Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali haitomvumia mtu yeyote
atakayebainika kuhujumu mkakati wake wa kulifufua zao la michikichi
nchini.
Amesema
wanataka kuona wakulima zao hilo wakinufaika kama wengine wa mazao
makuu ya biashara, hivyo haitomfumbia macho mtu atakayezembea.
Aliyasema
hayo jana jioni (Jumapili, Februari 17) mara baada ya kukagua shamba la
michikichi la kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Bulombora.
Alisema Serikali inataka kuona wakulima wa zao hilo wakinufaika kama
ilivyokuwa kwa wakulima wa korosho, chai, kahawa, pamba na tumbaku.
Alisema
Serikali imeamua kulifufua zao hilo kwa lengo la kumaliza tatizo la
upatikanaji wa mafuta ya kula kwani inatumia fedha nyingi kuagiza nje ya
nchi. Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi mkoani Kigoma
kwamba suala la kilimo cha michikichi liwe ajenda ya kudumu kwenye vikao
vyao.
Kadhalika,
Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Kilimo ianzishe shamba darasa la zao la
michikichi ili wananchi waweze kujifunza mbinu bora za kulima zao hilo.
Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba alisema Serikali imetenga
zaidi ya sh. bilioni 10 kwa ajili ya kuboresha kilimo cha zao la
michikicho.
Waziri
huyo alisema kiasi hicho cha fedha kimetengwa katika bajeti ya wizara
hiyo ya mwaka 2019/2020 kwa ajili ya kuboresha kilimo cha michikichi
nchini. Alisema iwapo kilimo cha zao hilo kitaboreshwa kitasaidia
Serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni zilizokuwa zikitumika kuagiza
mafuta kutoka nje ya nchi.
Pia,
Waziri Mgumba alisema tayari wizara hiyo imeshaongeza watafiti zaidi ya
10 wa zao la michikichi katika kituo cha utafiti wa zao hilo cha
Kihinga. Waziri Mgumba alipongeza Jeshi la Magereza na JKT kwa
ushirikiano wanaoutoa kwa wizara katika kipindi hiki cha ufufuaji wa zao
la michikichi.
Naye
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi
alimuhakikishia Waziri Mkuu kuwa maelekezo yote aliyoyatoa kuhusu kilimo
cha michikichi watayatekeleza.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa,
Meja Jenerali , Martin Busungu wakati alipowasili kwenye Kambi ya JKT
ya Bulombora wilayani Uvinza, kuhamasisha ufufuaji wa zao la michikichi,
Februari 17, 2019. Wapili kulia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe Mary (kushoto) wakitazama sabuni
zinazotengenezwa na Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa katika Kambi ya
Bulombora wilayani Uvinza wakati alipotembelea kambi hiyo kuhamasisha
ufufuaji wa zao la michikichi, Februari 17, 2019. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasha trekta ikiwa ni ishara ya kuzindua
trekta hilo katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Bulombora wilayani
Uvinza, Februri 17, 2019. Mheshimiwa Majaliwa yuko mkoani Kigoma kwa
ziara yenye lengo la kuhamasisha ufufuaji wa zao la michikichi. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akipanda mchikichi ikiwa ni ishara ya kuzindua
upanuzi wa shamba la zao hilo katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya
Bulombora wilayani Uvinza, Februari 17, 2019. Mheshimiwa Majaliwa yuko
mkoani Kigoma kwa ziara yenye lengo la kuhamasisha ufufuaji wa zao la
michikichi.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment