Matokeo chanyA+ online




Thursday, August 5, 2021

TANZANIA NA KENYA WAKUBALIANA KUZIPATIA UFUMBUZI CHANGAMOTO ZA KUPIMA UVIKO 19 WASAFIRI


Na.WAMJW-Nairobi

Tanzania na Kenya wamekubaliana ndani ya wiki nne zijazo kufanyia kazi changamoto kubwa nne katika eneo la kupima wasafiri UVIKO 19.

Makubaliano hayo yamefanyika leo kwenye mkutano wa pamoja baina ya Mawaziri wa Afya wa Tanzania Dkt. Dorothy Gwajima na Waziri wa afya nchini Kenya Sen. Mutahi Kagwe mjini Nairobi.

Moja ya makubaliano ya kufanyia kazi changamoto hizo ni pamoja na kushusha gharama za upimaji wa UVIKO-19 kwa wasafiri wanaoingia na kutoka katika nchi hizo mbili ili kuchochea masuala ya biashara na utalii baina na nchi hizo mbili.

Nchi hizo pia zimekubaliana kufanyia kazi changamoto ya kulipisha fedha kipimo cha haraka cha Corona (PCR) kwa wasafiri wanaotumia njia ya barabara ikiwemo kuona uwezekano wa kushusha kwa kiasi kikubwa gharama hizo kwa wasafiri wanaotumia ndege.

Kwa upande wa madereva wanaosafirisha mizigo na bidhaa muhimu wamekubaliana kufanyia kazi uwezekano wa kutokutozwa gharama kwa kipimo cha Corona ili kupunguza mzigo kwa wasafirishaji ikiwa ni njia ya kuchochea uchumi kwa nchi hizo mbili.

Aidha Tanzania na Kenya wamekubaliana kuona uwezekano wa kutumia mifumo ya kielektroniki kwa ajili ya kufuatilia afya za wasafiri pamoja na kudhibiti wasafiri wasio kuwa waaminifu kwa kugushi vyeti hivyo wanapopita mipakani.

Hata hivyo katika mkutano huo Mawaziri hao wamekubaliana kufanyia kazi mpango wa kuvitambua vyeti vya upimaji vinavyotolewa na mamlaka za afya za nchi hizo mbili, pamoja na kubadilishana taarifa zinazohusu masuala ya afya ili kuimarisha udhibiti wa magonjwa mbalimbali yanayowaathiri wananchi wa pande hizo mbili ikiwemo Malaria, Polio na Corona.

Akiongea wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari Waziri wa Afya Dkt. Gwajima amesema kuwa tatizo la ugonjwa wa Corona ni la dunia nzima hivyo lazima kuangalia ni namna gani halitowadhuru sana ili uchumi na ustawi wa jamii na nchi uendelee kwa kuweka makubaliano ya kuishi kwa Amani kama watu wanaoishi katika kijiji kimoja cha afrika mashariki.

Dkt. Gwajima amesema ugonjwa huo uliowafika hauwezi kuwaacha iwapo kutakuwa hakuna suluhu ya pamoja ya kuudhibiti kwani hadi sasa ugonjwa huu umetufundisha mengi na viongozi wa nchi zote mbili wamekuwa wakitoa maono mengi. Hivyo, kama Mawaziri wenye dhamana kwa kushirikiana na wataalam watahakikisha wanatafsiri dhamira ya viongozi wakuu wa nchi ili kuja na uhalisia.

Aliongeza kuwa janga hilo ni kubwa hivyo ni lazima kuendelea kushirikiana katika kudhibiti na kuzuia anuai mpya za ugonjwa wa Corona kwa pamoja kwani miundombinu ya uchumi inashuka katika nchi zetu na kwa jamii pia.

"Baada ya kutokea janga hilo wasafiri na madereva walikua wanatakiwa kuendelea kusafirisha abiria,mizigo na bidhaa muhimu hivyo kubwa ni lazima kuweka jitihada ili kuwarahisishia wananchi kuendelea na shughuli za uchumi na maisha kwa usalama kwa ushirikiano baina ya nchi zetu hizi”.

Naye Waziri wa Afya nchini Kenya Sen.Mutuhi Kagwe amesema kwamba Tanzania na Kenya ni majirani wa muda mrefu hivyo vyovyote watakacho fanya hawawezi kuwaacha majirani zao ambao ni Tanzania.

Katika kukabiliana na Corona Waziri Kagwe amesema lazima kujifunza kuishi nao hivyo ni jambo la kuelewa kwamba hakuna nchi itakayokuwa na nguvu bila kushirikiana.

“Sisi ni wamoja lazima tuendelee kujisaidia wenyewe Katika mapambano haya na vile vile kwenye Malaria,Polio kwa wananchi wetu mipakani” Alisisitiza.

Aliongeza kwamba nchi hizo mbili zina mashirikiano ya muda mrefu katika maeneo na sio tu masuala ya afya tu, hivyo wataimarisha ushirikiano hata katika maeneo mengine.






 

Tuesday, August 3, 2021

RAIS SAMIA AHITIMISHA ZIARA YAKE YA SIKU MBILI NCHINI RWANDA KWA KUTEMBELEA MIRADI MBALIMBALI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana  na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame mara baada ya kuwasili katika eneo la Uwekezaji wa kiwanda cha Inyange Plant Entrance kilichopo mjini Kigali Rwanda  Agosti 03,2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na mwenyeji wake Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakiangalia baadhi ya Bidhaa mbalimbali zinazozalishwa katika kiwanda cha Inyange Plant mjini Kigali wakati walipotembelea kiwanda hicho tarehe  03 Agosti,2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake Rais Paul Kagame wa Rwanda wakitembelea katika kiwanda cha Inyange Plant Entrance mjini Kigali kinachozalisha Juisi, Maziwa na Maji ya kunywa  tarehe 03 Agosti,2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiangalia moja ya aina ya simu zinazotengenezwa katika kiwanda cha Mara Phone Mjini Kigali Rwanda, wakati alipokua katika ziara yake ya siku ya pili nchini Rwanda  tarehe 03 Agosti,2021. Kulia ni Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame, wakiwa katika picha mbele ya Gari aina ya Volkswagen mara baada ya kutembelea kwenye Kiwanda cha kutengenezea Magari CFAO MOTORS Mjini Kigali Nchini Rwanda tarehe  03 Agosti,2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiagana na Rais Paul Kagame wa Rwanda kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Rwanda baada ya kukamilisha ziara yake ya siku mbili Nchini Rwanda  tarehe  03 Agosti,2021.



RAIS SAMIA AREJEA NCHINI KUTOKA RWANDA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 03 Agosti, 2021 amehitimisha Ziara yake ya siku mbili nchini Rwanda kwa kutembelea viwanda vitatu na kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazofanywa na viwanda hivyo.

Katika kiwanda cha kwanza cha Inyange kinachotengeneza vinywaji, Mhe. Rais Samia akiwa na mwenyeji wake Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wamejionea shughuli za uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na maji ya kunywa, maziwa na juisi.

Aidha,  Rais Samia pia ametembelea kiwanda cha kutengeneza simu za mkononi cha Mara Phone na kujionea hatua mbalimbali za utengenezaji wa simu kuanzia hatua ya awali hadi kukamilika kwake.

Pia Mhe. Rais Samia ametembelea kiwanda cha uunganishaji magari cha Volkswagen kilichopo nchini humo na kujionea hatua mbalimbali za kuunganisha magari hayo ambayo huuzwa nchini humo.

Mhe. Rais Samia amewaagiza Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Uwekezaji Mhe. Geoffrey Mwambe kukutana na wamiliki wa viwanda hivyo ili kutumia fursa zilizopo katika viwanda hivyo ikiwa ni pamoja na kuwauzia malighafi zinazopatikana nchini Tanzania.

Mhe. Rais Samia ameagana na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kigali na kurejea Jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza Ziara Rasmi ya siku mbili nchini humo.

Jaffar Haniu

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam Agost 03,2021 akitokea Nchini Rwanda baada ya kukamilisha ziara yake ya Kiserikali ya siku mbili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam  Agost 03,2021 akitokea Nchini Rwanda baada ya kukamilisha ziara yake ya Kiserikali ya siku mbili.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam  Agost 03,2021 akitokea Nchini Rwanda baada ya kukamilisha ziara yake ya Kiserikali ya siku mbili.

WAZIRI MKENDA AIELEKEZA CPB KUNUNUA MAHINDI YALIYOHIFADHIWA NA NFRA KANDA YA MAKAMBAKO


Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akikagua ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa vinavyojengwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Makambako leo tarehe 3 Agosti 2021, wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Njombe. 
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akikagua Skimu ya Umwagiliaji ya Itipingi leo tarehe 3 Agosti 2021, wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Njombe.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Njombe iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe Marwa Rubirya leo tarehe 3 Agosti 2021, wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Njombe.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akisisitiza akikagua hali ya upatikanaji wa mbolea alipotembelea kwenye ghala la kuhifadhia mbolea la Mtewele General Traders leo tarehe 3 Agosti 2021, wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Njombe.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akisisitiza akisisitiza jambo mara baada ya kukagua ghala la kuhifadhia mbolea la Mtewele General Traders leo tarehe 3 Agosti 2021, wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Njombe.
(Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Iringa

Serikali imeelekeza Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) kununua mahinidi kiasi cha Tani 10,400 zilizohifadhiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula-NFRA Kanda ya Makambako kwa miaka mitatu mfululizo.

Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Njombe iliyoanza tarehe 3 Agosti 2021, Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda amesema kuwa Bodi hiyo imepewa jukumu na serikali la kununua na kuuza nafaka hivyo inapaswa kununua mahindi hayo ambayo yamehifadhiwa katika ubora wa hali ya juu.

Waziri Mkenda amesema kuwa mahindi hayo yaliyohifadhiwa na NFRA yanapswa kuzungushwa/kuuzwa ili kutoa fursa kwa NFRA kuingia sokoni kununua mahindi mengine jambo litakalopelekea wakulima kuwa na ahueni ya soko.

“NFRA ikiingia sokoni itatoa nafasi kwa wakulima watakaouza mahindi yao kuweza kununua pembejeo bora na kulima zaidi mazao ya nafaka” Amekaririwa Waziri Mkenda

Amesema kuwa kazi ya NFRA ni kununua nafaka na kuhifadhi ili ikitokea changamoto yoyote nchini nafaka hiyo iweze kutolewa lakini kwa kuwa hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza nchini kwa kipindi cha miaka mitatu hivyo wanapaswa kuyauza ili kununua mahindi mengine kwa ajili ya kuhifadhi.

 Waziri Mkenda amesema kuwa pamoja na mahindi yaliyohifadhiwa kwenye ghala la NFRA Makambako lakini pia kuna Tani 5009.267 za mpunga ambazo pia zinapaswa kutafutiwa masoko hususani ya nje ya nchi.

Akizungumzia kuhusu kusuasua kwa mradi wa ujenzi wa Maghala na Vihenge vya Kisasa Waziri Mkenda amesema kuwa ujenzi huo unafanywa kwa mkopo wa bei nafuu hivyo mkandarasi anapaswa kuhakikisha anamalizia kazi kwa haraka kwa mujibu wa makubaliano.

Katika ziara hiyo ya kikazi ya Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda kwa siku mbili mkoani Njombe, Waziri Mkenda ametembelea na kukagua ghala la mbolea na Mtewele General Traders, Ghala la YARA, Ghala la ETG, pamoja na kukagua Skimu ya umwagiliaji ya Itipingi.

Waziri Mkenda anatarajiwa kuendelea na ziara ya kikazi katika mkoa wa Songwe na Rukwa kesho tarehe 4 Agosti 2021 na tarehe 5 Agosti 2021.

Saturday, July 31, 2021

RAIS SAMIA APOKEA UJUMBE MAALUM KUTOKA KWA RAIS TSHISEKEDI WA CONGO

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimkaribisha Mjumbe Maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mhe. Felix Antoine Tshisekedi, ambaye ni Waziri wa Fedha wa Nchi hiyo Mhe. Nicolas Kazadi Kadino, mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika mazungumzo na Mjumbe Maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mhe. Felix Antoine Tshisekedi, ambaye ni Waziri wa Fedha wa Nchi hiyo Mhe. Nicolas Kazadi Kadino, mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe Maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mhe. Felix Antoine Tshisekedi ulioongozwa na Waziri wa Fedha wa Nchi hiyo Mhe. Nicolas Kazadi Kadino, ulipowasili Ikulu Jijini Dar es Salaam  tarehe 30 Julai, 2021. Picha na Ikulu

Wednesday, July 28, 2021

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AZINDUA CHANJO YA UVIKO 19 JIJINI DAR ES SALAAM

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizindua Chanjo ya Uviko 19 katika Viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam leo Julai 28,2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akionesha Cheti cha Uthibitisho wa Chanjo muda mfupi baada ya kuzindua Chanjo ya Uviko 19 katika Viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam leo Julai 28,2021.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akipata Chanjo ya Uviko 19 katika Viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam leo Julai 28,2021. Picha na Ikulu.

RAIS SAMIA AKUTANA NA MKURUGENZI WA KITUO CHA KUDHIBITI NA KUZUWIA MAGONJWA BARANI AFRIKA (CDC)


 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Mkurugenzi wa Kituo cha kudhibiti na kuzuia Magonjwa Barani Afrika (CDC) Dkt. John Nkengasong, Wakati Dkt. John alipofika  Ikulu Jijini Dar es salaam leo Julai 27,2021. (Picha na Ikulu).


Tuesday, July 27, 2021

WAZIRI MKUU MAJALIWA: HAKUNA MTU ALIYELAZIMISHWA KUCHANJA CHANJO YA UVIKO 19,WANANCHI WAPUUZE UPOTOSHWAJI UNAONDELEA MITANDAONI.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali haijamlazimisha na wala haitamlazimisha mwananchi kuchanjwa chanjo ya ugonjwa wa UVIKO 19, hivyo amewataka Watanzania wapuuze upotoshaji unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.

"Hakuna aliyelazimishwa kuchanja chanjo hiyo na wala hakuna mahali palipoandikwa kwamba lazima wananchi wachanjwe. Chanjo ni hiari tusipotoshane kwa sababu hakuna Serikali inayoweza kuandaa mpango wa kuwaangamiza wananchi wake."

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 27, 2021) wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nandagala ambapo amewasisitiza waendelee kuchukua tahadhari na kujikinga na UVIKO 19.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imeleta chanjo hiyo ili kutoa fursa kwa Watanzania watakaohitaji kuchanjwa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 waweze kuipata kwa ukaribu na urahisi zaidi na si vinginevyo.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza Watanzania waendeleze tabia ya kunawa mikono mara kwa mara na maji safi yanayotiririka na sabuni, watumie vitakasa mikono pamoja na kuvaa barakoa zilizothibitishwa na mamlaka husika.

Mbali na maelekezo hayo, Pia Waziri Mkuu amesema ni vema kwa sasa wananchi wakajiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima na inapolazimu basi wazingatie kukaa umbali wa mita moja au zaidi kutoka mtu mmoja hadi mwingine lengo likiwa ni kujikinga na UVIKO 19.

Mheshimiwa Majaliwa amesema wananchi wanatakiwa wafanye mazoezi ya mara kwa mara kulingana na afya zao pamoja na mazingira yanayowazunguka, pia amewasihi wazingatie lishe bora.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwamba Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya yao na Tanzania kwa ujumla, hivyo waendelee kuiamini Serikali yao.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha wananchi wote nchini wanapata huduma hiyo karibu na maeneo yao ya makazi. Amewataka waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu imedhamiria kuwatumikia.

Amesema tatizo la maji wilayani Ruangwa linaenda kuwa historia kwa sababu Serikali inatekeleza ujenzi wa mradi wa maji wa Mbwinji ambao unatoa maji Ndanda hadi Ruangwa. “Mradi huu mkubwa utapunguza tatizo la upatikanaji wa maji wilayani Ruangwa.”

Kwa upande wake, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba atasimamia ipasavyo kuhakikisha mradi wa maji wa Mbwinji-Ruangwa unakamilika kwa wakati ili wananchi wa wilaya hiyo waweze kuondokana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama.

Aweso amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo yote nchini, amewaomba wananchi waendelee kuwa na subra.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Thursday, July 22, 2021

RAIS DKT.MWINYI AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA WASANII WA BONGO FLEVA IKULU ZANZIBAR.






Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Msanii wa Muziki wa Bongo Fleva Faustina Charles ( Nandy ) akizungumza wakati walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar, akiwa Zanzibar katika onesho lake la Tamasha la Muziki la Nandy lililofanyika jana usiku 21-7-2021 katika Uwanja wa Mao Zedung Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu, wakiwa Zanzibar wakishiriki katika Tamasha la Muziki la Nandy lililofanyika jana usiku 21/7/2021 katika Uwanja wa Mao Zeding.(Picha na Ikulu)



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva ukiongozwa na Mwanamuzi Nandy, walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar, wakiwa Zanzibar katika Tamasha la Muziki la Nandy lililofanyika jana usiku 21/7/2021. Katika uwanja wa Mao Zedung Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)

RC SINGIDA AWATAKA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA KUTOKA TAASISI YA PASS

Mkoa Singida Dkt.Binilith Mahenge, akizungumza na wadau wa kilimo wakati akifungua mkutano wa wadau hao jana ulioandaliwa na Taasisi ya mikopo ya Pass inayojishughulisha na utoaji wa mikopo na udhamini kwa wakulima.
Meneja Maendeleo ya Biashara wa Taasisi hiyo,  Hamisi Mmomi akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa Taasisi hiyo kwenye mkutano huo.
Meneja wa Kanda ya Kati wa Taasisi hiyo,  Hadija Seif  akizungumza kwenye mkutano huo.
Wadau wa kilimo wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Wadau wa kilimo wakiwa kwenye mkutano huo.
 



Na Dotto Mwaibale, Singida

Mkuu wa Mkoa Singida Dkt.Binilith Mahenge amewataka wananchi wa mkoa huo kuchangamkia ujio wa Taasisi ya mikopo ya Pass inayojishughulisha na utoaji wa mikopo na udhamini kwa wakulima kama fursa kwao katika kilimo cha alizeti.

Dkt. Mahenge aliyasema hayo mjini hapa jana wakati akifungua mkutano wa wadau wa kilimo cha zao la alizeti ulioandaliwa na taasisi hiyo.

"Nawahasa wananchi wangu wa  Singida muichukulie taasisi ya Pass kuwa ni fursa moja wapo itakayowawezesha kuharakisha kuwaletea maendeleo," alisema Mahenge.

Alisema Serikali mkoani hapa itawapa Pass ushirikiano wa kutosha ili wananchi wapate huduma hizo muhimu zitakazo wainua kiuchumi kupitia kilimo cha alizeti.

Mahenge aliitaka  taasisi hiyo kupanua wigo wa kujenga uelewa kwa kufanya mikutano mbalimbali kuanzia ngazi ya wilaya jambo litakalosaidia kuharakisha upatikanaji wa huduma bora kwa kutumia fursa ya uwepo wa Taasisi hiyo na mabenki kwa ufanisi zaidi.

Pia alisema itawezesha kutengeneza mazingira mazuri ya kuibua changamoto nyingi na kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kukabiliana nazo ili kuyafikia mapinduzi ya kilimo.

Alisema wakulima wengi ni wadogo na bado wanatumia teknolojia duni lakini kupitia taasisi  kama hiyo wataweza kuweka mazingira rafiki ya kuwafikia wadau wengi wa sekta ya kilimo kundi ambalo kwa muda mrefu limekuwa haliwezi kuzifikia taasisi za kifedha kwa ufanisi.

Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Taasisi hiyo Hamisi Mmomi akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa Taasisi hiyo alisema tangu taasisi hiyo ianzishwe hadi kufikia mwezi Desemba mwaka jana tayari wamekwisha wakopesha wakopaji zaidi ya 46,000 na kudhamini mikopo ya Trioni 1.08.

Alisema katika wakopaji hao 46,000 wanufaika wa moja kwa moja ni zaidi ya milioni 1.6 kwa sababu wakopaji wengine kama vyama vya ushirika kuna wanachama kuanzia 50, 100 hadi 200 hivyo kufikisha idadi hiyo.

Alisema mikopo hiyo imetengeneza ajira zaidi ya milioni 2.5 kutokana na wakulima kuajiri wakulima na kuwa mikopo hiyo wakopaji wamekuwa wakiirejesha kwa wakati kutokana na utaratibu mzuri waliouweka wa kuipitia  miradi walioikopea fedha hizo.

WAZIRI MKUU AITAKA BODI YA KOROSHO KUTAFUTA MASOKO YA UHAKIKA

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya Korosho Tanzania ihakikishe inatafuta masoko ya uhakika ya zao hilo na yatakayotoa bei nzuri na kuwanufaisha wakulima.

 Pia, Waziri Mkuu ameitaka bodi hiyo isimamie mwenendo wa ujenzi wa viwanda vidogo na vikubwa vya kubangulia korosho katika maeneo yote yanayolima zao hilo ili kuondokana na uuzwaji wa korosho ghafi.

 Mheshimiwa Majaliwa ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi, Julai 22, 2021) wakati akizungumza na Wakuu wa mikoa ya Lindi, Pwani, Mtwara na Ruvuma, Mrajisi wa Ushirika, Viongozi wa vyama Vikuu vya Ushirika wa Korosho katika kikao kilichohusu upatikanaji wa pembejeo za korosho kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa mkoani wa Lindi.

 Amesema lazima bodi hiyo ambayo ameizindua lazima iwajibike ipasavyo katika kuhakikisha inaongeza uzalishaji wa zao hilo na iwapo itashindwa Serikali haitosita kuivunja. 

 "Lazima mfuatilie na kuufahamu mwenendo wa zao mnalolisimamia na mjue mfumo unaotumika katika mauzo yake. Pia muwe na takwimu za wakulima na ukubwa wa mashamba yao ili kuweza kuwahudumia kwa urahisi."

 Waziri Mkuu amesema bodi hiyo inatakiwa iandae kalenda maalumu inayoonesha hatua zote zinazopaswa kufuatwa katika kilimo cha zao hilo kuanzia hatua za uandaaji wa shamba hadi mavuno kwa kuzingatia hali ya hewa ya eneo husika na ipelekwe kwa wakulima.

 Amesisiza kwamba utaalamu lazima ufuatwe na uzingatiwe katika kilimo hilo kwa lengo la kuongeza tija kwa wakulima. Pia, Waziri Mkuu ameitaka bodi hiyo ihakikishe pembejeo ikiwemo miche bora na viuatilifu vinapatikana kwa urahisi.

 Kadhalika, Waziri Mkuu ameigiza bodi ya korosho iweke mkakati wa utoaji wa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo cha zao hilo ikiwa ni pamoja na faida ya kulima zao la korosho. "Tumieni magari maalumu kwa ajili ya kwenda kuwafuata wakulima katika maeneo yao na kuwapa elimu."

 Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema tayari mchakato wa kuviwezesha vyama vya wakulima kuanza ubanguaji wa korosho umeanza ambapo katika msimu wa mwaka huu TANECU imepata mkopo kutoka CRDB na itaanza kubangua tani 2,500.

 Amesema vyama vingine vitakavyofuata utaratibu huo baada ya TANECU ni TAMCU, MAMCU na RUNALI ambavyo vyote vinampango wa kuanzisha viwanda vyenye uwezo wa kuchakata tani 2,5000 za korosho kwa mwaka.

 Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile amesema wamepokea maelekezo na maagizo yote kwamba watayafanyia kazi kwa kusirikiana na wajumbe wa bodi hiyo na Menejimenti na kwamba hawatafanyakazi kwa mazoea.





 

KIVUKO CHA MV. MAFANIKIO KUREJEA MTWARA BAADA YA WIKI TATU

 

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akimuonyesha kitu Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Khalid Songoro kulia wakati wakikagua moja ya milango ya kivuko cha MV. MAFANIKIO kinachofanyiwa ukarabati na Kampuni ya Songoro Marine katika yadi yake iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara kinatarajiwa kurejea Mtwara baada ya wiki tatu kuendelea kutoa huduma. Katikati ni Mkuu wa Kivuko Magogoni Kigamboni Mhandisi Samuel Chibwana

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle (wa tatu kushoto) akizungumza jambo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Khalid Songoro (wa tatu kulia) wakati akikagua maendeleo ya kivuko cha MV. MAFANIKIO ambacho kimeletwa katika yadi ya Songoro Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati. Kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara kinatarajiwa kurejea Mtwara baada ya wiki tatu kuendelea kutoa huduma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Khalid Songoro (wa pili kulia) na Mkuu wa Kivuko Magogoni Kigamboni Mhandisi Samuel Chibwana kulia wakikagua kivuko cha MV. MAFANIKIO kinachofanyiwa ukarabati na Kampuni ya Songoro Marine katika yadi yake iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara kinatarajiwa kurejea Mtwara baada ya wiki tatu kuendelea kutoa huduma.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Khalid Songoro akimuonyesha kitu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle wakati akikagua kivuko cha MV. MAFANIKIO kinachofanyiwa ukarabati na Kampuni ya Songoro Marine katika yadi yake iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kivuko hicho kinachotoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara kinatarajiwa kurejea Mtwara baada ya wiki tatu kuendelea kutoa huduma. Kulia ni Mkuu wa Kivuko Magogoni Kigamboni Mhandisi Samuel Chibwana

 

PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA DAR ES SALAAM)

*****************************

Huduma za Kivuko kwa wakazi wa Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara zinatarajiwa kurejea baaada ya takribani wiki tatu kutoka sasa, hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle leo wakati alipotembelea eneo la Yadi ya Songoro Marine Kigamboni jijini Dar es Salaam kukagua maendeleo ya ukarabati huo unaofanywa na kampuni ya Songoro.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kukagua ukarabati wa kivuko hicho, Mtendaji Mkuu Maselle amesema kivuko hicho kipo mbioni kukamilika kwani Mkandarasi ametakiwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya muda mfupi ili wakazi wanaotegemea kivuko hicho Mkoani Mtwara waweze kurejeshewa huduma zake mapema iwezekanavyo.

‘’Tumekisafirisha kivuko hiki kutoka Mtwara kuja hapa Dar es salaam kwakuwa ni gharama ndogo kukileta hapa kuliko kusafirisha vifaaa vyote vya matengenezo kwenda kufanyia Mtwara ndio maana mkandarasi akaamua kukivuta kivuko hiki kije hapa ili muda wa matengenezo uwe mfupi zaidi’’.

Mhandisi Maselle amesisitiza kuwa utaratibu wa kufanya matengenezo kwa vivuko vya TEMESA ni muhimu sana kwa vyombo vya maji kwakuwa maji ya bahari yana chumvi nyingi na kali hivo kama kivuko kitakuwa hakijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu kitakuwa kinaharibika na kitashindwa kufanya kazi kwani chuma chake kitaliwa na maji ya chumvi na hivyo kushindwa kudumu kwa muda mrefu.

‘’Ni utaratibu wa kawaida kwa TEMESA kila ambapo kivuko kinafikia muda wake wa matengenezo kinga, lazima kitolewe na kupelekwa kufanyiwa ukarabati na matengenezo na hii ni hatua mojawapo ambayo tumefanya na tunaendelea na ukarabati wa vivuko vingine  ambavyo muda wake wa ukarabati umefika’’. Alisema Mhandisi Maselle ambapo amewaomba wakazi wa Mtwara wavumilie wakati kivuko hicho kikiendelea kufanyiwa ukarabati ambapo wakazi hao wamepelekewa boti mbili za MV. TANGAZO na MV. KUCHELE ambazo zinatoa huduma kwa sasa kwa wakazi hao.

 Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Khalid Songoro akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya tukio hilo la ukaguzi amesema, ukarabati wa kivuko hicho umefikia asilimia 85% na ameongeza kuwa wanatarajiwa kumaliza ukarabati wake ifikapo Tarehe 15 mwezi Agosti.

‘’Kazi kubwa zote tulizozifanya ziko kwenye hatua ya mwisho ili kuweza kukamilisha ukarabati wa kivuko hicho,’’ amesema Songoro.

Kivuko cha MV. MAFANIKIO kina uwezo wa kubeba abiria 100 na magari 6 sawa na tani 50 na kinatoa huduma zake kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara mjini.