mbalimbali za kuhifadhisha Qur’an nchini katika kujenga Taifa bora la vijana wenye maadili na kutoa wataalamu wa fani mbalimbali ambao wana hofu ya Mwenyezi Mungu katika mioyo yao.

 

Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zuber ametumia fursa hiyo kuwahamasisha waumini wa dini ya kiislam kujenga utamaduni wa kuhifadhi Qur’an kwa kuwa ndiyo jambo muhimu kwa sasa.

 

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur’an Tanzania, Sheikh Othman Kaporo aliziomba  taasisi mbalimbali za kiislaam kushirikiane katika kuwalea vijana kwenye maadili mema.

 

Katika mashindano hayo mshiriki kutoka nchini Yemen, Mohammed Abdo Ahmed (22) ameshinda nafasi ya kwanza katika upande wa kuhifadhi qur’an na amepata zawadi ya Dola za Marekani 5,000 na Mohammed Haruna Hassani (37) ameshika nafasi ya kwanza kwa upande wa kusoma Qur’an kwa njia ya tajweed na kupewa zawadi ya shilingi milioni mbili.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Fainali za Mashindano ya 29 ya Kimataifa ya Qur'an kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam, Mei 2, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

Baadhi ya waumin wa dini ya kiislaam wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipozungumza katika Fainali za Mashindano ya 29 ya Kimataifa ya Kuhifadhi  Qur'an Tukufu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Mei 2, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

Baadhi ya waumin wa dini ya kiislaam wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipozungumza katika Fainali za Mashindano ya 29 ya Kimataifa ya Kuhifadhi  Qur'an Tukufu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Mei 2, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Mshindi wa kwanza wa kusoma Qur'an kwa njia ya tajweed kutoka Tanzania, Mohammed Harun  (kushoto) katika Fainali za Mashindano ya Kimataifa ya Qur'an kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam, Mei 2, 2021.  Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Abubakar Kunenge, Wa pili kushoto ni  Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir , wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Kuhifadhisha Quran, Shekh  Othman Kaporo na kulia ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Mshindi wa Kwanza  wa Mashindano ya 29 ya Kimataifa ya Kuhifadhi  Qur'an Tukufu kutoka Yemen, Mohammed Abdo Ahmed  (kushoto) hundi ya Dola za Marekani 5,000 katika fainali za mashindano hayo kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam, Mei 2, 2021.  Kulia ni Mwenyekiti Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur'an, Sheikh  Othman Kaporo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na viongozi baada ya kukabidhi zawadi na kuzungumza katika Fainali za Mashindano ya  Kimataifa ya Kuhifadhi Qur'an Tukufu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam, Mei  2, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

BASATA, BODI YA FILAMU NA COSOTA ZAAGIZWA KURATIBU VYEMA SUALA LA UHAKIKI WA WASANII

 


Na Richard Mwamakafu, Arusha

Waziri ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Innocent Bashungwa amezitaka taasisi za Barazala la Sanaa la Taifa (BASATA) Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Bodi ya Filamu (TBF) kufanya uhakiki wa kazi za sanaa kwa utaratibu ambao haukwamishi kazi za wasanii nchini.

Mhe. Bashungwa amesema hayo Mei 02, 2021 Jijini Arusha ambapo ameeleza kuwa uhakiki unaofanywa na taasisi hizo lengo lake ni kulinda maadili kwa kuhakikisha maudhui ambayo yapo kinyume na mila na desturi za Mtanzania bila kuathiri ubunifu wa wasanii wetu, maendeleo ya sanaa nchini na kudumaza ukuaji wa ajira.

“Kwa upande wa filamu, uhakiki unasaidia kujua maudhui yaliyopo kwenye filamu husika ili kuamua ipangiwe daraja gani na unasaidia kuepusha maudhui mabaya ya kuharibu maadili ya jamii yetu, yadhibitiwe kabla ya kufika kwa mtazamaji/msikilizaji” amesema Waziri Bashungwa.

Waziri ameongeza kuwa Wizara inaendelea kupokea maoni na kukutana na wadau ikiwa ni sehemu ya namna ya kuboresha chambuzi na hoja zilizowasilishwa ambazo zitasaidia kuziunganisha BASATA, COSOTA na Bodi ya Filamu ili kuleta tija na kusimamia kazi za Sanaa na Wasanii nchini.

Vilevile amewasisitiza wadao ambao hawajawasilisha maoni yao, kuendelea kutoa maoni yatakayosaidia kuwa na Sheria na Kanuni zinazosimamia maudhui ya kazi za Sanaa kupitia taasisi hizo ili yasiende kinyume na mila, desturi na utamaduni wa Mtanzania.