Matokeo chanyA+ online




Monday, June 29, 2020

WAZIRI ZUNGU AKUTANA NA MENEJIMENTI YA NEMC NA WADAU WA MAZINGIRA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Mussa Azzan Zungu  akifafanua jambo wakati wa kikao na Menejimenti ya Baraza la Taifa la Uhifadhi na Mazingira (NEMC) pamoja na Wadau wa Mazingira kilichofanyika katika Ofisi za NEMC jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Mussa Azzan Zungu  akiongea wakati wa kikao na Menejimenti ya Baraza la Taifa la Uhifadhi na Mazingira (NEMC) pamoja na Wadau wa Mazingira kilichofanyika katika Ofisi za NEMC jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Mazingira (NEMC) Dkt Samuel Gwamaka akitoa ufafanuzi wa jambo wakati wa kikao hiko.

Mdau wa Mazingira kutoka Mkoani Mbeya Bwana Ali Adon akionyesha nyaraka mbalimbali ambazo alihitaji kuzipatia ufafanuzi kuhusiana na biashara yake ya Kituo cha Mafuta kilichoko Mkoani Mbeya.


Mfanyabiashara kutoka Wellworth Company Bwana Zulfakir Ismail akichangia jambo wakati wa kikao hiko kilichoitishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Mussa Azzan Zungu  kilichokutanisha Menejimenti ya NEMC na Wadau mbalimbali wa Mazingira

WAZIRI MHAGAMA KUFUNGUA KIKAO CHA MSAJILI NA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA KUJADILI TAARIFA YA CAG


Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu Jenister Mhagama anatarjiwa kufungua kikao cha siku mbili baina ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Waziri wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu Jenister Mhagama

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Abuu Kimario, kikao hicho cha Msajili na viongozi wa vyama vya siasa kitafanyika tarehe 29 na 30 ya mwezi huu kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) kuanzia saa mbili asubuhi na kitawahusu viongozi wa kisiasa na watendaji waandamizi wa vyama vya siasa.

Siku ya kwanza ya kikao hicho kitawashusu wenyeviti wa taifa, makatibu wakuu na maafisa wanaohusika na masuala ya kisheria. Siku ya pili itawahusu wenyeviti bodi ya wadhamini, maafisa masuuli, wahasibu au weka hazina.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa ajenda kuu za mkutano huo ni kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na zoezi la uhakiki wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililofanyika mwezi Machi mwaka huu.

Mbali na ajenda hizo kuu mbili, taarifa hiyo imeeleza kuwa mada zingine ambazo zinalenga kuondoa migogoro na kuongeza ufanisi kwenye uendeshaji wa vyama vya siasa zitawasilishwa. Baadhi ya mada zitakazowasilishwa ni pamoja na maadili ya viongozi wa umma, umuhimu wa bima ya afya, jinsi ya kuandaa taarifa za fedha kwa ajili ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi wa Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wajibu wa bodi ya wadhamini ya chama cha siasa na Sheria ya Vyama vya Siasa kuhusu usimamizi wa mapato na matumizi na vyama vya siasa.

Kikao hicho cha siku mbili baina ya Msajili wa Vyama vya Siasa na viongozi wa vyama vya siasa ni mwendelezo wa juhudi za Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakikisha vyama vya siasa vinajiendesha kama taasisi na kuondoa migogoro ambayo imekuwa ikiathiri demokrasia ya vyama vingi nchini.

‘WALIOKACHA’ KUCHUKUA HATI ZA ARDHI KUANZA KUDAIWA KODI JULAI MOSI


Na Munir Shemweta, WANMM NJOMBE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema kuanzi Julai Mosi mwaka huu wananchi wote wasiochukua hati za ardhi huku maeneo yao yakiwa yamepimwa na michoro yake kuidhinishwa wataanza kudaiwa kodi ya pango la ardhi.

Hatua hiyo inafuatia Bunge la kumi na moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Sheria inayomtaka mwananchi aliyepimiwa ardhi na michoro kuidhinishwa kuchukua hati katika kipindi kisichozidi siku tisini na asipofanya hivyo ataanza kudaiwa kodi ya ardhi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikata utepe kuzindua rasmi Ofisi ya Ardhi mkoa wa Njombe jana. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Lucy Msafiri, wa tatu kulia ni katibu Tawala mkoa wa Njombe Catarina Revocatu na kulia ni Kamishna Msaidzi wa Ardhi mkoa wa Njombe Christopher  Mwamasage.

Akizungumza na wananchi mkoani Njombe jana wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya ardhi ya mkoa  huo, Naibu Waziri Mabula alisema, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wamiliki wa ardhi  kukwepa kuchukua hati za ardhi wakati taratibu zote zikiwa zimekamilika ikiwemo  kuidhinishwa michoro na kuwekewa alama za mawe.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi hati yake ya ardhi mkazi wa Njombe Naomi Msafiri wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi  mkoa wa Njombe jana. kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Lucy Msafiri.

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, kuanzia Julai Mosi mwaka huu muarobaini kwa wamiliki wasiotaka kuchukua hati za ardhi umefika kwa kuwa atakayeshindwa kuchukua hati atalazimika kudaiwa kodi kuanzia pale michoro yake ilipoidhinshwa.

‘’Kuanzia leo wamiliki wa ardhi hapa Njombe ambao wamepimiwa na michoro yao kuidhinishwa waende halmashauri za wilaya kurekebisha kumbukumbu zao na baada ya hapo asiyerekebisha baada ya siku tisini tunaanza kumdai’’ alisema Dkt Mabula


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Ramani ya Tanzania pamoja na ile ya mkoa wa Njombe Mkuu wa wilaya ya Njombe Lucy Msafiri wakati wa uzinduzi wa ofisi ya ardhi  mkoa wa Njombe jana.

Aliwaagiza maafisa ardhi katika halmashauri za wilaya kuhakikisha kuanzia Julai mosi wanawapelekea hati ya madai wale wote waliopimiwa na michoro kuidhinishwa ili waanze kulipa kodi ya pango la ardhi.

Alisema, pamoja na wananchi wakiwemo wa Njombe kufurahia usogezwaji huduma za sekta ya ardhi karibu lakini ni lazima wawajibike kwa kulipa kodi ya ardhi na kupatiwa hati aliyoieleza kuwa inaongeza thamani ya ardhi sambamba na hati miliki yake kutumika katika shughuli za kiuchumi.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya majalada katika ofisi ya ardhi mkoa wa Njombe jana wakati wa uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa huo.wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Lucy Msafiri na kulia ni  Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Njombe Christopher Mwamasage.

Aidha, amezitaka ofisi za ardhi katika halmashauri zote nchini kutoa elimu kwa wananachi wa maeneo yao kuhusiana na umuhimu wa kuchukua hati ili kujua takwa la kisheria hasa ikizingatiwa wengi wao wameshindwa kuchukua hati kwa sababu mbalimbali.

Akiegeukia uchukuaji hati za ardhi kwa mkoa wa Njombe, Dkt Mabula alisema mkoa huo una jumla ya hati 42,516 zilizoidhinishwa lakini kati ya hizo ni hati 11,246 tu ndizo wamiliki wake walijitokeza kuzichukua huku wamiliki 31,270 wakiwa hawajachukua.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia Kabati za kutunzia nyaraka za ardhi katika ofisi ya ardhi mkoa wa Njombe jana wakati wa uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa huo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Lucy Msafiri.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe Lucy Msafiri aliyemuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Njombe katika hafla ya uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa alisema, uanzishwaji ofisi za ardhi katika mkoa wa Njombe utaondoa changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika masuala ya ardhi kwenye mkoa huo.

Mkuu huyo wa wilaya ya Njombe alibainisha kuwa, mkoa wa Njombe ni maarufu kwa kilimo cha Miti, Chai, Mahindi, Viazi na Parachichi na baadhi ya wamiliki wa mashamba hayo hawana hati miliki za ardhi hivyo uanzishwaji ofisi hizo unafungua milango kwa wamiliki wa mashamba  kumilikishwa kwa haraka.


Kamishna Msaidizi wa ardhi kutoka Makao Makuu ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wilson Ruge akisoma taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu wake wakati wa uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa wa Njombe jana. (PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE WA WIZARA YA ARDHI)


Naye Kamishna Msaidizi wa ardhi Wilson Ruge ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo, alisema uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa ni moja ya mikakati iliyopewa kipaumbele na serikali ya awamu ya tano katika kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kubainisha kuwa tayari kazi kubwa imefanyika ikiwemo usambazaji vifaa na kuwataka wananchi kujitokeza kumilikishwa ardhi zao.

TAKUKURU MKOA WA SINGIDA KUWAFIKISHA MAHAKAMANI HAKIMU, MZAZI MWENZAKE KWA TUHUMA ZA KUOMBA RUSHWA

 Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida , Adili Elinipenda, akizungumza leo asubuhi kuhusu kukamatwa, Bahati  Ilikunda Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kilimatinde wilayani Manyoni na Mzazi mwenzake Haji Bwegege kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa. Kulia ni Afisa wa TAKUKURU, Shemu Mgaya.
Maafisa wa TAKUKURU wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Na Dotto Mwaibale, Singida

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida inatarajia kuwafikisha kwenye Mahakama ya Wilaya ya Manyoni, Bahati  Ilikunda Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kilimatinde na Mzazi mwenzake Haji Bwegege ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kwa makosa ya kuomba na kupokea Rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya Mwaka 2007.

Akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye ofisi  za PCCB, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, alisema walipokea taarifa kutoka kwa mwananchi mmoja ambaye jina lake wamelihifadhi, kuwa Bahati Ilikunda wa Mahakama ya Mwanzo Kilimatinde Wilayani Manyoni anaomba Rushwa ya shilingi 350,000/=, ili atoe upendeleo kwa mtoa taarifa kwenye shauri la madai namba 03/2020, shauri ambalo lipo mbele yake

Alisema Juni 28/ 2020 huko wilayani Manyoni  maeneo ya kituo cha mabasi yaendayo Dodoma, Maofisa wa TAKUKURU walimkamata Haji Bwegege ambaye ni mzazi mwenzake na Bahati baada ya kupokea rushwa ya  shilingi 170,000/= ikiwa ni sehemu ya  shilingi 350,000/=zilizoombwa.

Alisema uchunguzi wa TAKUKURU mkoa wa Singida umejiridhisha kuwa Haji Bwegege na Bahati Ilikunda  wana mahusiano ya kifamilia (Wana mtoto waliyezaa pamoja) jambo linaloashiria uwezekano wa Bahati kumtumia Haji katika kupokea rushwa anazoziomba. 

Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa  Singida inatoa shukrani za dhati kwa Idara ya Mahakama mkoani hapa kwa jinsi wanavyoshirikiana kwenye mapambano dhidi ya Rushwa  kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama ya Mkoa. 

MV VICTORIA YATIA NANGA BANDARI YA BUKOBA KATIKA SAFARI YAKE YA KWANZA YA MAJARIBIO


Mwonekano wa New MV Victoria ikitia Nanga katika Bandari ya Bukoba katika safari yake ya kwanza ya Majaribio Mara baada ya kusimama takribani miaka sita kwa marekebisho.
Mwonekano wa New MV Victoria ikitia Nanga katika Bandari ya Bukoba katika safari yake ya kwanza ya Majaribio Mara baada ya kusimama takribani miaka sita kwa marekebisho.
Mwonekano wa New MV Victoria ikitia Nanga katika Bandari ya Bukoba katika safari yake ya kwanza ya Majaribio Mara baada ya kusimama takribani miaka sita kwa marekebisho.

Mwonekano wa New MV Victoria ikitia Nanga katika Bandari ya Bukoba katika safari yake ya kwanza ya Majaribio Mara baada ya kusimama takribani miaka sita kwa marekebisho.

MBUNGE MTATURU ATOA MSAADA WA MABATI, PIKIPIKI, TENKI LA MAJI KUSAIDIA JIMBONI



 Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki,  Mhe. Miraji Mtaturu akizungumza wakati akitoa mchango wa mabati 1000  kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za matawi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zaidi ya 40 katika Wilaya ya Ikungi.


 Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki,  Mhe. Miraji Mtaturu  akitoa msaada wa tenki la maji.
  Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki,  Mhe. Miraji Mtaturu  akitoa msaada wa mabati 1000.
 Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki,  Mhe. Miraji Mtaturu  akitoa msaada wa pikipiki.




Na Mwandishi Wetu, Singida

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki,  Mhe. Miraji Mtaturu ametoa mchango wa mabati 1000  kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Matawi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zaidi ya 40 katika Wilaya ya Ikungi.

Mbali ya kutoa mabati hayo Mtaturu ametoa tenki la maji, pikipiki  mbili kwa  ajili ya matumizi ya kiofisi kwa makatibu na moja kwa Msikiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Ikungi vyote vikiwa na thamani ya shilingi 30.270,000.

Mchango huo ni muendelezo wa jitihada zake za kukiimarisha  chama kilichomuamini na wananchi kumpatia ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo. 

Aidha Mtaturu amekabidhi pikipiki moja kwa ajili ya matumizi ya Chama Cha Mapinduzi katika wilaya hiyo.

Akikabidhi vifaa tu hivyo Mtaturu alisema anatekeleza ahadi yake aliyoahidi wananchi ambapo amewataka wanufaika wa vitu hivyo kuhakikisha wanavitunza na kuendelea kuiamini Serikali iliyopo madarakani inayoongozwa na  Rais John Magufuli ambaye pia ni  Mwenyekiti wa CCM Taifa. 

DKT. MPANGO AAGIZA MATUMIZI YA FEDHA UJENZI KITUO CHA AFYA MUNZEZE KIGOMA YACHUNGUZWE


Muonekano wa baadhi ya majengo likiwemo jengo la upasuaji na wodi ya wazazi katika  Kituo cha Afya Munzeze kilichopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.

Na. Josephine Majula na Peter Haule, WFM, Kigoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameagiza kufanyika uchunguzi wa kina wa matumizi ya zaidi ya shilingi milioni 400 zilizotumika kujenga Kituo cha Afya  Munzeze, wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, baada ya kutoridhishwa na ubora wa majengo ya Kituo hicho.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza na Wananchi wa Kata ya Munzeze alipotembelea na kukagua maendeleo ya  Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Munzeze kilichopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, ambacho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wakazi 25,000 wa kata hiyo

Dkt. Mpango alitoa agizo hilo wakati alipotembelea na kukagua Mradi wa Ujenzi wa Kituo hicho cha Afya ambacho kikikamilika kinatarajiwa kutoa huduma kwa zaidi ya wakazi 25,000 wa Kata hiyo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayopatiwa fedha na Serikali.

 “Nakuagiza Mkuu wa Wilaya  ya Buhingwe uanze kufuatilia matumizi ya fedha hizo na nitatuma  timu ya uhakiki ili tuhakikishe kwamba shilingi milioni 400 zilizotolewa na Serikali zilitumika vizuri au la”, alieleza Dkt. Mpango.


Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Kituo cha Afya Munzeze, Bw. Linus Conrad, akimuongoza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, (katikati), kukagua majengo matano ya Kituo cha Afya Munzeze,  kilichopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, likiwemo jengo la upasuaji, wodi ya wazazi, maabara, chumba cha kuhifadhia maiti na nyumba ya Mganga Mkuu. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina

Dkt. Mpango alisema kuwa uhakiki huo ukibaini ubadhirifu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watu wote waliohusika na ubadhirifu huo na kuonya kuwa huu si wakati wa  kubembelezana.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina alisema atayafanyia kazi maelekezo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango, kwa kuwa tayari alifanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa Ujenzi wa Kituo hicho.

Aidha alimshukuru Dkt. Mpango kwa kufanya ziara katika Wilaya hiyo katika jitihada za kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kikamilifu katika miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa manufaa ya wananchi.


Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Munzeze, Bw. Linus Conrad, ameiomba Serikali itoe kiasi kingine cha shilingi milioni 123 kwa ajili ya kununua vifaa tiba ili Kituo hicho kianze rasmi kutoa huduma kwa wananchi mapema mwezi Julai, 2020.

Bw. Conrad alisema ujenzi wa Kituo hicho ulitakiwa kukamilika Machi, 2019 lakini ilishindikana kutokana na uwepo wa mvua nyingi uliosababishja kushindwa kusafirisha vifaa kwenda eneo la ujenzi na changamoto ya ununuzi.

Kituo hicho cha Afya Munzeze kikikamilika kitaongeza idadi ya watu wanaohudumiwa katika zahanati iliyopo hivi sasa wapatao 16,000 hadi kufikia takribani wakazi 25,000 kutoka vijiji vine vinavyounda kata hiyo vya Munzeze, Kishanga, Kigogwe na Murungu.

Katika hatua nyingine Dkt. Mpango amewaahidi wananchi wa mkoa wa Kigoma kwamba Serikali itajenga barabara inayoanzia katika Mpaka wa Burundi na Tanzania kupita katika maeneo ya Wilaya ya Buhigwe, Kasulu, Kibondo na Kakonko, hivyo kuwawezesha wakazi hao kusafirisha bidhaa katika nchi jirani ikiwemo Uganda na Burundi.

“Baada ya muda mfupi barabara hiyo itakamilika kwa kiwango cha Lami kwani tayari Serikali imeingia mkataba na wakandarasi wane baada ya kupata fedha kutoka mfuko wa b Abudhabi na Kuwait”, alieleza Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango alisema kuwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma watakuwa na uwezo wa kufanya biashara ya mazao likiwemo zao la Tangawizi katika mikoa jirani na pamoja nan chi za Burundi na Uganda.

Sunday, June 28, 2020

KATIBU MKUU VIWANDA ATAKA UJENZI WA KIWANDA KIPYA CHA VIATU CHA KARANGA KUKAMILIKA KWA WAKATI

Baadhi ya vifaa vinavyosubiri kufungwa katika kiwanda cha Karanga  
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe (wa pili kulia) akizungumza na Mhandisi Mkuu wa ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Karanga  Mhandisi Emmanuel Mwangalaba (SP) alipotembelea kiwandani hapo kuangalia Maendeleo ya ujenzi. 
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe ameitaka kampuni ya Tanelec - Arusha kuharakisha utengenezaji wa vifaa  vya umeme ikiwemo  (switch gears ) ambazo zinasubiriwa kufungwa kwenye kiwanda cha kuzalisha bidhaa za ngozi  cha Karanga kilichopo Mkoani Kilimanjaro.

Prof. Shmdoe aliyasema hayo alipofanya ziara kwenye kiwanda cha Karanga ambacho kinajengwa na Shirika la Uzalishaji la Magereza. Lengo la ziara hiyo ni kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kipya ambacho kinajengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni tisa.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe akikagua ujenzi unaondelea katika kiwanda cha kuzalisha bidhaa za ngozi Karanga Mkoa wa Kilimanjaro
 
Katika ziara hiyo Prof.Shemdoe alikagua ujenzi ambao kwa sehemu kubwa umekamilika na kinachosubiriwa ni ufungaji wa (switch gears) ambazo zinatengenezwa na Kampuni ya TANELEC ya Mkoani Arusha.

Prof. Shemode alisisitiza kazi hiyo ifanyike kwa haraka ili wataalamu wa kufunga vifaa hivyo watakapofika wasiwe na sababu ya  kushindwa kujaribu mitambo kwa ajili ya kukosa umeme.

”Ombi langu kwa Tanelec  mhakikishe mnatengeneza kwa wakati  vifaa vya umeme ili vifungwe na kufanyiwa majaribio ili wataalam wa kufunga mashine wakija kusiwe na kikwazo”.

Aidha aliwasihi wasimamizi wa ujenzi  kuhakikisha wanamalizia kazi zilizobakia kwa haraka kwenye ujenzi wa majengo ya awamu ya kwanza.

"Nategema baada ya kukamilika kwa majengo haya uzalishaji utaongezeka mara dufu".

Kwa upande wake msimamizi wa ujenzi huo Mhandisi Mwangalamba (SP)  alimueleza Katibu Mkuu kuwa ujenzi huo ungekuwa umekamilika ila changamoto yao ni utengenezaji wa vifaa  vya umeme kutoka Kampuni ya Tanelec kuchukua muda mrefu hivyo baadhi ya vifaa haviwezi kufungwa mpaka hapo (switch gears)  zitakapofungwa.

Ujenzi wa majengo ya kiwanda  cha Karanga unatekelezwa  na shirika la Uzalishaji la Magereza tangu Juni, 2019 na unatarajiwa kukamilika mwaka huu.

Kiwanda Cha Karanga kitakapokamilika kinatarajia kutoa ajira 5000 za moja kwa moja na zisizokuwa rasmi 4000 kutokana na shughuli mbalimbali katika eneo hilo.


Friday, June 26, 2020

NAIBU WAZIRI NYONGO AMALIZA MGOGORO KWENYE MACHIMBO YA MADINI HANDENI


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wananchi kwenye eneo la machimbo ya dhahabu la Kwandege lililopo wilayani Handeni mkoani Tanga tarehe 25 Juni, 2020.


Naibu Waziri  wa Madini, Stanslaus Nyongo ametatua mgogoro wa muda mrefu kati ya mmliki wa machimbo ya dhahabu ya Kwandege yaliyopo wilayani Handeni  mkoani Tanga, Godfrey Bitesigirwe na wananchi wanaoendesha shughuli za uchimbaji wa madini katika machimbo hayo mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Tanga  yenye lengo la kukagua shughuli za madini na kutatua changamoto  mbalimbali.

Mara baada ya kusikiliza kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi kupitia mkutano wa hadhara mapema jana tarehe 25 Juni, 2020 alielekeza mmiliki wa leseni ya madini, Godfrey Bitesigirwe, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Zabibu Napacho, Afisa Mgodi Mkazi wa Handeni na wananchi kukaa pamoja na kuweka makubaliano ya pamoja yatakayowezesha wananchi na mmiliki wa leseni kunufaika kwa pamoja huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.

Aidha Naibu Waziri Nyongo alielekeza kuangaliwa upya na kufanyiwa marekebisho kwa mkataba kati ya wachimbaji wa madini na mmiliki wa leseni ili kuondoa kasoro zilizokuwa zinalalamikiwa na wananchi hao.

Wananchi wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) kwenye eneo la machimbo ya dhahabu la Kwandege lililopo wilayani Handeni mkoani Tanga tarehe 25 Juni, 2020


Alisema kuwa ili kuhakikisha wananchi maskini wananufaika  na rasilimali za madini, Serikali imeweka utaratibu wa kurasimisha wachimbaji wasio rasmi na kuwasaidia ili waweze kutajirika huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.

Katika hatua nyingine Nyongo aliwataka wananchi kuchimba kwa kufuata sheria na kanuni za madini huku wakijikinga na magonjwa hatarishi kama COVID 19.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo alimpongeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Zabibu Napacho na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe kwa hatua za awali za utatuzi wa mgogoro zilizofanywa kwa mafanikio makubwa.

Awali akisimulia historia ya mgogoro huo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Zabibu Napacho alieleza kuwa awali ofisi yake ilipata taarifa za kuwepo kwa uvamizi wa  wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika eneo la kijiji cha Kwandege  kwenye leseni inayomilikiwa na Godfrey Bitesigirwe ambapo ofisi ilimshauri  kuchukua hatua za kuzuia uchimbaji usio rasmi ili kuepusha ajali pamoja na upotevu wa kodi za serikali pamoja na utoroshaji wa madini.

Alisema kuwa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Ofisi ya Afisa Migodi Mkazi wa Handeni na Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Handeni ilifanya ukaguzi ili kujionea hali halisi na kubaini wachimbaji 300 wakiendelea na shughuli za uchimbaji kwenye leseni husika na kuwataka wachimbaji hao kusubiri utaratibu maalum utakaowekwa kabla ya kuendelea na shughuli za uchimbaji.


Mmoja wa wananchi wa eneo la machimbo ya dhahabu la Kwandege lililopo wilayani Handeni mkoani Tanga akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani).

Na Greyson Mwase, Tanga

Aliendelea kusema kuwa katika hatua nyingine, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga iliwaelekeza wamiliki wa ardhi katika maeneo yenye leseni za uchimbaji wa madini kukutana na mmiliki wa leseni ambapo mara baada ya kukutana walikubaliana wamiliki wa mashamba katika maeneo yatakayofanyika uchimbaji wa madini ya dhahabu kupata asilimia saba ya thamani ya madini baada ya tozo za Serikali na gharama zote za uchimbaji wa madini  kuwa chini ya mmiliki wa leseni.

Makubaliano mengine yalikuwa ni pamoja na umiliki wa mashamba kuendelea kuwa chini ya wamiliki na tozo za Serikali  ambazo ni mrabaha asilimia 6 ada ya ukaguzi asilimia 1 na ushuru wa huduma za jamii 0.3 ya thamani ya madini zitakatwa kabla ya mgawanyo wa makubaliano.

Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti mbali na kuipongeza Wizara ya Madini kwa kumaliza mgogoro  wananchi hao walieleza changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutozwa kodi ambazo zingetakiwa kulipwa na mmiliki wa leseni ya madini na ukosefu wa vifaa vya uchimbaji wa madini.