Matokeo chanyA+ online




Thursday, June 10, 2021

TANZANIA KUSHIRIKI MKUTANO WA 26 WA NCHI WANACHAMA WA MKATABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MABADILIKO YA TABIANCHI






Tanzania inatarajiwa kushiriki Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika kuanzia Novemba mosi hadi 12, 2021 mjini Glasgow nchini Uingereza.

Hayo yamebainika leo Juni10, 2021 wakati wa kikao kati ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. David Concar aliyemtembelea ofisini kwake jijini Dodoma leo Juni 10, 2021.

Waziri Jafo alisema kuwa mkutano huo utakaofanyika utatoa mchango mkubwa katika sekta ya mazingira kwani nchi mbalimbali zitakutana na kujadili namna gani ya kuchangia kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kupunguza hewa ya ukaa duniani na ukataji wa miti.

Alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kukuza uhusiano wa kidiplomasia na nchi mbalimbali na ambazo zimekuwa zikitoa mchango katika hifadhi ya mazingira.

“Changamoto ya mazingira imekuwa ni kubwa kwa hiyo ni jukumu letu Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia Sera na kuratibu shughuli zote za mazingira na kuhakikisha nchi yetu inakuwa kinara katika uhifadhi mazingira,” alisema Jafo.

Pia aliwaomba wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuungana kwa pamoja na kuifanya Tanzania kuwa ya mfano katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yanayoikabali nchi yetu.

Katika mazungumzo yao, Balozi Concar alipongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais hususan katika kuhakikisha suala la uhifadhi na usafi wa mazingira linakuwa endelevu.

Balozi huyo aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa yakisababisha madhara kwa binadamu yakiwemo ukame na mafuriko.

Alisema mkutano huo utakaofanyika Uingereza utakuwa na mchango mkubwa kwa kuwa nchi mbalimbali zitakutana na kujadili namna gani ya kuchangia katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza hewa ya ukaa duniani na ukataji wa miti.

Kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Mazingira, Dkt. Andrew Komba pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira, Bi. Catherine Bamwenzaki Akizungumza na Balozi Concar.

 


 

RAIS SAMIA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS WA BOTSWANA DKT. MASISI IKULU JIJINI DAR ES SALAAM


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akisalimiana na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Botswana Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Juni 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Zawadi za Picha Rais wa Jamhuri ya Botswana Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Juni 2021.

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akipokea na kuiangalia zawadi ya picha aliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Botswana Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Juni 2021.

 

Wednesday, June 9, 2021

RC SINGIDA AZITAKA HALMASHAURI KUSIMAMIA VYANZO VYA MAPATO

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba jana, wakati akikagua jengo la maabara ya Hospitali ya wilaya iliyopo Old Kiomboi katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge, akisisitiza jambo wakati akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba jana.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula, akisoma taarifa ya miradi mbalimbali ya maendeleo ya wilaya hiyo.

Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.
Baadhi ya watumishi wa Wilaya ya Iramba wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Makofi yakipigwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba,  Innocent Msengi akizungumza kwenye kikao hicho.
Dkt.Mahenge (katikati) akipokea taarifa ya ujenzi wa Maabara ya Hospitali ya Wilaya ya Iramba kutoka kwa Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Hussein Sepako (kushoto)  wakati alipofika kuona maendeleo ya ujenzi huo. 
Baadhi ya wauguzi wa hospitali hiyo wakiwa nje wakati wa ziara hiyo.
Mhasibu wa mapato wa wilaya hiyo, Optatusy Ottolikiliwike, akitoa maelezo ya ukusanyaji wa mapato kwenye mnada wa Igumo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na wananchi alipotembelea Mnada wa Igumo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula.
Mkazi wa Iramba, Lutha Nathaniel, akimpongeza mkuu wa mkoa kwa kufanya ziara katika wilaya hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na  Mjasiriamali  alipotembelea Mnada wa Igumo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na watendaji wa wilaya hiyo  alipotembelea Mnada wa Igumo. Kulia ni Askari Polisi wakiimarisha ulinzi eneo hilo. Katikati ni Mkurugenzi wa Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge, akipata maelezo ya Mradi wa Maji uliopo Kijiji cha Kyalosangi Kinampanda..

 Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASAWilaya ya IrambaMhandisi Ezra Mwacha, akitoa taarifa ya mradi huo kwa mkuu wa mkoa.

Mwonekano wa tenki la maji la mradi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge, akiagana na Watendaji na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba baada ya kumaliza ziara yake hiyo.

 

Na Dotto Mwaibale, Singida 

MKUUwa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amewataka watendaji wa halmashauri kusimamia ipasavyo vyanzo vya mapato vilivyopo kwenye maeneo yao.

Mahenge alitoa agizo hilo jana wilayani Iramba mkoani hapa katika muendelezo wa ziara zake za kutembelea halmashauri zote kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na watumishi, watendaji na wananchi.

Alisema anataka viongozi hao hasa watendaji kujua kuwa kupata mapato makubwa sio lazima kuwa na vyanzo vikubwa kama madini na miradi ya mashamba bali ni  hivihivi vidogo vilivyopo ambapo vikisimamiwa vizuri vitazifanya  halmashauri kupata mapato yakutosha.

"Nataka watendaji na viongozi wenzangu wajue kwamba mnada ni chanzo kizuri sana cha mapato hivyo kitiliwe maanani, kuna dhana kuwa ili kupata mapato makubwa ni lazima kuwepo na miradi mikubwa na vitu vingine vinavyofanana na hivyo hapana hivi hivi vidogo vikisimamiwa vitafanya mambo makubwa," alisema Mahenge.

Dkt.Mahenge alisema katika ziara yake hiyo wilayani humo aliamua kutembelea mnada ikiwa ni chanzo mojawapo cha mapato ambacho kimsingi kinajumuisha watu wengi sana.

Aliyata makundi hayo ya watu kuwa ni wachoma nyama, wauza nguo,mifugo na makundi mengine na kuwa alichojifunza ni kutokuwepo kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato licha ya kuwepo kwa makundi hayo.

" Nimejifunza hatuna usimamizi mzuri na kuwa chanzo hicho  kipokipo tu kwa sababu hayupo mtu anaye hakiki upatikanaji wa mapato kama yamepanda au kushuka na kwanini makusanyo yana kuwa yale yale kila wakati.

Alisema katika minada aliyoitembelea amebaini kutokuwepo kwa utaratibu wa kuwa sajili wanunuzi wa mifugo kwenye eneo moja badala yake kila mtu anafanya kivyake jambo linalosababisha upotevu wa mapato.

Dkt. Mahenge alisema kukosekana kwa usimamizi mzuri wa mapato katika maeneo hayo kunasababishwa na baadhi ya watendaji wa serikali ambao sio waaminifu ambao wamechangia kutotumika kwa maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za ununuzi na uuzaji wa mifugo na badala yake kwa kushirikiana na wanunuzi hao wamekuwa wakifanyia shughuli hizo nje ya maeneo hayo.

Aidha alisema jambo kubwa analolihitaji ni usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato kwenye mifugo na kwa wafanyabiashara wengine ambao wanafanya shughuli za kibiashara kwenye eneo hilo la mnada ambao wengi wao hawana vitambulisho vya ujasiriamali hivyo ametaka kuongezwa kasi ya utoaji wa vitambulisho hivyo kwani wananchi wako tayari lakini hawajapa fursa ya kuvipata. 

Alizitaka timu za ukusanyaji wa mapato za halmashauri kunapokuwa na minada kwenda kujionea ukusanyaji wa mapato badala ya kumuachia mtu mmoja ambaye anaweza kurubuniwa na kusababisha upotevu wa mapato. 

Dkt.Mahenge katika ziara yake alitembelea na kukagua ujenzi wa jengo la maabara hospitali ya wilaya ambapo hakuridhishwa na gharama halisi zilizotumika kwa ujenzi huu kuanzia msingi hadi hatua ya linta na kumwagiza mkuu wa wilaya hiyo kufanya uchunguzi.

Aidha alikagua ukusanyaji wa mapato katika Mnada wa Igumo na mradi wa maji uliopo Kijiji cha Kyalosangi.

EPUKENI MAPUNGUFU KATIKA KUSIMAMIA MIRADI ILI KUONDOKANA NA HOJA ZA UKAGUZI


Na Anthony Ishengoma-Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha zinakuwa na miradi inayozingatia masharti ya kitaalamu ikiwemo usanifu, michoro na taratibu za manunuzi zilizowekwa na Serikali ili kuepukana na hoja za ukaguzi.

Dkt. Sengati amesema hayo leo Katika Manispaa ya Kahama alipokaribishwa kwa mara ya kwanza na wadau mbali mbali kutoka Wilaya ya Kahama na kuwataka watendaji na viongozi katika Wilaya hiyo kuwa na fikra za kimapinduzi zitakazo sukuma maendeleo ya mkoa na Taifa kwa ujumla.

Dkt. Sengati pia amewataka viongozi wa Halmashauri kuweka katika mipango yao miradi yote inayoibuliwa na Halmashauri ili miradi hiyo isije kuonekana na miradi hewa lakini pia kuwataka watendaji hao kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya masuala ya lishe.

Aidha Dkt. Sengati amekumbusha kuwa Halmashauri zimekuwa zikijisahau kutenga sh.1000 kwa ajili ya mipango ya lishe au kutenga fedha lakini fedha izo zimekuwa hazipelekwi kama inavyokusudiwa na hivyo kusababisha masuala ya lishe nchini kushindwa kupimika.

‘’Fedha nyingi zinaenda kwenye posho na kwenye mambo ya kiuendeshaji na bahati mbaya baadhi ya Taasisi zimekuwa hazitekelezi miradi yenye mashiko kwa kipindi cha mwaka mzima’’. Aliongeza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Dkt. Batlida Buriani amewapongeza Wilaya ya Kahama kwa ujenzi wa shule nyingi na kuongeza kuwa hiyo haitoshi bali juhudi za kuhakikisha ufaulu unaongezeka zinatakiwa ili kuhakikisi kasi ya ujenzi wa shule katika Wilaya ya Kahama.

Adha Dkt. Buriani ameongeza kuwa Wilaya hiyo inapaswa kuangazia upya suala la ugonjwa wa ukumwi ambapo Wilaya ya Kahama haijafanya vya kutosha kuhakikisha maambukizi ya Ukimwi yanapungua.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama Bw. Anamlingi Macha amesema wachimbaji wadogo wadogo wamekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Halmashauri za Wilaya ya Kahama ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/21 jumla ya kilo takribani elfu 1.7 zilitokana na wachimabaji wadogo.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Kahama Mzee Wilfred Bilago amesema Wilaya ya Kahama imekuwa ikifanya vizuri katika kuhakikisha wazee wilayani humo wanapatiwa huduma za Bima ya Afya iliyoboreshwa.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa huo wako katika Wilaya ya Kahama kwa ajili ya kukutana na wadau wa Wilaya hiyo lakini pia kukutana na viongozi na baadhi ya wananchi wa Wilaya hiyo.



KATIBU MKUU WA CCM CHONGOLO AKUTANA NA BALOZI WA KOREA KASKAZINI


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea nchini Tanzani Mhe. Kim Yong Sung kulia ni Katibu wa NEC Uhusiano wa Kimataifa Kanali Ngemela Lubinga

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea nchini Tanzania Mhe. Kim Yong Sung.



Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea nchini Tanzani Mhe. Kim Yong Sung.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo tarehe 9 Juni, 2021 katika Ofisi za CCM Makao Makuu Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, pamoja na mambo mengine Balozi huyo amekutana na Katibu Mkuu kwa lengo la utambulisho na kuendeleza Ushirikiano na Urafiki wa Kihistoria uliopo kati ya Chama Cha Mapinduzi na Chama Tawala cha Wafanyakazi Cha Korea Kaskazini (Workers Party Of Korea).

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Ndg. Ngemela Lubinga.

Huu ni Muendelezo wa Katibu Mkuu kukutana na Mabalozi wa nchi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania kuendelea kutambulishana na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na nchi nyingine, ambapo mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu alikutana na Balozi wa China nchini Tanzania.

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWAAGIZA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI KUFUFUA MADARASA YA MEMKWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafufua madarasa kwa ajili ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA) ili kusaidia kupunguza ongezeko la watu wazima wasiojua kusoma na kuandika.

Ametoa agizo hilo  (Jumatano Juni 9, 2021) wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania.

“Naagiza madarasa ya MEMKWA yahuishwe. Wakuu wa Mikoa na Wilaya suala la elimu ya watu wazima liwe sehemu ya ajenda zenu mnapofanya ziara. Fuatilieni kuiona elimu ya watu wazima inahuishwa ili kupunguza na ikiwezekana kuondoa kabisa tatizo la kutokujua kusoma na kuandika”

Aidha, amewataka watumie madarasa hayo kuwezesha watu wazima wapate stadi mbalimbali pamoja na stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK)

Waziri Mkuu amesema kuwa pamoja na kutekeleza majukumu mengine, Taasisi ya Elimu ya Watu wa Wazima iendelee kutekeleza kikamilifu jukumu lake la msingi la utoaji wa elimu ya watu wazima hadi katika ngazi ya wilaya

“Andaeni mkakati wa kusimamia utoaji mafunzo ya stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watu wazima badala ya kutoa astashahada, shahada na stashada tu. Idadi wa Watu wazima wasiojua kusoma imeongezeka hamna jinsi ya kukwepa jukumu lenu hili. Jipangeni upya ninafahamu fika Elimu ya Watu Wazima ni zaidi ya KKK”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wataalam na wanataaluma wa Elimu ya Watu Wazima kutoa ushauri kuhusu namna ya kuboresha Vyuo vya kati vinavyotoa mafunzo mbalimbali ili kuzalisha wahitimu mahiri wanaohitajika katika viwanda na taasisi nyingine.

Akizungumza wakati alipotembelea mabanda katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu ameitaka Taasisi ya Elimu ya Watu wazima kuwatumia maafisa elimu ya watu wazima waliopo kwenye Halmashauri kwa kuwapelekea programu za elimu ya watu wazima ili wazitekeleze bila kujali kama wako kwenye mamlaka gani.

Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kutoa mafunzo ya elimu kwa watu wazima wanaohitaji kujiendeleza kitaaluma na kitaalam.

Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha wanawasaidia kujishughulisha kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na hatimaye kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo wakionyesha vitabu baada ya Waziri Mkuu kufungua kongamano la kimataifa la kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania kwenye ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Juni 9, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha tuzo aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kutokana na mchango wake katika kufanikisha kongamano la Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania baada ya kufungua Kongamano hilo kwenye ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Juni 9, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi tuzo Balozi Nicholas Kuhanga ambaye pia Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Mstaafu wakati Waziri Mkuu alipofungua Kongamano la Kimataifa la Kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania kwenye ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Juni 9, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo (wa pili kulia) na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa William Anangisye (kulia) wakati alipowasili kwenye Viwanja vya Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kufungua kongamano la kimataifa la miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania, Juni 9, 2021. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Kimataifa la kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua kongamano hilo kwenye ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Juni 9, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Kongamano la Kimataifa la Kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania kwenye ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Juni 9, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipofungua Kongamano la Kimataifa la kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania kwenye ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Juni 9, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

SERIKALI KUZINDUA MAKAO YA TAIFA YA WATOTO WAISHIO MAZINGIRA HATARISHI

Na WAMJW - Dodoma

Kuelekea Siku ya Mtoto wa Afrika, Serikali inatarajia kuzindua Makao ya Taifa ya Malezi na Makuzi ya Watoto yaliyojengwa katika Kata ya Kikombo, jijini Dodoma.

Akizungumza leo na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto, Dkt Dorothy Gwajima  amesema Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Isdor Mpango atazindua makao hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yatakayofanyika tarehe 16 mwezi huu.

Dkt. Gwajima amesema lengo la kujengwa kwa makao hayo ni kutatua changamoto za makao ya Taifa ya awali yaliyokuwa Kurasini Dar es Salaam za ufinyu wa maeneo ya shughuli mbalimbali ikiwemo michezo, bustani, ujasiriamali na ufugaji kutofanyika sawasawa hivyo kufanya hali ya lishe na uchumi kuwa duni.

" Ujenzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Taifa wa Kimkakati wa kuwatambua, kutengamanisha na kuwaunganisha na familia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, pia ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais kuwa watoto wanaotunzwa kwenye makao waandaliwe mapema kadri inavyowezekana kuwaunganisha na familia ili kuwawekea msingi wa malezi" alisema Dkt. Gwajima.

Ameongeza pia watoto wanatakiwa kukaa kwenye makao kwa muda tu na wakiisha kuimarika warejeshwe kwenye makazi ya kawaida iwe ya kambo au kuasili ili waishi kawaida katika familia.

Dkt. Gwajima amesema, uzinduzi huo utaambatana na uzinduzi wa vituo vya Jamii vya malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya watoto pamoja na Baraza la Taifa la Watoto hapo tarehe 14 mwezi huu.

Aidha, Dkt. Gwajima ametoa rai kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanatimiza jukumu la malezi ya watoto wao na kuwa, hatua ya kulelewa katika makao iwe ni ya mwisho baada ya hatua zote kushindikana.
 
Mradi wa  Ujenzi wa  Makao ya Watoto Kikombo, umetekelezwa kwa Ushirikiano kati ya Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto  na  Shirika la ABBOT Fund Tanzania na Makao hayo yana uwezo wa kuhudumia watoto 250 kwa wakati mmoja na hadi sasa watoto wanaohudumiwa katika Makao hayo ni 28.

RAIS DK.MWINYI AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA VIONGOZI WA DINI ZANZIBAR IKULU LEO



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Katibu wa Dini mbalimbali Zanzibar Askofu Dickson D.Kaganga, walipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar na (kulia kwa Rais) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kabi, Katibu wa Mufti.Sheikh. Khalid Ali Mfaume na Fr.Damas Mfoi wa Kanisha Katoliki Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Viongozi wa Dini mbalimbali Zanziubar wakiongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kabi (kulia kwa Rais) waipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo.9-6-2021

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kabi, baada ya kumaliza mazungumzo na Viongozi wa Dini mbalimbali Zanzibar yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

Katibu wa Umoja wa Dini Mbalimbali Zanzibar Askofu Dickson D Kaganga akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar baada ya kumaliza mazungumzo yao na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar, ujumbe huo wa Viongozi wa Dini ukiongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar.Sheikh Saleh Omar Kabi.(Picha na Ikulu)