Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma (hawapo pichani) alipofanya ziara ya kikazi
katika ofisi ya Sekretarieti hiyo jijini Dodoma kwa lengo la kuhimiza
uwajibikaji. Kushoto ni Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi
wa Umma, Jaji Mst. Harold Nsekela.
Kamishna
wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mst. Harold
Nsekela (kushoto) akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa
(Mb) kuhusu majukumu ya ofisi yake wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri
huyo na Menejimenti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,
alipoitembelea ofisi hiyo kuhimiza uwajibikaji jijini Dodoma.
Baadhi
ya watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) wakati
wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi hao cha kuhimiza
uwajibikaji kilichofanyika katika ofisi ya Sekretarieti hiyo jijini
Dodoma.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akitia saini kitabu cha wageni mara baada ya
kuwasili Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini
Dodoma kwa ajili ya kuhimiza uwajibikaji.
Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetakiwa kuwachukulia hatua kali za
kinidhamu viongozi wanaokula Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu na kutoa Tamko
la Rasilimali na Madeni lakini wanashindwa kutekeleza kiapo hicho.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akizungumza na
watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, alipofanya
ziara ya kikazi makao makuu ya ofisi hizo jijini Dodoma yenye lengo la
kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma na kujiridhisha namna inavyotekeleza wajibu
wake.
Dkt.
Mwanjelwa amesema, baadhi ya viongozi wamekuwa wakila Kiapo cha Ahadi
ya Uadilifu na kusoma Tamko la Rasilimali na Madeni lakini maisha na
tabia zao ni tofauti kabisa na viapo wanavyoapa, hivyo ameisisitiza
Sekretarieti ya Maadili kutumia sheria kuwawajibisha viongozi wa namna
hiyo kwani ni mzigo kwa taifa. Dkt. Mwanjelwa amesema viapo na matamko
ni lazima viendane na uhalisia, hivyo ameitaka Sekretarieti hiyo kufanya
ufuatiliaji na kuchukua hatua bila uwoga wowote kwa kiongozi anayeenda
kinyume kwani kiongozi wa namna hiyo anakosa sifa ya kuwa kiongozi
bora.
Dkt.
Mwanjelwa amesema ni lazima kuunga mkono kwa vitendo jitihada za
Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na viongozi ambao hawana maadili
mema ili kuleta maendeleo kwa taifa. Aidha,
Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa Sekretarieti hiyo kuishi na
kufanya kazi katika maadili mema ili wawe mfano kwa wanaowasimamia
katika suala zima la maadili. “Ni
lazima maadili mema yaanzie kwetu sisi ili tunapozungumza na kutoa
elimu ya maadili kwa viongozi tuwe kioo kwani huwezi ukazungumzia
maadili kwa viongozi kama wewe mwenyewe huna maadili, hivyo ni lazima
kuonyesha mfano,” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Awali,
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu, Harold Nsekela amesema, Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma ilianzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 132 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuchunguza tabia
na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha
kwamba masharti ya Sheria ya Maadili ya viongozi wa umma yanazingatiwa
ipasavyo.
Nsekela
ameyataja majukumu ya Sekretarieti kuwa ni pamoja na kupokea matamko ya
viongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni yanayopaswa kutolewa kwa
mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kuanzisha na kufanya
uchunguzi wowote kuhusu ukiukwaji wa maadili yaliyotajwa na Sheria,
kupokea na kushughulikia malalamiko na taarifa za ukiukwaji wa maadili
kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoka kwa wananchi
na kufanya uhakiki wa Tamko la Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma
wanaotajwa na Sheria.
Nsekela
ameyataja baadhi ya matarajio ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma kuwa ni kujenga na kuimarisha maadili ya kitaifa na kuyafanya yawe
sehemu ya jamii ili kuzuia mmomonyoko wa maadili katika nchi kwa
kujumuisha somo la maadili katika mitaala kuanzia shule za msingi hadi
vyuo vikuu, kufanya marekebisho ya Sheria zinazohusu ukuzaji wa maadili
nchini ikiwemo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na kutungwa
kwa Sheria ya Kudhibiti Mgongano wa Maslahi.
No comments:
Post a Comment