Mkurugenzi
Mkuu wa Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Dkt. Hussein
Mansoor (kushoto) kwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya INDO
Power Solutions ya nchini Kenya, Bw. Brian Mutembei (kulia) wakisaini
Mkataba wa mauziano ya korosho ghafi kiasi cha tani laki moja kwa malipo
ya Shilingii bilioni 418. Wanaoshuhudia tukio hilo muhimu ni Prof.
Palamagamba Kabudi (wa pili kushoto), Waziri wa Katiba na Sheria, Joseph
Kakunda (kushoto), Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Innocent
Bashungwa (wa pili kulia), Naibu Waziri wa Kilimo na Dan Kazungu, Balozi
wa Jamhuri ya Kenya nchini. Tukio hilo lilifanyika kwenye Ukumbi wa
mikutano uliopo Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha
tarehe 30 januari 2019. Mawaziri hao wapo jijini humo kwa ajili ya
kushiriki Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Dkt. Mansoor na Bw. Mutembei wakibadilishana Mkataba huo mara baada ya kusaini
Prof.
Kabudi akizungumza kabla ya kuanza kwa tukio hilo la kihistoria la
kusainiwa mkataba wa ununuzi wa tani laki moja za korosho ghafi
Kakunda nae akizungumza
Dkt. Bashungwa akizungumza mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani)
Balozi
wa Kenya nchini, Kazungu akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi ya
kusainiwa mkataba wa ununuzi wa tani laki moja za korosho kutoka
Tanzania
Bw. Mutembei nae akieleza furaha yake katika kukamilisha ununuzi wa korosho kutoka Tanzania
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Joseph Buchweshaija
akizungumza kwa ufupi kuhusu hafla hiyo ya uwekaji saini mkataba wa
ununuzi wa korosho. Wengine katika picha ni Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania, Prof. Florens Luoga ( kulia walioketi) akifuatiwa na Prof.
Sifuni Mchome, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria na Dkt.
Evaristo Longopa, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mkutano ukiendelea. Kushoto ni Mkurugenzi wa TanTrade, Bw. Edwin Rutageruka
Serikali
ya Tanzania kupitia Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko
imesaini mkataba wa mauzo ya korosho ghafi kiasi cha tani laki moja kwa
Kampuni ya Kenya ya INDO Power Solutions kwa malipo ya Shilingi bilioni
418.
Mkataba
huo umesainiwa jijini Arusha tarehe 30 Januari 2019 kati ya Mkurugenzi
Mkuu wa Bodi hiyo Dkt. Hussein Mansoor kwa niaba ya Serikali ya Tanzania
na Bw. Brian Mutembei, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya INDO Power
Solutions ya nchini Kenya.
Tukio
hilo la kihistoria lilishuhudiwa na Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa
Katiba na Sheria, Joseph Kakunda, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt.
Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Kilimo, Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania, Prof. Florens Luoga, Dkt. Evaristo Longopa, Naibu Mwanasheria
Mkuu wa Serikali,
Viongozi
wengine walioshuhudia ni Balozi wa Kenya nchini, Dan Kazungu, Prof.
Sifuni Mchome, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Joseph
Buchweshaija, Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, Prof. Siza Tumbo,
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Edwin Rutaberuka, Mkurugenzi
wa TanTrade, Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini na Waandishi wa
Habari.
Awali
wakizungumza kabla ya kusainiwa kwa Mkataba huo Mawaziri hao
wakiongozwa na Prof. Kabudi, kwa pamoja walipongeza kwa dhati uamuzi wa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
wa Serikali kununua korosho kutoka kwa wakulima ili kuepusha wakulima
hao kuuza korosho zao kwa bei ya chini kwa watu wasio kuwa na nia njema
kwa wakulima. Itakumbukwa kuwa, mwezi Novemba 2018, Rais Magufuli alitoa
maelekezo kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara
ya Kilimo waratibu zoezi la ununuzi wa korosho kutoka kwa wakulima kwa
shilingi 3,300 kwa kilo moja.
Kwa
upande wake Prof. Kabudi alisema kuwa anampongeza Rais Magufuli kwa
uamuzi huo wa Serikali kununua korosho yote ili wakulima wapate bei
inayolingana na jasho lao ambao hatimaye umezaa matunda kwa faida na
maendeleo ya nchi.
Naye
Kakunda alieleza kuwa Bw. Mutembei ni mnunuzi wa kwanza kati ya wengi
ambao walikuwa kwenye mazungumzo na Serikali kuhusu ununuzi wa korosho
hizo. Kakunda alisema katika majadiliano Serikali iliangalia kufanya
biashara ya faida ambayo itawezehsa kulipa gharama mbalimbali ikiwemo
gharama za upakiaji na upakuaji, malipo kwenye Serikali za Mtaa na
michango mingine ya kijamii kwa mujibu wa makubaliano. Hivyo aliwataka
watanzania na wenye viwanda kutokuwa na wasiwasi kwani Serikali ina nia
njema ya kuwaletea maendeleo wananchi hususan kupitia sekta ya kilimo
cha korosho.
“Wakulima
wa Korosho wanatakiwa kumshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi wake ambao
unalinda maslahi ya mkulima na umewawezesha kuuza korosho zao kwa faida.
Nawakaribisha wafanyabiasha makini kuja nchini kwani Serikali ipo
tayari kuwasikiliza watu wa aina hiyo na kufanya nao biashara” alisema
Kakunda.
Kwa
upande wake, Bashungwa alieleza kuwa katika msimu wa korosho wa mwaka
2018/2019 tayari zimekusanywa tani 213,159 ambazo kati ya hizo tani
126,194 zimehakikiwa na tayari wakulima wa mikoa ya Lindi, Mtwara,
Ruvuma na Pwani wamelipwa fedha zao kwa zaidi ya asilimia 95.5.
Bashungwa aliongeza kuwa, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha Wakulima
wote kulipwa fedha zao hadi kufikia tarehe 05 Februari 2019.
Akizungumza
wakati wa tukio hilo, Balozi wa Kenya nchini, Kazungu alisema kuwa
kusainiwa kwa mkataba huo ni faraja kubwa kwake katika historia ya
mahusiano kati ya Tanzania na Kenya ambayo yanaendelea kuimarika siku
hadi siku. Aidha, alieleza kuwa mkataba huo ni mfano mzuri wa kuimarika
kwa mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hususan katika masuala ya
kilimo na biashara.
Kwa
upande wake, mnunuzi wa korosho hizo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya Indo Power Solutions, Bw. Mutembei alisema amekuja kuunga
mkono jitihada za Rais Magufuli za kumwinua mkulima wa Tanzania na
kwamba anawataka wale wote wanaobeza jitihada hizo za Rais Magufuli
kuacha mara moja huku akilaani kitendo cha baadhi ya wafanyabiashara
kuendelea kuwakandamiza wakulima kwa kununua mazao yao kwa bei ndogo
wanazopanga wao huku wakijua wazi kuwa wakulima hao wametumia gharama
kubwa katika uzalishaji wa mazao hayo.
Pia
aliwataka wafanyabiashara kufuata taratibu na sheria katika kufanya
biashara kama Serikali zinavyoelekeza na kuacha kuchanganya biashara na
siasa.
Naye
Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka, Dkt. Mansoor alieleza kufurahishwa na
tukio hilo ambalo limekuja wakati mwafaka wakati nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki zikijiandaa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi
utakaofanyika jijini humo hivi karibuni. Aidha alisema kuwa, kwa kiasi
kikubwa tukio hilo limeiinua Bodi yake na kwamba anatoa wito kwa
wafanyabiasha wengine wa ndani na nje ya Tanzania kuja nchini na
kushirikiana na Bodi hiyo ili kuwakomboa wakulima wengi Zaidi.
No comments:
Post a Comment